loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Japan yamwaga mabilioni kufufua TAFICO

SERIKALI imesaini mkataba na Serikali ya Japan wa kupokea msaada wa fedha za Kijapan Yen milioni 200, sawa na Sh bilioni 4.2 kwa ajili ya kulifufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), lililositisha shughuli zake tangu mwaka 1998.

Mkataba huo ulisainiwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James kwa upande wa Serikali ya Tanzania na kwa upande wa Serikali ya Japan, ulisainiwa na Kaimu Balozi wa Japan nchini, Katsutoshi Takeda. Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, James alisema fedha hizo ambazo ni msaada usiokuwa na masharti, zitatumika kwa ajili ya kuifufua TAFICO ikiwemo kununua meli mpya ya uvuvi yenye vifaa vya kisasa, mashine ya kutengeneza barafu, ghala la baridi la kuhifadhia samaki na vifaa vya kuvulia samaki na vya karakana, gari lenye mitambo maalum ya barafu na gari aina ya Pickup kwa ajili ya kusambazia samaki.

Alisema kufufuliwa kwa shirika hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kufufua mashirika yote yaliyokufa, ambayo serikali inaona bado yanahitajika katika kuchangia uchumi wa taifa, kama ilivyofanya kwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kiwanda cha Kubangua Korosho cha BUCCO mkoani Lindi walichokabidhiwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Kiwanda cha Chai cha Mponde mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa James, Japan wamekuwa marafiki wa kweli kwa maendeleo ya Tanzania, kutokana na misaada ya kifedha isiyokuwa na masharti na mikopo ya kifedha yenye masharti nafuu inayoitoa kwa Tanzania.

Alisema tangu mwaka 2012 mpaka 2019, misaada na mikopo yote ya Japan kwa Tanzania inafikia Sh trilioni 1.3 ikiwemo misaada yenye thamani ya Sh bilioni 451.31 na mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya Sh bilioni 891.

“Tunaishukuru serikali ya Japan kwa msaada huu ambao utasaidia kulifufua shirika letu la uvuvi la TAFICO ambalo liliharibika na kushindwa hata kubinafsishika, kufa kwa shirika hili kulifanya sekta ya uvuvi kuyumba na kusababisha samaki kama vile sato kutoka nchi za nje. Pia tunamshukuru Rais Dk John Magufuli kwa jitihada na miongozo yake ya kuhakikisha mkataba huu unasainiwa leo,” alisema Katibu Mkuu.

Aliongeza kuwa, “utekelezaji wa mradi huu utachangia kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya Pili (FYDP II), ambayo pamoja na mambo mengine unalenga kuboresha sekta ya uvuvi, kuongeza uuzaji wa samaki nje ya nchi, kuongeza uhakika wa chakula nchini, kuboresha usindikaji wa samaki, kuongeza thamani na masoko na kupunguza upotevu wa mazao ya samaki baada ya kuvua.”

Katibu Mkuu huyo alisema kiwango cha ukuaji kwa shughuli ndogo za kiuchumi za uvuvi, kilifikia asilimia 9.2 mwaka 2018 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 8.4 mwaka 2017.

Lakini, pia shughuli za uvuvi zilichangia asilimia 1.7 katika Pato la Taifa mwaka 2018. Hivyo, alisema msaada huo utasaidia jitihada za serikali katika kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, Malengo Endelevu ya mwaka 2030 na Agenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063.

Mbali na kuifufua TAFICO, James alisema serikali pia imeanza taratibu za kujenga bandari ya uvuvi katika mwambao wa Bahari ya Hindi. Alisema hivi sasa suala hilo liko kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na kukamilika kwake, kutaondoa bandari bubu zinazokwepa kodi ya serikali katika eneo hilo.

Japan

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Japan, Takeda, aliisifu serikali ya Tanzania kwa kutambua umuhimu wa rasilimali endelevu za baharini, ambazo ni muhimu kwa usalama wa chakula, fursa za ajira, kipato na maisha ya watu.

Takeda alisema kutokana na umuhimu huo, Japan iliamua kuidhinisha msaada huo wa fedha kwa ajili ya kuifufua TAFICO, lakini pia Japan imekuwa ikiisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile miundombinu ya barabara na madaraja, uzalishaji wa nishati na usambazaji, afya, maji, kilimo na nyinginezo kwa ajili ya kuimarisha ukuaji wa kiuchumi na kupunguza umaskini ili kuboresha maisha ya watu nchini.

TAFICO ilivyokufa

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Rashid Tamatamah alisema kuwa TAFICO ilifanya kazi kwa miaka 28 tangu ianzishwe mwaka 1974 na ilisimamishwa kufanya kazi mwaka 1998, kutokana na Sera ya Ubinafsishwaji ya mwaka 1996. Dk Tamatamah alisemaTume ya Kurekebisha Mashirika ya Sekta ya Umma (PSRC), iliiweka TAFICO kwenye orodha ya mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa. Ilipofika mwaka 1998 TAFICO waliambiwa wasimamishe shughuli zao na PSRC ilianza kumtafuta mnunuzi wa kulinunua shirika hilo.

“Kwa bahati nzuri au mbaya hakupatikana mnunuzi. Ilipofika mwaka 2005, PSRC ilishindwa na kulirudisha shirika hili kwa iliyokuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ili iendelee na mchakato wa kutafuta mnunuzi, kwa sababu sekta ya uvuvi wakati huo ilikuwa chini ya wizara hiyo, lakini kwa miaka miwili wizara haikupata mnunuzi,” alisema Dk Tamatamah.

Aliongeza kuwa, “Ilipofika mwaka 2007 Baraza la Mawaziri lilisitisha mchakato wa kuiuza TAFICO na kuamua ibaki kuwa shirika la serikali, na mwaka 2015 Baraza la Mawaziri liliagiza iliyokuwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kuifufua TAFICO kwa ubia na mchakato wa kuifufua ulianza mwaka 2015. Ilipofika Julai 2018 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliunda timu ya kuanza mchakato wa kuifufua TAFICO.”

Alisema moja ya majukumu iliyopewa timu hiyo ni kuzitambua mali zote za TAFICO nchi nzima. Mpaka sasa mali zilizorejeshwa zina thamani ya Sh bilioni 118.16 na kazi hiyo bado inaendelea, kwa kuwa mali zingine zilichukuliwa na halmashauri na watu binafsi.

Samaki waongezeka

Kwa mujibu wa Dk Tamatamah, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na vyombo vya ulinzi na usalama, waliendesha operesheni mbalimbali za kukabiliana na uvuvi haramu, hali iliyosaidia kuongezeka kwa samaki baharini na kwenye maziwa.

Alisema kabla ya mwaka 2017, idadi ya samaki aina ya sangara ilipungua sana katika Ziwa Victoria kutokana na uvuvi haramu. Alisema kisheria sangara wenye ukubwa wa sentimita 50 kushuka chini, wanahesabika kama vifaranga, hivyo kukutwa nao ni kosa kisheria. Aliongeza kuwa sangara wenye ukubwa wa sentimita 50-85 ni wakubwa na wanaruhusiwa kuvuliwa, lakini waliozidi sentimita 85 hao ni wazazi na hairuhusiwi kisheria kuwavua.

Dk Tamatamah alisema kwa tathmini iliyofanyika katika kipindi cha mwaka 2016/2017, ilibaini kuwa sangara wenye ukubwa wa sentimita 85 waliobakia walikuwa sawa na asilimia 0.4, sangara wadogo wenye ukubwa wa sentimita 50 kushuka chini waliobakia walikuwa sawa na asilimia 96.6. Lakini kwa mwaka 2018, sangara wenye ukubwa wa sentimita 85 kwenda juu, waliongezeka kutoka asilimia 0.4 hadi asilimia 5.2 na wadogo walipungua kutoka asilimia 96.6 hadi asilimia 62.8

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi