loader
Picha

Wasiolipa kodi kuadhibiwa

MAMLAKA ya Mapato (TRA) mkoani Dodoma, imewakumbusha walipa kodi kuhakikisha wanafuata taratibu zote za kulipa kodi na kufanya zoezi hilo kwa wakati ili wasipate usumbufu wa kisheria.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja Msaidizi (Madeni), Castro Angelo wakati akizungumzia wajibu wa walipa kodi na ukusanyaji wa madeni ya TRA mkoani hapa, hasa kodi ya mapato kwa wanaokadiriwa ambayo mwisho ni Desemba 31.

Angelo alisema mwezi huu ndio mwezi wa mwisho kwa walipa kodi wanaokadiriwa, kulipa awamu yao ya mwisho kabla ya Desemba 31 na kutofanya hivyo kutasababisha riba na adhabu.

Alisema kutokulipa kodi ni kinyume cha sheria, hivyo ni muhimu wafanyabiashara wazingatie ulipaji wa kodi. “Sio watu wa mapato tu, bali wapo watu wa VAT ambao wamewasilisha nyaraka zao lakini hawajalipa.

Pia wapo watu wa ushuru, mabango na majengo,” alisema Angelo na kusisitiza kwamba watakaochelewa, watapata adhabu kwa mujibu wa sheria.

Amesema ni wajibu wa mamlaka kukumbusha walipa kodi kuhusu wajibu wao ili wakwepe adhabu na riba.

Akizungumzia walipaji wanaotekeleza mkataba wa msamaha wa riba na adhabu, Angelo alisema ni vyema wakafanya kwa mujibu wa mkataba ili wasije kulazimika kulipa riba kwa kuchelewa kutekeleza mkataba.

Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Julai mwaka huu ilitunga sheria iliyotoa nafasi kwa wafanyabiashara kuongezewa muda wa kulipa kodi ili kuwapatia unafuu kwa wenye malimbikizo ya madeni ya riba na adhabu, kwa kuwapa fursa ya kulipa madeni msingi ya kodi.

“Kwa mfano kama ulikuwa unadaiwa malimbikizo ya shilingi milioni 100 kama usipolipa kwa mujibu wa makubaliano, utalipa hiyo uliyosamehewa na deni la msingi, hivyo ni vyema waliofaidika na msamaha huo wakatekeleza wajibu wao,” alisema Angelo.

Angelo pia alisema mamlaka hiyo mkoani Dodoma, itaingia mitaani kuhakikisha risiti za EFDs zinatumika katika manunuzi na kuwataka wateja kudai risiti na wauzaji kutoa risiti. “Tutaingiza timu ya maofisa wetu mitaani kuangalia kwamba sheria inatekelezwa na kodi ya serikali inakusanywa,” alisema Angelo.

Amesema wauzaji wamejisahau na kurejea katika desturi ya kutotoa risiti ya EFDs, akisema ni wajibu wao kutoa risiti kwa kila kitu wanachokiuza, huku akizungumzia kwa upande wa wanunuzi kuwa nao kuwajibika kudai risiti.

“Kwa kile wanachonunua kutokudai risiti na kutotoa risiti ni uvunjifu wa sheria na hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa muuzaji ameuza bila kutoa risiti au mnunuzi amenunua bidhaa bila kudai risiti,” amesema Angelo.

Akizungumzia kodi ya majengo na mabango, aliwataka wananchi kwenda kulipa mapema na wasisubiri mpaka tarehe za mwishoni ili kuweza kuokoa muda. Lakini, kwa wale ambao hawajajiandikisha, wanatakiwa kwenda TRA kujiandikisha ili nao waweze kulipa kodi zao.

WAFANYABIASHARA wa mchele mkoani hapa wameomba kuwepo kwa soko la ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi