loader
Picha

JPM ashusha presha ya mamilioni

RAIS Dk John Magufuli amesajili laini yake ya simu kwa alama za vidole na ameongeza siku 20 baada ya Desemba 31 kwa yeyote ambaye atakuwa hajasajili.

Amesisitiza kuwa muda huo ukiisha, laini zote zitakazokuwa hazijasajiliwa, zitafungwa. Awali, mwisho wa kusajili laini uliowekwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikuwa ni Desemba 31 mwaka huu. Hata hivyo, mpaka katikati ya Desemba, wateja milioni 19.6 pekee ndio walikuwa wamesajili laini zao kwa mfumo huo kati ya milioni 47 wenye laini za simu nchini.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, Chato na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa Rais Magufuli aliongeza muda huo wakati akizungumza na wananchi, baada ya kusajili laini yake ya simu kwa alama za vidole jana Chato Mjini mkoani Geita. Alisisitiza kuwa baada ya muda huo, hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika, kwa atakayekuwa hajasajili kwa mfumo huo.

Aliagiza TCRA kuhakikisha laini ambazo hazijasajiliwa, zinazimwa baada ya muda huo. Aidha, taarifa hiyo ilieleza pia kuwa Rais ameongeza siku 20 za usajili, ili kuwawezesha wananchi ambao watakuwa hawajasajili laini zao kwa alama za vidole hadi Desemba 31, mwaka huu kwa sababu mbalimbali, waweze kufanya hivyo.

“Lakini kwa wale Watanzania wengine waliokuwa wamelazwa hospitalini wamechelewa, wengine walikuwa wanasherehekea vizuri sherehe, wamejisahau kidogo kusajili laini zao, lakini wapo wengine walikuwa hawajaelewa maana ya kusajili, lakini kupi- tia wito huu watakuwa wameelewa, nimeongeza siku ishirini,” alisema Rais.

Siku alizoongeza Rais Magufuli ni kuanzia Januari Mosi hadi Januari 20, 2020. Nyongeza hiyo kama alivyoeleza Rais Magufuli ni kwa wote watakaoshindwa kusajili laini zao katika kipindi cha kuishia Desemba 31, 2019, kama ilivyotangazwa na TCRA kutokana sababu mbalimbali zikiwemo kuugua na kukamilisha upataji wa Namba ama Vitambulisho vya Taifa.

“Wale ambao watakuwa hawajasajili laini zao, naomba TCRA wahusika wote wakate mawasiliano,” alisisitiza Rais Magufuli.

Magufuli alisisitiza kuwa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni muhimu kwa usalama wa nchi, ikiwemo kuepusha vitendo vya utapeli na ujambazi vinavyofanywa na wahalifu, ambao licha ya wengi wao kukamatwa na vyombo vya dola wameendelea kusababisha usumbufu na upotevu wa mali za wananchi hususani fedha.

Rais pamoja na kuwasalimu wananchi wa Chato Mjini waliojitokeza kushuhudia akijisajili, alisikiliza maoni yao kuhusu zoezi hilo la usajili. Aidha, mwananchi Steven Wandwi anayefanya biashara ya kuuza chipsi na mishikaki, aliwaongoza wenzake kumuombea Rais Magufuli na kumshukuru kwa utumishi wake mzuri, ulioongeza kasi ya maendeleo kwa taifa, hasa vijana ambao sasa wanachapa kazi bila bughudha.

Kabla ya kwenda kusajili laini yake ya simu, Rais Magufuli alitembelea Mtaa wa Chato Kati na kutoa pole kwa familia ya Atanasi Mnaku, aliyefariki dunia juzi na mazishi yake yamepangwa kufanyika kesho.

Kabla ya kauli hiyo ya Rais Magufuli ya kuongeza muda wa kusajili laini za simu kwa alama za vidole, baadhi ya viongozi akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alieleza Bungeni kuwa hakuna mwananchi atakayefungiwa laini yake ya simu Desemba 31 mwaka huu.

Lugola aliziagiza mamlaka zinazohusika na utoaji wa vitambulisho muhimu vya kuwezesha mtu kusajiliwa, ikiwamo vyeti vya kuzaliwa vinavyotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na Kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuongeza kasi ya utendaji ili kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa anajisajili.

Katika mitandao ya kijamii jana baada ya taarifa ya Rais kuongeza muda kutolewa, wananchi walionekana kufurahia hatua hiyo. Walieleza kuwa Rais Magufuli wakati wote amekuwa akiwafikiria wananchi wanyonge na kumshukuru kwa kuongeza muda. Wengine waliandika katika makundi ya mtandao wa Whatsapp, wakihimizana kutouchezea muda ulioongezwa.

Baadhi walilaumu mtindo wa Watanzania wengi, kusubiri dakika za mwisho agizo linapotolewa, kuwa siyo mzuri. Baadhi walizilaumu taasisi zinazotoa vitambulisho, kwa kufanyakazi kwa kasi ndogo na kutaka kila mmoja ahakikishe lengo la kusajili wateja wote wenye laini, linafikiwa kwa muda alioongeza Rais, kwani ni kwa mustakabali wa maendeleo ya kampuni za simu, wananchi na uchumi wa nchi nzima.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi