loader
Picha

Matumizi ya fedha mkoani Songwe yalivyomkosha JPM

AKIWA ziarani katika Mkoa wa Songwe hivi karibuni, Rais John Magufuli alikoshwa na maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa nguvu za wananchi na kuuzawadia mkoa huo Sh bilioni 2.3 ili kukamilisha madarasa 1,510 yanayojengwa ndani ya miezi minne katika Halmashauri ya Mbozi.

Fedha hizo zimeokolewa na viongozi wa Mkoa wa Songwe katika ujenzi wa ofisi za mkoa huo uliokuwa umetengewa Sh bilioni 6.5 na serikali, lakini kutokana na usimamizi mzuri wa viongozi wa Mkoa Songwe, ujenzi huo ulitumia Sh bilioni 4.2 na hivyo, kuokoa Sh bilioni 2.3.

“Hiyo fedha iliyookolewa na viongozi wa mkoa huu katika ujenzi wa ofisi ya mkoa nawapongeza viongozi wote mkoani Songwe, hivyo hela siwezi kuipeleka sehemu nyingine naiacha hapa hapa ikamilishe hayo madarasa yaliyojengwa na wananchi ili wanufaike kwa kazi nzuri walioifanya,” akasema Rais Magufuli.

Akaongeza: “Pamoja na mkoa huu kuwa mpya, lakini unafanya vizuri sana katika uzalishaji na usimamizi wa miradi, wangekuwa viongozi wengine wangeficha hizo hela zilizobaki, halafu wangeomba na fedha nyingine” anasema Rais.

Gazeti hili lilizungumza na Mchumi wa Mkoa wa Songwe, Halima Mpita aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi ndani ya miezi minne ili kujua namna walivyofanikiwa kujenga madarasa 1,510 na matundu 2,400 ya vyoo kwa nguvu za wananchi hadi Rais kuzawadiwa Sh biloni 2.3.

Mchumi huyo anasema, takwimu zinaonesha kuwa Halmashauri ya Mbozi pekee ina uhaba wa matundu ya vyoo 2566, wakati huo takwimu zikionesha Mkoa wa Songwe ukiwa nafasi ya 23 kufanya vibaya kwa upande wa vyoo kati ya mikoa 26 nchini. Uhaba wa vyumba vya madarasa ukiwa ni zaidi ya vyumba 1200 kwa shule za awali na msingi.

Anasema Mei 23, mwaka huu walianza kutekeleza shughuli mbalimbali muhimu baada ya yeye kukabidhiwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na Mkuu wa Mkoa wa Songwe kama Kaimu Mkurugenzi.

Kwamba, jambo la kwanza lilikuwa kutengeneza ushirikiano mkubwa kati ya viongozi, watumishi na wananchi hali iliyosababisha kwa kiasi kikubwa, kupata madarasa mengi na matundu ya vyoo kwa muda mfupi.

“Kutokana na uhaba wa madarasa na matundu ya vyoo uliokuwa ukiikumba Halmashauri yetu tuliamua kuanzisha operesheni tuliyoiita ‘Operesheni Tokomeza Uhaba wa Matundu ya Vyoo na Uhaba wa Madarasa’ ya awali na shule za msingi huku viongozi wa Halmashauri tukihamishia ofisi katika kata na vijiji vya Mbozi kutoa elimu kwa wananchi,” anasema Mpita.

Anasema thamani ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa inakadiriwa kuwa Sh bilioni 3.6, wakati huo huo matundu 2,400 yakichimbwa na kujengwa kufikia hatua mbalimbali huku mengi yakiwa yameanza kutumika.

Mpita anasema: “Tunamshukuru Rais wetu (John Magufuli) kwa kuona juhudi zetu na kutuzawadiaSh bilioni 2.3 kwa ajili ya kupaulia madarasa yetu yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi ndani ya miezi minne tu, baada ya wananchi kupewa elimu ya kutosha.”

Aidha mchumi huyo anasema, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi pia kwa muda mfupi imeweka historia ya kuwa ya kwanza kitaifa kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka asilimia 93 na kufikia asilimia 171 kufikia Juni 2019.

MKUU WA MKOA ANAFAFANUA

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nicodemas Mwangela katika kikao cha watendaji wa sekta ya elimu hivi karibuni, anasema fedha walizozawadiwa na Rais Magufuli baada ya usimamizi mzuri wa ujenzi wa ofisi ya Mkoa kuwa zitatumika kwa shule zilizokamilisha madarasa kufikia hatua rinta tu. Anasema Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ndiyo itanufaika zaidi kutokana na kujenga madarasa kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na halmashauri nyingine za Mkoa wa Songwe.

“Fedha zikishaingia tutanunua mabati kwa ajili ya kukamilisha maboma yaliyojengwa na wananchi ambapo maboma 1,510 yanapatikana katika Halmashauri ya Mbozi, kwa hili, Halmashauri ya Mbozi kupitia watendaji wake wamefanya vizuri sana hivyo watakuwa wanufaika wakubwa kutokana na fedha hizo,” anasema Mkuu wa Mkoa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Elick Ambakisye anasema kutokana na changamoto ambazo Halmashauri ya Mbozi ilikuwa nazo katika miundombinu ya madarasa na vyoo katika shule za awali na kata wakishirikiana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na Mkuu wa Wilaya waliamu kupeana majukumu mazito yaliyowawezesha kuhamishia ofisi zao katika Vijiji vya Halmashauri ya Mbozi kufanya mikutano ya kuhamasisha na kutoa elimu.

“Baada ya kuunda timu na kupeana majukumu, tuliitisha vikao vilivyojumuisha madiwani 43, watendaji kata 29, waratibu kata 29, watendaji wa vijiji, wenyeviti wa vijiji 121 na wakuu wa idara wanne, lengo letu likiwa kufikisha elimu kwa wananchi ambao ni wahusika wakuu ambapo lilipokelewa vizuri licha ya sehemu nyingine kupata changamoto ambazo zilitatuliwa baada ya viongozi kufanya mikutano ya hadhara,” anasema Ambakisye.

Aidha, Ambakisye anasema walikutana na changamoto ya baadhi ya wanasiasa kuhusisha mikakati hiyo ya maendeleo na mambo ya siasa jambo lililosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kukamilisha ujenzi kwa muda uliopangwa.

“Kwa kuwa shughuli hii muhimu tumeifanya mwaka huu ambao ni mwaka ambao ni mwaka wa maandalizi kwa ajili ya uchaguzi mwakani, wanasiasa wengi wamekuwa wakikwamisha maendeleo kwa kuingiza mambo ya siasa,” anasema Ambakisye.

WANANCHI WANENA

“Tunajivunia ubunifu uliofanywa na viongozi wetu wa Halmashauri wakiongozwa na Halima Mpita aliyekuwa Mkurugenzi kwa kutushirikisha katika shughuli muhimu za maendeleo mpaka Rais akatuzawadia nadhani, baada ya miaka kadhaa hivi halmashauri yetu itakuwa mfano zaidi kwani kwa muda mfupi tumefanya vizuri na kukuza uchumi na heshima ya Wilaya ya Mbozi,” anasema Keneth Nzunda, kazi wa Kata ya Hasamba wilayani Mbozi.

Naye Jose Haonga anasema wananchi wengi walikuwa wanashindwa kushiriki kwenye miradi ya maendeleo kutokana na kukosa elimu kuhusu umhimu wa kuboresha miundo mbinu katika shule zinazowazunguka na faida zake.

“Maeneo ambayo elimu ilifika vizuri wananchi walihamasika vizuri katika ujenzi na kukamilisha ujenzi wa madarasa kwa muda mfupi, lakini sehemu nyingine mambo ya siasa na elimu kutotolewa na viongozi wa kata na mitaa kumepelekea kutokamilika baadhi ya vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Namile na Shule ya Msingi Muungano,” anasema Haonga.

Naye Ofisa Elimu wa Mkoa wa Songwe, Juma Kaponda anasema ujenzi wa madarasa kwa kiasi kikubwa ili kutatua changamoto ya wanafunzi wa awali na darasa la kwanza kupokezana darasa moja hali iliyokuwa inakwamisha ujifunzaji mzuri kutokana na wengine kulazimika kuingia mchana.

“Ili kuboresha ujifunzaji hasa kwa watoto wa awali wanatakiwa kutengewa darasa lao ambao huwa na zana mbalimbali za kufundishia, lakini kutokana na uhaba wa madarasa ilikuwa inatulazimu kutumia madarasa ya wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili,” anasema Kaponda.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Baraka Messa

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi