loader
Simba, Azam hapatoshi leo

Simba, Azam hapatoshi leo

SIMBA leo inashuka dimbani kucheza nusu fainali dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Mashindano ya Kombe la Mapinduzi utakaochezwa Uwanja wa Amaan Unguja, Zanzibar kuanzia saa 2:15 usiku.

Azam FC ambayo ni bingwa mtetezi inacheza na Simba ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga katika fainali zilizopita kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Gombani Pemba, hivyo mchezo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa. Akizungumza kocha msaidizi wa Simba, Suleman Matola alisema mfumo wa mtoano umezidi kuifanya mechi kuwa ngumu, lakini wamejipanga kuondoka na ushindi dhidi ya Azam .

Nahodha wa Simba, John Bocco alisema mchezo huo utakuwa wa ushindani kwa sababu Azam FC watakuwa wanatafuta ushindi ili wafuzu fainali kutetea Kombe lakini na wao wanahitaji kufuzu fainali na ili warudi na taji hilo Dar es Salaam kuwapa raha mashabiki wao.

“Azam FC ina wachezaji wazuri kama ilivyo Simba hivyo mchezo huu tumeuchukulia kwa uzito mkubwa na tutaingia uwanjani kwa lengo la kutafuta ushindi ili tufuzu fainali na kombe lije Dar es Salaam,” alisema Bocco.

Naye kocha wa makipa wa Azam FC, Iddi Abubakar alisema wamekuja katika mashindano kushindana sio kushiriki, hivyo wataonesha ushindani kudhihirisha kuwa ndio mabingwa watetezi .

Naye nohodha wa Azam FC, Aggrey Morris alisema wamejiandaa kuikabili Simba na wanaamini watashinda mchezo huo na kutinga fainali.

“Tunajua tunakwenda kucheza na timu bora ila hata sisi ni bora ndio maana tumefika kwenye hatua hii, hivyo tumejipanga kushinda ili tufuzu fainali,” alisema Moris.

Simba iliifunga Zimamoto kwa mabao 3-1 na Azam FC iliifunga Mlandege kwa bao 1-0 hivyo mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani ukizingatia kwenye msimamo wa Ligi Kuu, Simba inaongoza ikiwa na pointi 35 na Azam FC inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 26.

Kwa msimu huu kwenye ligi hiyo, Simba iliifunga Azam FC kwa bao 1-0 na baada ya kipigo hicho ikaamua kuachana na kocha Etienne Ndayiragije na kumchukua Aristica Cioaba ambaye yupo na kikosi hicho hadi sasa.

Mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa wa Mapinduzi ni mwaka 2011 baada ya kuifunga Yanga kwa mabao 2-0 na mwaka jana ilishika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Azam FC kwa mabao 2-1.

Mashindano haya ya 13 yalishirikisha timu nne za Zanzibar ambapo zote zimeaga mashindano na timu nne za Tanzania Bara na yanachezwa kwa mtindo wa mtoano ambapo bingwa anatarajiwa kuondoka Sh Milioni 15 pamoja na Kombe. Timu ambazo zimeaga mashindano kutoka Kundi A ni Mlandege na Jamhuri na Kundi B timu za Zimamoto na Chipukizi.

Mashindano hayo maalum kwa ajili ya kusherehekea miaka 56 ya Mapinduzi yalianza mwaka 2007 na hufanyika kila mwaka ambapo Azam ndio bingwa mtetezi, ambapo aliifunga Simba mabao 2-1 mwaka jana katika Uwanja wa Gombani Pemba. Fainali za mashindano hayo zitafanyika Januari 13 katika Uwanja wa Amaan majira ya saa 2:15 usiku.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8383be9aeaede507e78395d9df4c2e04.jpg

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi