loader
Picha

JPM awapa mtihani mabalozi wapya

MABALOZI wapya wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Nigeria, wametakiwa kutengeneza ajira za Watanzania katika nchi hizo.

Hayo yalibainishwa jana na Rais John Magufuli wakati akiwaapisha mabalozi wapya wanne Ikulu jijini Dar es Salaam ikiwa ni moja ya mitihani yao watakapokuwa wameripoti katika ofisi zao.

Mabalozi hao ni Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi anayewakilisha Tanzania nchini Afrika Kusini, Dk Modestus Kipilimba (Namibia), Profesa Emmanuel Mbennah (Zimbabwe) na Dk Benson Bana nchini Nigeria.

Rais Magufuli aliwataka Mabalozi hao kutimiza majukumu yao kwa faida ya taifa ikiwemo kutengeneza ajira kwa Watanzania katika nchi wanazowakilisha. Aliwataka kutambua kuwa kila nchi kati ya hizo wanazokwenda ina umuhimu wake katika kujenga uchumi wa Tanzania, hivyo wanapotimiza majukumu yao watambue kuwa wanaliwakilisha taifa lenye mwelekeo mpya katika maendeleo ya watu wake.

“Nchi ya Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), mnafahamu mikakati tuliyonayo Tanzania ndani ya SADC katika kujenga maendeleo na uchumi wa kisasa, nchi zote nne tunazowapeleka ni umuhimu katika kujenga uchumi, nina matumaini makubwa kuwa mtafanya kazi kwa mujibu wa sheria ya nchi yetu, hivyo kasimamieni uchumi wa taifa letu,”alisisitiza Rais Magufuli.

Ili kuondokana na utamaduni wa hapo awali kwa wateuliwa kuchelewa kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi, Magufuli alimtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi kumkabidhi barua za Mabalozi hao ili ikiwezekana ndani ya wiki moja au mbili wawe wameripoti kwenye vituo vyao vya kazi.

Alisema mtu anapoteuliwa anatakiwa kwenda kuchapa kazi na siyo kuanza kuzunguka kwenye ofisi mbalimbali kwa ajili ya kuaga kwani jambo hilo linakinzana na dhana ya hapa kazi tu.

Kwa upande wake Waziri Kabudi aliwataka Mabalozi hao wapya kuhakikisha taifa linanufaika na fursa zilizoko kwenye nchi wanazokwenda kuwakilisha ikiwemo fursa ya kufundisha Lugha ya Kiswahili. Alisema nchi ya Afrika Kusini ambako Balozi Milanzi anakwenda walishakubali Kiswahili kianze kufundishwa nchini humo, hivyo akamtaka akalisimamie jambo hilo na ikiwezekana kabla ya Februari liwe limekamilika.

“Fursa hii ya kufundisha Lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini ilikuwa imeshatuteleza, lakini kutokana na juhudi za Rais Magufuli za kukutana na kuzungumza na Rais Cyril Ramaphosa alipofanya ziara nchini humo, zimesaidia kuturudishia tena fursa hii, lazima tukiri kwamba uzembe wetu ulichangia kutaka kuikosa fursa hii, kwa hiyo Balozi, kabla ya Februari jambo hili liwe limekamilika ili tusifanye tena kosa la pili la kuipoteza fursa hii,”alieleza Waziri Kabudi.

Kuhusu Ubalozi mpya wa Tanzania nchini Namibia, alimwelekeza Balozi Dk Kipilimba anayekwenda nchini humo kuhakikisha taifa linanufaika na utalaam na teknolojia ya uvuvi wa bahari kuu ambapo Namibia wamepiga hatua kubwa katika sekta hiyo pamoja na sekta ya nyama. Mbali na hilo pia alimtaka ahakikishe Tanzania inanufaika na fursa ya kuuza nafaka nchini humo.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Profesa Emmanuel Mbennah, ametakiwa kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na fursa nyingi za kibiashara zilizomo nchini humo. Alisema wananchi wa Zimbabwe walifarijika na ziara ya Rais Magufuli nchini humo kwani ilikuwa muhimu katika kupaza sauti na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuiondolea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi.

“Dk Bana unakwenda Nigeria kumwakilisha Rais katika nchi 16 ambazo zipo zinazozungumza Kifaransa na zingine Kiingereza, ni eneo kubwa sana la Afrika Magharibi, tunahitaji kulijengea mkakati, nchi kama Ivory Coast inazalisha tani 750,000 za korosho kwa mwaka ikilinganishwa na tani 250,000 ambazo Tanzania tunazalisha kwa mwaka,”alisema Profesa Kabudi.

Alisema Wizara yake ilishaanza mazungumzo na Waziri wa Kilimo wa Ivory Coast, hivyo akamtaka Balozi Bana afuatilie ili kuona namna bora ya kushirikiana nao katika suala la korosho hususani katika kuongeza thamani ya zao la korosho na mikakati ya uuzaji wa zao hilo. Mbali na korosho, alisema Ivory Coast wamefanya utafiti mkubwa wa kahawa na kufanikiwa kuunganisha Robusta na Arabica, hivyo akamtaka Dk Bana pia afuatilie jambo hilo ili taifa linufaike na utalaam huo kupitia ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Kwa kutambua kuwa Dk Bana ana vituo vingi vya nchi 16, Profesa Kabudi alimweleza Rais kuwa wanakamilisha taratibu ili ikiwezekana Rais aweze kumpunguzia baadhi ya vituo anavyovisimamia na vihamishiwe Algeria. Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana, kabla ya kuwaapisha Mabalozi hao, Rais Magufuli aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mawaziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na Naibu Katibu Wakuu, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wengine mbalimbali walihudhuria hafla hiyo ya kuapishwa kwa Mabalozi hao.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi