loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Askofu Shao aipongeza SMZ kwa elimu bure

VIONGOZI wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wamepongezwa kwa juhudi zao kubwa za kuendelea kutoa huduma muhimu za jamii kwa wananchi wake bila malipo, ikiwamo elimu ya sekondari na matibabu.

Akisoma salamu za Krismasi katika Kanisa la Minara Miwili, Askofu Mkuu wa Kanisa la Katoliki Zanzibar, Augustine Shao alisema anaunga mkono juhudi zinazochukuliwa katika kuwapatia wananchi huduma muhimu za jamii ikiwemo matibabu bure na elimu ya msingi na sekondari. Askofu Shao alisema mafanikio hayo yote, yamekuja kwa kudhibiti fedha za umma na kupambana na ufisadi na rushwa katika sehemu za kazi.

“Serikali yetu imepiga hatua kubwa na kufanya mambo makubwa kwa maslahi ya taifa letu ambapo tunajionea wananchi wanavyopata huduma za afya bure, elimu hadi ya msingi na sekondari,” alisema.

Aidha, Askofu Shao aliitaka serikali na taasisi zake, kulipatia ufumbuzi tatizo la upatikanaji wa rasilimali ya mchanga, ambalo limewafanya wananchi kushindwa kuendeleza shughuli zao za ujenzi na makaazi. Alisema kanisa linaunga mkono juhudi zinazochukuliwa katika kutunza mazingira na uharibifu wake ili kukifanya kisiwa cha Zanzibar kuwa salama.

“Lipo tatizo la uhaba wa mchanga linalowakabili wananchi wetu...tunataka lifanyiwe kazi huku suala la kutunza mazingira likizingatiwa kwa kiwango kikubwa,” alisema Askofu Shao.

Suala la amani Askofu wa Kanisa la Anglikana Mkunazini Unguja, Dk Michael Hafidh aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Ali Mohamed Shein kwa kuimarisha amani na utulivu katika kipindi chote. Alitaka juhudi za kulindwa amani ziongezwa zaidi huku taifa likielekea katika kipindi kigumu cha harakati za Uchaguzi Mkuu mwakani.

“Sisi Wakristo wa Zanzibar tunaridhishwa na juhudi za kulinda amani na utulivu chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein ambapo tunataka mkazo zaidi wa kulinda amani katika kipindi kigumu tunachoelekea cha Uchaguzi Mkuu wa mwakani,” alisema Dk Hafidh.

Aidha, aliwataka wananchi wakiwamo Wakristo, kutumia nafasi ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya kutumia haki yao ya kikatiba. Alisema huwezi kupiga kura na kuchagua viongozi wakuu wa serikali kama utashindwa kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.

“Huo ndiyo wito wetu... watu waliokuwa hawajaandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura waitumie nafasi hiyo...ndiyo neema kutoka kwa Rais Shein,” alisema.

Dk Hafidh aliwaasa wafuasi wa dini ya Kikristo, kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuwafanya watoto kuwa salama wenye amani. Alisema matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, vinatishia amani ya jamii ya wanawake na watoto huku vikimchukiza kwa kiwango kikubwa bwana Mungu.

“Nasikitishwa sana na wimbi la matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa jamii yetu huku watoto na wanawake chini ya umri wa miaka 18 wakiathirika vibaya,” alisema.

Ibada ya sikukuu ya Krismasi ilifanyika katika makanisa yote, ikiwemo yaliyopo vijijini kwa utulivu mkubwa. Wakristo huadhimisha sikukuu ya Krismasi kukumbuka kuzaliwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi