loader
Dstv Habarileo  Mobile
Dawa ya viluwiluwi yapata soko

Dawa ya viluwiluwi yapata soko

HATIMAYE dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu inayozalishwa nchini, imepata suluhisho la soko la ndani baada ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kupewa rasmi jukumu la kuiuza, baada ya kutokuwapo mpango madhubuti wa kuiingiza kwenye masoko nchini.

Uamuzi huo umekuja ikiwa imepita takribani miaka miwili, tangu kiwanda cha Tanzaninia Biotech Production Limited (TBPL) kilichopo Kibaha mkoani Pwani, kilipoanza uzalishaji bila mpango madhubuti wa kuzifikisha kwa watumiaji.

Kiwanda hicho ambacho thamani ya uwekezaji wake ni takribani Sh bilioni 50.6, kilijengwa kwa ushirikiano kati ya NDC na Kampuni ya LABIOFAM ya Cuba na kilianza uzalishaji mwaka 2017 kwa msaada wa teknolojia kutoka Cuba.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Profesa Damian Gabagambi aliliambia gazeti hili juzi kwamba kulingana na mkataba, kampuni ya Cuba ilitakiwa kuendesha kiwanda sambamba na kutafuta masoko ya bidhaa, jambo ambalo halikutekelezwa ipasavyo, hivyo kusababisha uzalishaji kuwa chini. Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha lita milioni sita za dawa, lakini sasa kinazalisha lita 570,000 kutokana na kutokuwapo soko la uhakika.

Alikiri kuwa ukosefu wa masoko, ulisababisha sehemu ya dawa kuharibika ikizingatiwa kwamba ukomo wa matumizi ni miaka miwili.

“Wacuba walikabidhiwa kiwanda wakiendeshe, watafute masoko lakini baada ya kusubiri miaka mingi fedha ikawa haiingii. Tukawaambie tupeni NDC kazi ya kuuza. Suala la masoko tumelichukua sisi…tulikabidhiwa mwezi uliopita (Desemba mwaka jana),” alisema Profesa Gabagambi.

“Tumepewa hili jukumu mwezi uliopita…zipo njia nyingi tutafanya. Sasa tunaandaa mpango wa masoko,” alisema na kubainisha kwamba wameandaa mkutano wa wadau utakaofanyika Januari 20 mwaka huu, kujadiliana namna ya kuwauzia na matumizi ya dawa hizo kwenye mazingira yao.

Wadau hao ni kampuni kubwa za migodi, mashamba makubwa na viwanda mbalimbali. Gabagambi alisema mkataba wa kuuziana dawa, utawezesha kiwanda kuongeza uzalishaji, mapato na pia kupanua wigo wa matumizi ya dawa hizo. Akizungumzia soko la nje, Profesa Gabagambi alisema mkataba kati ya serikali na kampuni ya Cuba, hauruhusu NDC kuuza moja kwa moja nje ya nchi.

“Mkataba haujakaa vizuri. Sisi haturuhusiwi kuuza nje. Tukitaka lazima tumuuzie M-Cuba ndipo auze nje. Imetuweka katika mazingira magumu,” alisema. Alisema mkataba unaweza kupitiwa upya, lakini unapaswa kushughulikiwa kidiplomasia.

“Soko la ndani kimkataba liko huru, la nje lazima mkataba ubadilishwe,” alisema na kuongeza kwamba mikakati iliyopo, inaleta matumaini makubwa ya bidhaa hiyo kupata soko. tofauti na awali.

Alifafanua kwamba kutakuwa na wakala kila mkoa, ambaye kazi yake itakuwa ni kuuza kwa watu wote, baada ya kupatiwa mafunzo na kujengewa uwezo wa kuuza dawa hizo. Vile vile, halmashauri zimetenga asilimia tatu ya bajeti yake kwa ajili ya kununua dawa hizo, jambo ambalo linaipa NDC matumaini ya kuingiza mapato. Agosti mwaka jana wakati wa ziara ya washiriki wa maonesho ya viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kiwandani TBPL, ilielezwa kuwa dawa hizo hazifahamiki wala kutumika ipasavyo. I

lielezwa kwamba upo umuhimu wa kuitambulisha na kuhakikisha inapatikana kwa urahisi mitaani isaidie kutokomeza mbu waenezao malaria na dengue. TBPL ni kiwanda pekee Afrika kilichozinduliwa Julai, 2015 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa ajili ya kutafuta suluhisho la kudumu la kupambana na malaria kwa kuua viluwiluwi, badala ya kusubiri kuangamiza mbu (waliokomaa).

Kilianza uzalishaji mwaka 2017 kwa thamani ya uwekezaji wa takribani Sh bilioni 50.6 kwa msaada wa teknolojia kutoka Cuba. Taasisi ya Utati na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPRI) imethibitisha dawa hiyo inaua viluwiluwi wa mbu aina ya aedes, waenezao homa ya dengue, anofelesi waenezao malaria na culex waenezao matende.

Dawa zinauzwa kuanzia ujazo mdogo wa matumizi ya nyumbani; Mililita 30 ambazo huuzwa kwa Sh 1,000 bei ambayo kila mwananchi anaweza kumudu. Nyingine ni kwenye ujazo wa lita 20 hadi lita 1,500 kwa ajili ya matumizi makubwa.

Lita ya dawa inapaswa kuchanganywa katika kila eneo lenye kilometa za mraba 200 za maji yaliyotuama, machafu, mabwawa ya samaki, mashimo ya vyoo, madimbwi, mito, mifereji na mashamba ya mpunga. Mtumiaji anaweza kuweka matone 20 katika kila lita 50 za maji katika matangi, makaro au vyombo vya kuhifadhia maji nyumbani .

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c0be60bce53800aab855a4feb1f047eb.png

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameweka jiwe la ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi