loader
Picha

JPM aapa kufa na majizi 2020

RAIS Dk John Magufuli amesema mpaka sasa bado wapo wezi wanaokula nchi ; na anamuomba Mungu aendelee kumpa uhai mwaka huu, aendelee kuwatumbua wote.

Alisema hayo juzi wakati akiagana na maofisa na Askari Wanyamapori wa Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, ambako alitembelea na kujionea vivutio vya utalii.

Pia alikuwa akiwasalimia wananchi wa Nyabugera na Muganza wakati akiwa njiani kurejea nyumbani kwake Chato mkoani Geita. “Nchi hii ilikuwa inaliwa sana na majizi na mpaka sasa bado wapo, namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kunipa uhai ili katika mwaka 2020 niendelee kuwatumbua majizi wote na fedha tutakazopata tuzipeleke kwenye miradi ya maendeleo kama ambavyo tumenunua ndege 11, tunajenga reli (standard gauge), tunatoa elimu bure na mengine mengi,” alisema.

Vilevile, Rais Magufuli alimuonya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Eliud Mwaiteleke kwa matumizi mabaya ya fedha, yanayofanywa na halmashauri hiyo na alitaka dosari hizo zirekebishwe mara moja.

“Nataka ujirekebishe, wananchi hawa wanateseka sana,” alisema. Kabla na baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli aliweka bayana dhamira yake ya kuhakikisha anapambana na wezi na mafisadi. Katika hotuba yake bungeni, Rais Dk Magufuli aliwaeleza wabunge kwa wazi kwamba ahadi yake ya kupambana na rushwa na ufisadi, haikuwa kwa sababu ya kurubuni wananchi wampe kura zao bali aliongea kwa dhati.

“…Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua majipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu, lakini bahati mbaya halina dawa nyingine. Hivyo naomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, mniombee na mniunge mkono wakati natumbua majipu,” Rais Magufuli aliwaambia wabunge.

Mwezi Februari 2016 akihutubia Watanzania kupitia mkutano ulioandaliwa na Wazee wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema ameipokea nchi ikiwa katika hali mbaya kutokana na watu wachache, kujilimbikizia mali za kutosha, huku wananchi wa chini wakizidi kuumia kwa umasikini. Wazee hao waliandaa mkutano huo, kumpongeza Rais Magufuli kwa aliyoyafanya akiwa madarakani kwa siku 100.

Alisema nchi ina majipu kila mahali. “Kuna watu hawana shida ya pesa kabisa, ni watu wachache na fedha hizo walizipata visivyo halali na Watanzania wengi wamebakia masikini wa kutupwa,” alisema.

Aliongeza: ‘’Nawasihi Watanzania wenzangu mkiniona natumbua majipu au mawaziri wangu wanafanya hivyo, waungeni mkono, nchi hii kila kona ni majipu, ni lazima tuyatumbue ili pesa zipatikanne zikahudumie wananchi wa hali ya chini.’’

Wazee wa Mkoa wa Dar es salaam kupitia kwa Mwenyekiti wao, Hemed Mkali walimhakikishia kwamba wazee wote wanamuunga mkono kwa dhati, kwa kasi yake ya utendaji serikalini. Tangu alipoingia madarakani Novemba 5, 2015, Rais Dk Magufuli ameendelea kuwajibisha viongozi na watendaji mbalimbali, kwa kuwatumbua kutokana na sababu mbalimbali, wakiwamo walioshindwa kuwajibika, waliotuhumiwa kujihusisha na wizi wa fedha pamoja na matumizi mabaya ya ofisi.

WALIOTUMBULIWA

Miongoni mwa nyadhifa (za uteuzi wa Rais) ambazo zimeguswa na zinaendelea kuguswa, kwa maana ya kuvuliwa madaraka wahusika kutokana na ama utendaji usiokidhi kasi yake au tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi ni wakuu wa mikoa, makatibu tawala, mawaziri, mabalozi wa nje, wakurugenzi wa halmashauri na makatibu wakuu. Vile vile taasisi mbalimbali za serikali watendaji wake wakuu/ bodi, walitumbuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

NIDA Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma za kuwepo ubadhirifu wa fedha katika mamlaka hiyo.

Alichukua uamuzi huo miaka minne iliyopita, baada ya kupata tuhuma za matumizi ya Sh bilioni 179.6, huku kukiwa na malalamiko ya utendaji usioridhisha wa mamlaka hiyo katika utoaji wa Vitambulisho vya Taifa. Mbali na Maimu, wengine waliotumbuliwa ni Mkurugenzi wa TEHAMA Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.

TCRA

Rais Magufuli alivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Ally Simba kwa tuhuma za kutosimamia ipasavyo mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS) na kusababisha nchi kupoteza mapato ya takriban Sh bilioni 400 kwa mwaka.

Mwezi Machi 2013 TCRA iliingia mkataba na Kampuni ya SGS kuhusu uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu. Kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano, lakini inadaiwa kuwa hadi hatua hizo zinachukuliwa, ilikuwa haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusu udhibiti wa mapato ya simu za ndani.

NSSF Vigogo sita ambao ni wakurugenzi katika Shirika la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF), makao makuu jijini Dar es Salaam, wakiwamo mameneja watano, walisimamishwa kazi.

Wakurugenzi hao walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira. Vile vile Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dk. Ramadhan Dau na kumteua kuwa Balozi.

MUHIMBILI

Novemba 9, 2015 Rais Magufuli alifanya ziara ya kushitukiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukuta mashine za MRI na CT-Scan, hazifanyi kazi, hivyo alivunja Bodi ya Wadhamini ya hospitali hiyo iliyokuwa na wajumbe 11. Aidha, alimsimamisha kazi Dk. Hussein Kidanto, aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Hospitali hiyo na kumrudisha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jami.

BANDARINI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza Bandari ya Dar es Salaam Novemba 27, 2015 na kubaini kontena 329 zilitolewa bandarini bila kulipiwa kodi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 80. Maofisa 12 walienguliwa na alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka.

TAKUKURU

Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, kwa kile kilichoelezwa kuwa alijiridhisha alishindwa kushughulikia rushwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

TANESCO

Desemba 6, 2015 Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), lilisimamisha maofisa saba, kwa kile kilichodaiwa kwamba ni kutokana na makosa mbalimbali ikiwamo wizi na ubadhirifu.

EWURA

Juni 11, 2017 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi.

RAHCO

Mwaka 2015 Rais alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito kupisha uchunguzi wa kina wa tuhuma za ukiukwaji wa taratibu za manunuzi katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati. Alivunja pia bodi ya kampuni hiyo sambamba na ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

OCEAN ROAD

Mwaka 2015 Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alimsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk.Diwani Msemo kupisha uchunguzi wa tuhuma za mgongano wa kimaslahi ulioathiri utendaji wa taasisi. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na ziara alizofanya Rais Magufuli.

WAHUJUMU UCHUMI

Katika mkakati wake wa kubana na kuwajibisha wezi wanaokula nchi, wapo watuhumiwa lukuki wakiwamo wafanyabiashara wakubwa, wanaoshikiliwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Baada ya mwaka jana Rais Magufuli kushauri mahabusi wa makosa mbalimbali hasa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, walio tayari kuomba msamaha na kurudisha fedha walizotakatisha, taarifa inaonesha watu 467 wamekiri makosa hayo na kukubali kurejesha zaidi ya Sh bilioni 107 walizolisababishia hasara Taifa.

Rais alitoa ushauri huo kwa Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) na fedha hizo zinazorudi, zinaelekezwa katika miradi ya kijamii.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi