loader
Simba uso kwa uso na Azam Mapinduzi Cup

Simba uso kwa uso na Azam Mapinduzi Cup

SIMBA itacheza nusu fainali dhidi ya Azam FC katika mchezo wa mashindano ya Mapinduzi yanayochezwa visiwani Zanzibar kesho kutwa.

Mchezo huo utachezwa katika Uwanja wa Amaan, Unguja baada ya jana kuifunga Zimamoto kwa mabao 3-1 katika Uwanja wa Gombani, Pemba. Azam FC ambaye ni bingwa mtetezi wa mashindano hayo, anakutana na Simba ambayo katika fainali zilizopita waliifunga kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Gombani Pemba, hivyo mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Simba ambayo ipo Kundi B iliifunga Zimamoto jana kwa mabao 3-1 inakutana na Azam FC ambayo ipo Kundi A ambayo iliitoa Mlandege kwa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa juzi Uwanja wa Amaan kwa bao la Obrey Chirwa dakika ya 57.

Simba ilianza kupata bao la kwanza dakika ya nne likifungwa na John Bocco na dakika tano baadaye iliongeza bao la pili lililofungwa Sharaf Shiboub katika dakika ya tisa akiunganisha kona iliyopigwa na Ibrahim Ajibu, lakini dakika ya 28 Zimamoto walipata bao la kwanza lililofungwa na Ibrahim Ahmada na timu hizo kwenda mapumziko zikiwa 2-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na katika dakika ya 53 Ibrahim Ajib aliifungia Simba bao la tatu baada ya kuwazidi mbio walinzi wa Zimamoto, bao lililodumu hadi dakika 90 kipyenga cha mwisho kilipopulizwa.

Kwa mara ya kwanza Simba ilimchezesha Louis Mequissone raia wa Msumbiji iliyemsajili juzi katika dirisha dogo ambaye aliingia dakika ya 78 kuchukua nafasi ya Hassan Dilunga.

Baada ya mchezo huo, nahodha wa Simba, John Bocco, alisema wanakwenda kuangalia makosa yao na kuyafanyika kazi na mchezo wao dhidi ya Azam FC utakuwa wa ushindani na wao watahitaji kushinda mchezo huo ili kuwapa raha mashabiki.

“Azam FC ina wachezaji wazuri kama ilivyo Simba hivyo mchezo huo tumeuchukulia kwa uzito mkubwa na tunakwenda kujiandaa ili tuweze kushinda,” alisema Bocco.

Mtibwa Sugar ambayo ipo Kundi B inatarajiwa kucheza nusu fainali kesho na mshindi wa mchezo wa Yanga dhidi ya Jamhuri ambao ulichezwa jana usiku. Mtibwa Sugar iliifunga Chipukizi kwa penalti 4-2 baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1 mchezo uliochezwa Uwanja wa Gombani, Pemba, ambapo kipa Said Mohammed ‘Ndunda’ aliokoa penalti mbili.

Chipukizi ilitangulia kufunga bao dakika ya tano lililofungwa na Suleiman Nassor na Haroun Chanongo kuisawazishia Mtibwa Sugar dakika ya 63. Shujaa wa Mtibwa alikuwa Nduda ambaye aliokoa penalti za Jumaa Kassim na Abdallah Mohamed, huku penalti za Mtibwa Sugar zikifungwa na Omar Sultan, Abdulhalim Humud, Riffat Khamis na Dickson Job na zile za Chipukizi zilifungwa na Salim Abui na Abdallah Khalisan.

Mashindano hayo ya 13 yanashirikisha timu nne za Zanzibar na timu nne za Tanzania Bara na mecho zitachezwa kwa mtindo wa mtoano, ambapo bingwa anatarajiwa kuondoka na Sh milioni 15 pamoja na kombe. Fainali za mashindano hayo zitafanyika Januari 13 katika Uwanja wa Amaan majira ya saa 2:15 usiku.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/34acbdd154c806ae94d0343afa1a0a38.png

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi