loader
Watatoka kweli leo?

Watatoka kweli leo?

LEO mashabiki wa soka hasa wa Simba na Yanga wanatarajiwa kusitisha shughuli zao kwa dakika 90 ili kufuatilia mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya mahasimu hao utakaochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.

Wakati mashabiki wakisubiri wakati huo uwadie, kumekuwepo na tambo za hapa na pale kila upande ukijinadi kuibuka na ushindi huku makocha na manahodha wa timu zote nao jana walitambiana mbele ya waandishi wa habari, kila mmoja akisema atashinda.

Alianza kocha wa Yanga, Charles Mkwasa , alisema licha ya kuwa nyuma kwa pointi 10 dhidi ya Simba leo wataibuka na ushindi ambao utawavuruga wapinzani wao katika mbio za ubingwa na kupunguza tofauti ya pointi.

Alisema uhakika wa kuchukua pointi tatu kwa Simba unatokana na maendeleo ya kiwango kilichooneshwa na kikosi chake toka alipoichukua kutoka kwa kocha Mwinyi Zahera aliyetupiwa virago kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo, ambapo ameshinda mechi tano na sare mbili.

“Licha ya kuonekana Yanga tuko nyumba hatuwezi kukubali kufungwa na Simba ila tuna uhakika wa kuchukua pointi tatu kutoka kwao zitakazotufanya kupunguza tofauti ya pointi zilizopo na kuvuruga mbio zao za ubingwa msimu huu,” alisema Mkwasa.

Alisema anatamani mchezo huo uchezwe hata leo (jana), lakini kwa vile utaratibu wa Bodi ya Ligi umepanga mchezo uchezwe kesho (leo), hivyo watawasubiri kuendeleza kauli mbiu ya kila mchezo kushinda kama walivyowatibulia Tanzania Prisons na ana historia ya kutokufungwa na Simba.

Yanga ndio timu pekee hadi sasa iliyoifunga Tanzania Prisons na kuitibulia rekodi yake ya kutofungwa tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga walishinda bao 1-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora Iringa. Mchezo huo ulihamishiwa Samora baada ya ule wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya sehemu yake ya kuchezewa kuharibiwa vibaya na tamasha la muziki la Wasafi lililofanyikia uwanjani hapo.

Mkwasa aliongeza kusema maandalizi ya mchezo ni mazuri ila wachezaji Tariq Kiakala aliyeumia kwenye mchezo uliopita na beki Lamine Moro, ambaye ana kadi tatu za njano watakosa ‘dabi’ hiyo ya Kariakoo na nafasi zao zitazibwa na nyota wengine.

Naye Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema wanajua mchezo huo utakuwa mgumu na malengo yao ni kutafuta pointi tatu muhimu zitakazo wafanya kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi.

“Najua utakuwa mchezo mgumu kwetu kutokana na michezo mingi ya watani inakuwa na mambo mengi, ikiwemo mihemko ila malengo yetu ni kutafuta pointi tatu zitakazo tufanya kuendelea kuwa mbele,” alisema Sven.

Pia alisema michezo ya ‘dabi’ mara nyingi inakuwa na mihemumko ndani na nje ya uwanja ila kupitia michezo minne waliyocheza anajua atakuwa na kikosi imara cha kuikabili Yanga isipokuwa wachezaji Juma Rashid na Miraji Athuman, ambao wanasumbuliwa na majeraha watakosa mchezo huo.

Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo na vinara kwa sasa wana pointi 34 baada ya kucheza mara 13 ndio wenyeji wa mchezo huo, wataikaribisha Yanga wanaoshika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 24 wakicheza michezo 11.

Pamoja na kutofautiana kwa pointi 10 msimu huu wanakutana kila mmoja akiwa amepoteza mchezo mmoja, ambapo Simba walifungwa na Mwadui na Yanga ilifungwa na Ruvu Shooting.

Hata hivyo, pamoja na Simba kupewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na ubora wa kikosi na kiwango cha kushinda michezo yake mingi hususani uliopita dhidi ya Ndanda kwa mabao 2-0, lakini mchezo wa watani hauko hivyo kwani lolote linaweza kutokea. Yanga wenyewe pamoja na kuonekana kupata matokeo kwa kushida, ikiweno mechi iliyopita dhidi ya Biashara United kwa bao 1-0, lakini bado nao wana nafasi ya kufanya maajabu na kuifunga Simba au kulazimisha sare.

Aidha, Simba inaonekana kuwa na washambuliaji wenye uchu wa kufunga kwani msimu uliopita mfungaji bora wa ligi alitoka kwao akiwa na mabao 22 ambaye ni Meddie Kagere na msimu huu bado ndiye anaongoza akiwa na mabao tisa na msimu uliopita Simba iliifunga Yanga kwa bao 1-0 katika mchezo wa marudio wakati mchezo wa awali walitoka suluhu.

MANAHODHA WANENA

Kwa upande wa Simba na Yanga manahodha wao, John Bocco wa Simba na Juma Abdul wa Yanga kila mmoja ametamba kuibuka na ushindi ili kuwafurahisha mashabiki wao na kuwapa zawadi ya Mwaka Mpya 2020. Bocco alisema hawataingia kwenye mchezo kwa kuangalia historia ya nyuma walifanya nini bali wanazingatia maandalizi waliyofanya na kutafuta matokeo ingawa utakuwa mchezo mgumu kwao kama michezo mingine.

“Tuna wachezaji bora kama wapinzani wetu na makocha wazuri, utakuwa mchezo mgumu lakini tutapambana kwa nguvu kutafuta ushindi, hatuwezi kuingia kwa kuangalia historia ya nyuma tunajikita kwenye maandalizi ya mechi ya kesho (leo) kutafuta pointi tatu,” alisema Bocco Naye Juma Abdul alisema wachezaji wote wana morali na wamejipanga kupata pointi tatu na kuwaomba mashabiki wa Simba wasije uwanjani na matokeo mfukoni kwani mchezo wa mpira una matokeo ya ajabu.

“Kikosi chetu kina morali ya kutosha kulingana na maandalizi tuliyofanya na wachezaji wapya waliosajiliwa wana muunganiko wa kutosha hivyo mashabiki wetu waje kwa wingi kupokea ushindi wa mwaka mpya ,“ alisema Abdul Nalo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeomba mashabiki wa timu zote kuja uwanjani kutazama mechi na kuachana vurugu, ambazo zinaweza kusababisha kukamatwa na vyombo vya usalama kwani ulinzi utakuwepo wa nguvu.

Viingilio katika mechi ya leo vitakuwa, kwenye mzunguko Sh 7,000, VIP C na B ni Sh 20,000 na VIP A ni Sh 30,000.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/262aafd27c5b32f7bfef0b838a3cf279.jpg

TAMASHA la muziki wa dansi ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi