loader
Picha

Neema yazidi kumshukia kijana aliyefanya maajabu kidato cha 4

TAASISI mbalimbali na watu binafsi, wameonesha nia ya kumsaidia mwanafunzi, Yonana Lugedenga pamoja na familia yake, kumwezesha aendelee na masomo yake, baada ya kufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, licha ya mazingira magumu aliyosomea.

Aidha, upande wa serikali, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema mwanafunzi huyo ambaye ni tunda la mafanikio ya sera ya elimu bure, atapewa Sh milioni moja na kununuliwa vifaa vinavyohitajika, kujiunga na kidato cha tano, kama ilivyo kwenye mpango uliofikiwa na mkoa. Hata hivyo, Mtaka alisema jana kutokana na maoni na hoja mbalimbali, zilizotolewa kuhusu mwanafunzi huyo, katika tathimini watakayoifanya, wataangalia uwezekano wa kuweka pia mpango wa kufuatilia na kuwezesha wanafunzi wanaofaulu hadi chuo kikuu.

Yohana ambaye amehitimu Shule ya Sekondari ya Igaganulwa Kata ya Dutwa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, amefaulu mtihani wa kidato cha nne kwa kupata alama A masomo yote tisa. Mtaka alisema miongoni mwa taasisi ambazo zimewasiliana naye, zikitaka kumsaidia mtoto huyo ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lililosema linataka kumsaidia.

“Unesco wamenipigia simu, nadhani wanataka kum-support. Wana nia hata ya kusaidia wadogo zake…” alisema na kuongeza kuwa pia mkurugenzi mtendaji wa benki ya NMB na watu binafsi, waliowasiliana naye, walionesha kuwa wana jambo wanataka kulifanya.

Akizungumzia matokeo na mjadala ulioibuka, kuhusu ufaulu wa Yohana aliyekuwa akisoma shule ya kata ya Igaganulwa, Mtaka alisema ni uthibitisho wa umma, kuanza kuamini shule za serikali.

Alisema jambo ambalo umma haujafahamishwa ni kwamba mwanafunzi huyo, anamulika mafanikio ya sera ya elimu bure, iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Magufuli.

“Hii ndiyo Form Four (kidato cha nne) ya kwanza tangu Rais Magufuli aingie madarakani. Kama isingekuwa elimu bure huyu mtoto angewezaje kusoma? Maeneo kama haya (vijijini) maisha yalikuwa magumu. Hata huyu mtoto asingeweza kusoma,” alisema Mtaka.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga pia katika ukurasa wake wa Facebook, baada ya kumtembelea Yohana ambaye taarifa zinasema baba yake mzazi hayupo nyumbani tangu akiwa darasa la tano, alimshukuru Rais Magufuli kwa mpango wa elimu bure.

Katika ukurasa huo wa Facebook, mkuu wa wilaya anaonekana katika picha tofauti akiwa na mama wa kijana huyo, Masalu Lulyalya pamoja na bibi yake, Mbuke Limbu na alisema, “Je isingekuwa elimu bure, ingekuwaje kwa watoto hawa kutoka familia masikini? Asante Dk Magufuli kwa maono ya hali ya juu kwa Watanzania hawa.”

“Inatia hamasa sana na kumshukuru sana Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kwa kuleta elimu bure. Maana taarifa ni kwamba kijana huyu hata uniform (sare) za shule kwa miaka yote alikuwa ananunuliwa na walimu wake kwa vile alijulikana kwa kuwa na akili nyingi sana”.

Kulingana na mkakati wa mkoa, kuhusu watoto wa shule za serikali wanaofaulu kwa kupata alama 7 kwa maana ya A katika masomo yote kidato cha nne, hupewa Sh milioni moja za kukidhi mahitaji yake. Vivyo hivyo, kwa kidato cha sita kwa mwenye ufaulu wa alama 3.

Kama angetajwa kuwa katika 10 bora kwa shule za serikali, angepata Sh milioni tatu ambazo huwekwa kwenye akaunti yake ya benki.

“Shilingi milioni moja tunazotoa zinatimiza mahitaji. Kuhusu kufuatilia mwanafunzi hadi chuo, tulikuwa hatujafanya hilo. Tumepata uzoefu, matokeo yakitoka wengi wanajitokeza kusaidia. Katika tathimini ya mkoa hili tutaliangalia,” alisema Mtaka.

Kwa mujibu wa Mtaka, mwaka jana pia mkoa wa Simiyu ulipata mwanafunzi aliyefaulu kwa alama 7 kutoka shule ya serikali. Alitoka Shule ya Sekondari ya kata ya Nkololo wilayani Bariadi. Akizungumzia kambi za kitaaluma, Mkuu wa Mkoa alisema zimekuwa na faida kubwa.

Alisema mwaka 2016 alipofika Simiyu, katika mitihani yote ya kitaifa; darasa la nne, la saba, kidato cha pili, cha nne na sita, mkoa ulikuwa ukishika nafasi za 26,25 na 22.

“Lakini leo katika mitihani yote, mkoa umeingia kumi bora. Utaona mwaka 2016 katika kidato cha nne tulikuwa wa 22, mwaka 2017 wa 14, mwaka 2018 wa tisa na mwaka 2019 tukawa wa tano. Wakati huo huo katika Darasala la Saba mwaka 2018 tulikuwa wa 22, mwaka 2019 namba tisa,” alisema Mtaka.

Kwa mujibu wa Mtaka, mwaka jana, katika matokeo kwa shule za serikali, Simiyu iliingiza watoto wanne katika 10 bora na shule moja katika shule 10 bora. Mtaka alisema jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa na serikali ni kutafuta namna ya kusaidia watoto, kuondokana na kusafiri umbali mrefu kwenda shule.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

1 Comments

  • avatar
    Tawhidy:From shinyanga
    16/01/2020

    Comment Hongera sana Rais wetu kwani amekua mkombozi wa familia za kimaskini kama ataendelea na msimamo huu Tanzania Ujinga tutabaki kuuskia kwenye vyombo vya habari kutoka nchi zingine

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi