loader
Picha

Tanzania na miundombinu ya usafirishaji kukuza uchumi

SEKTA ya Usafi rishaji nchini ni miongoni mwa sekta zilizopewa kipaumbele cha pekee na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli tangu aingie madarakani mwaka 2015.

Kipaumbele hicho kinatokana na unyeti wa sekta hii katika usafirishaji wa bidhaa, huduma na watu kutoka eneo moja hadi lingine kama mkakati wa kujenga uchumi na kujiletea maendeleo.

Ili kuhakikisha sekta ya usafirishaji inakuwa na mchango mkubwa kwa uchumi na maendeleo ya wananchi na taifa kwa jumla, Serikali hii imeamua kwa dhati kuifufua Kampuni ya Ndege nchini (ATCL) iliyokuwa hoi kutokana na kukosa ndege za kutosha. Kutokana na hali mbaya iliyokuwa nayo ATCL, Serikali iliamua kuifufua kampuni hiyo kwa kununua ndege mpya 11 zenye ukubwa na uwezo tofauti.

Uamuzi huu wa serikali unatokana na maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 ambayo pamoja na mambo mengine, yanaitaka Serikali kuifufua Kampuni ya Ndege nchini (ATCL).

Kuimarishwa kwa usafiri wa anga kunachochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo sekta ya utalii. Mara kadhaa, Rais John Magufuli amekuwa akikisitiza umuhimu wa taifa kuwa na ndege zake yenyewe kwa kuwa zitaweza kuwaleta watalii nchini moja kwa moja kutoka katika nchi zao na hivyo kuliingizia taifa fedha za kigeni.

“Tuliahidi kuimarisha usafiri wa anga kwa kuifufua ATCL, tumenunua ndege mpya 11 zikiwemo Boeing 787-8 Dreamliner mbili, Airbus A220-300 nne na Bombardier Dash 8 Q400 tano, ndege nane zimeshawasili hapa nchini, Bombardier nyingine itakuja mwezi Juni mwakani na Airbus mbili zitakuja Juni na Julai 2021,” alieleza Rais Magufuli wakati akipokea ndege ya nane aina ya Bombardier Dash 8 Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 78 jijini Mwanza.

Ndege hizi kwa sasa zinafanya safari za ndani na nje ya nchi. Miongoni mwa safari za nje ni pamoja na safari za Entebbe nchini Uganda, Bujumbura nchini Burundi, Harare nchini Zimbabwe, Lusaka nchini Zambia, Mumbai nchini India, huku safari za Afrika Kusini zikitarajiwa kuanza wakati wowote baada ya kusitishwa kwa muda, lakini pia kuanza kwa safari hizo ni jitihada za ATCL kujitanua kibiashara baada ya kuendelea kufanya vyema katika soko la ndani.

Sekta ya usafiri wa anga pia inatiwa nguvu baada ya kuanza kutumika kwa Jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (NJIA) maarufu Terminal 3 lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka.

Kaimu Meneja wa Jengo hili kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Barton Komba anasema ubora na uwezo wa jengo hili la tatu la abiria umechangia kuongezeka kwa idadi ya ndege za kimataifa zinazohudumiwa kiwanjani hapo.

Komba anasema uendeshaji wa jengo hili umefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 80 ikiwemo muda mfupi zaidi unaotumika kumkagua abiria kabla hajaingia kwenye ndege lakini pia JNIA inahudumia ndege 21 zinazoruka kimataifa za mashirika mbalimbali na ndege 19 kati ya hizo zimehamishiwa katika jengo hili kutoka jengo namba mbili.

TCAA Sambamba na kuifufua ATCL, Serikali pia imefanikiwa kulinusuru Taifa kutofungiwa na Shirika la Usafiri wa Anga duniani (ICAO) baada ya kupata asilimia 37.8 ya alama katika ukaguzi uliofanywa na shirika hilo kabla ya mwaka 2015 ambalo linataka mashirika ya udhibiti na usimamizi wa usafiri wa anga kufikia asilimia 60 au zaidi; katika ukaguzi wa mwaka 2017 ambao ndiyo muda wa kikomo uliowekwa na ICAO, Tanzania ilipata asilimia 64.4.

Shirika hili la Usafiri wa Anga duniani ambamo Tanzania ni mwanachama pamoja na Mkataba wa Chicago wa mwaka 1944, inazitaka nchi wanachama kudhibiti na kusimamia Sekta ya Usafiri wa Anga katika nchi zao ili kuleta tija na usalama.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari, amesema kuwa tafiti zilizofanyika miaka ya 1970, zilionesha kuwa Tanzania inahitaji kuwa na rada nne ambazo Serikali ya Awamu Tano imezinunua kwa gharama ya Sh bilioni 67.3 na kuzifunga katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Songwe.

Johari anasema wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani mwaka 2015, kulikuwa na rada moja yenye uwezo wa kuona asilimia 25 tu ya anga lote la Tanzania. Baada ya kufungwa kwa rada hizi ambazo kwa Dar es Salaam na Kilimanjaro zimeshakamilika na zinafanya kazi, huku ya Mwanza ikiwa imefikia asilimia 92 na itazinduliwa Januari mwakani na baadaye kufuatia ya Songwe iliyofikia asilimia 60, zimelifanya anga lote la Tanzania kuonekana hali inayosaidia kuongeza mapato ya serikali kutokana na ndege za kimataifa zinazopita katika anga la Tanzania.

Kuimarishwa kwa Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Usafiri wa Anga, TCAA imeweza kuongeza mapato yake kutoka Sh bilioni 44.7 mwaka 2015 hadi kufikia Sh bilioni 48.4 mwaka 2016, Sh bilioni 63 mwaka 2017, Sh bilioni 66.3 mwaka 2018, Sh bilioni 73 mwaka 2019 na matarajio ya kuingiza Sh bilioni 80 mwaka 2020. USAFIRI WA RELI Katika kuhakikisha sekta ya usafirishaji inaimarishwa angani, ardhini na majini, Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kutekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa awamu ya kwanza na kutoka Morogoro hadi Dodoma kwa awamu ya pili kwa gharama ya Sh trilioni 7.

Mradi huu wa ujenzi wa SGR utaendelea hadi Mwanza na Kigoma mradi ambao utaimarisha siyo tu biashara za ndani, bali pia biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Rwanda.

Meneja wa Mradi huu kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Maizo Mgedzi, amewahi kusema wakati huo kuwa ubora wa reli ya kisasa inayojengwa Tanzania uko juu ikilinganishwa na ubora wa reli ambazo zimeshajengwa kwenye baadhi ya nchi barani Afrika ikiwemo Ethiopia, Afrika Kusini, Kenya na Morocco.

Kwa kuzingatia viwango vya ubora, Mgedzi anasema: “Reli hii itakuwa na uwezo wa kupitisha mzigo wa tani kati ya milioni 17 hadi 25 kwa mwaka ikilinganishwa na reli ya sasa ambayo uwezo wake wa kupitisha mizigo kwa mwaka ni tani milioni tano tu; kutokana na urefu wa njia za kupishanisha treni, reli hii inaweza kusafirisha kiwango kikubwa cha abiria na kwa kuanzia itakuwa inasafirisha abiria wasiopungua milioni 1.2 kwa mwaka.”

Serikali pia imekarabati njia ya treni ya Dar es Salaam- Kilimanjaro na Tanga na kurejesha usafiri huo. Hivi karibuni TRC ilitangaza viwango vya nauli ya treni kwenda Moshi kuwa Sh 39,100 kwa daraja la pili kulala, Sh 23,500 kwa daraja la pili kukaa na Sh 16,500 kwa daraja la tatu, wakati nauli ya kwenda Korogwe ni Sh 25,400 kwa daraja la pili kulala, Sh 15,300 kwa daraja la pili kukaa na Sh 10,000 kwa daraja la tatu. Safari za Tanga-Moshi zilizinduliwa Julai mwaka huu baada ya kufanyika kwa ukarabati wa kina wa njia ya treni baada ya kuachwa bila kutumika kwa miaka 12.

Tani 800 za saruji kutoka Tanga zilisafirishwa kwa treni ya mizigo kwenda Moshi huku shirika hilo likijipanga kutoa huduma za uhakika kwa mikoa ya kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

USAFIRI KWA MAJI

Kwa kuwa Tanzania inapakana na nchi nyingi zisizo na mlango wa bahari ikiwemo DRC, Burundi, Rwanda, Malawi na Zambia, Serikali imeona haja ya kuimarisha bandari zake kwa kujenga gati zenye uwezo wa kupokea meli kubwa za mizigo zinazofikia hadi urefu wa mita 300. Miongoni mwa bandari hizo ni Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Mtwara na Bandari ya Tanga zilizopo Bahari ya Hindi. Uwekezaji huu wa maboresho ya bandari umeelezwa utasaidia utoaji wa huduma bora za kibandari hapa nchini.

“Uwekezaji huu utaongeza ufanisi wa utendaji kazi na kondoa ucheleweshaji wa mizigo bandarini. Mradi huu, kutaifanya bandari yetu kuongeza soko lake kwa watu inaowahudumia ikiwemo nchi za Zambia, DRC, Malawi, Rwanda, Uganda na Burundi,”alieleza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Dk Raphael Chegeni walipotembelea Bandari ya Dar es Salaam mwezi Machi mwaka huu.

Maboresho haya ya bandari pia yaliifanya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kukutana na wachimbaji wakubwa wa madini na wamiliki wa meli kubwa za mizigo duniani mwezi Julai mwaka huu kwa lengo la kuongeza kiwango cha biashara kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alitaja kampuni hizo kubwa kuwa ni Bridge Shipping, Acess World, Impala Terminals, Trafigula and Reload Logistics pamoja na wadau wengine wa bandari.

Kamwelwe anasema aliwaita wadau hao wa bandari ili kuzungumza nao ili waeleze changamoto wanazokumbana nazo katika bandari hapa nchini ili ziweze kutatuliwa kwa kuwa Serikali inataka mizigo yao ipitie Bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 100.

BARABARA

Sekta ya usafirishaji kwa njia ya barabara nayo haijaachwa nyuma. Tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, kumeshuhudiwa miradi mikubwa ya barabara ikijengwa maeneo mbalimbali nchini.

Ujenzi wa barabara hizi ni muhimu katika kuunganisha mkoa na mkoa na wilaya na wilaya ili kurahisisha shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara, usafirishaji wa bidhaa na watu. Miradi hiii ya barabara inafanyika katika mikoa mbalimbali ukiwemo Tabora, Dar es Salaam, Dodoma, Singida, Morogoro na mingine mingi.

Mbali na barabara hizi, pia Serikali imefanikisha ujenzi wa Daraja la Juu la Mfugale eneo la Tazara na Daraja la Juu eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam linaloendelea kujengwa.

NTAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) mkoa ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi