loader
Picha

Kingwangalla, Katibu Mkuu wake kitanzini siku 5

RAIS John Magufuli ametoa siku tano kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda kuondoa tofauti zao, vinginevyo atatengua uteuzi wao.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana, alipozungumza na maofisa na askari Wanyamapori wa Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, ambako ametembelea na kujionea vivutio vya utalii.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, katika salamu zake, Rais Magufuli amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kazi nzuri ya uhifadhi, kukuza utalii na kuchangia mapato ya serikali. Lakini, alieleza kusikitishwa kwake na mahusiano mabaya yaliyopo kati ya Dk Kigwangalla na Katibu Mkuu wake, Profesa Mkenda, hali ambayo inasababisha baadhi ya shughuli za wizara kusuasua.

“Ninafahamu watendaji wenu wa juu, Katibu Mkuu na Waziri kila siku wanagombana, na ninawatazama taratibu, nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite awaeleze lakini wasipobadilika nitawaondoa, hilo ni lazima nilizungumze kwa dhati, siwezi kuwa na watendaji wa kuteua mimi halafu kila siku wanagombana, kuna mambo mengi hayaendi, Katibu Mkuu hamheshimu Waziri na Waziri naye hataki kwenda na Katibu Mkuu, siwezi kuvumilia hilo.

“Kwa hiyo nalizungumza hili siku ya leo tarehe 31 ya mwezi wa 12 (2019) kwamba wajirekebishe na ikiwezekana wajirekebishe ndani ya siku tano, wawe wanasalimiana, wanazungumza, mimi ninafahamu nina vyombo, ninajua nani hafai zaidi,” alisisitiza Rais Magufuli.

Aidha, aliiongezea muda Bodi ya Tanapa iliyomaliza muda wake chini ya Mwenyekiti, Jenerali mstaafu George Waitara kutokana na kuridhishwa na kazi nzuri zilizofanywa na Tanapa chini ya uongozi wa bodi hiyo, ikiwamo kuunda Jeshi Usu la Askari Wanyamapori na Hifadhi ya Misitu.

Alitaka iendelee kupiga hatua kwa maslahi ya Taifa. Rais Magufuli alisema Tanzania yenye hifadhi za taifa 22, imetoa zaidi ya asilimia 32.5 ya eneo la ardhi yake kwa ajili ya hifadhi, na imefanya hivyo kwa maslahi ya Watanzania na watu wote duniani wanaotembelea hifadhi hizo.

Alimpongeza Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa, Dk Allan Kijazi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Fredrick Mofulu kwa kazi nzuri ya kudhibiti ujangili katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo, kutunza mazalia ya samaki na ndege, ambao husafiri kutoka nchi mbalimbali duniani na kutunza uoto na wanyama mbalimbali waliomo katika hifadhi hiyo.

Aliahidi serikali itatoa Sh bilioni mbili, kununua kivuko chenye uwezo wa kuchukua watu 100 na magari manne ili kurahisisha usafirishaji wa watalii, wanaoingia na kutoka Hifadhi ya Taifa ya Rubondo wakiwa na magari yao.

Alisema kwa sasa Tanzania, ina bustani za wanyamapori (zoo) 23, mashamba ya wanyama 20 na ranchi sita. Alitoa wito kwa Watanzania wakiwamo wastaafu katika tasnia ya wanyamapori, kujitokeza kuanzisha bustani za wanyamapori, mashamba ya wanyama na ranchi ambazo zitasaidia kuvutia watalii na kuongeza kipato.

Mapema akimkaribisha Rais Magufuli, Kamishna Kijazi alimshukuru kwa juhudi zake za kutilia mkazo shughuli za uhifadhi na kupanua maeneo ya uhifadhi kutoka hifadhi 16 mwaka 2015/2016 hadi kufikia hifadhi 22 hivi sasa.

Aliahidi kuwa Tanapa itahakikisha hifadhi hizo zinatunzwa kwa manufaa ya Taifa. Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Mofulu alisema hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 456.6, inao wanyama mbalimbali wakiwamo sokwe, pongwe, swala, tembo na twiga na pia ni mazalia ya samaki wa Ziwa Victoria na ndege mbalimbali.

Alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2014/15 hadi 2018/19, idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imeongezeka hadi kufikia 5,700 kwa mwaka, walioingiza Sh bilioni 1.4 katika Pato la Taifa. Rais Magufuli amekuwa Rais wa kwanza kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo akiwa madarakani.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi