loader
MO awatuliza Simba

MO awatuliza Simba

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ ametengua kauli yake ya kujiuzulu nafasi hiyo baada ya jana kuandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa twitter uliosababisha sintofahamu kwa mashabiki, wanachama na wadau wa soka.

Awali, baada ya Simba kufungwa mchezo wa Fainali wa Kombe la Mapinduzi kwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar juzi uliochezwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, Dewji aliandika ujumbe wa kuachia ngazi na atabaki kama mwekezaji tu.

“Ni huruma Simba kutoshinda, baada ya kulipa mishahara inayokaribia Sh Bilioni nne kwa mwaka, najiuzulu kama Mwenyekiti wa Bodi na kubakia mwekezaji, Simba Nguvu Moja, nitatia nguvu kwenye kuendeleza miundombinu na soka la vijana,” ujumbe wa MO.

Baada ya kutoa ujumbe huo uliozua mijadala mbalimbali kwenye vyombo mbalimbali vya habari, mwekezaji huyo kwa mara nyingine jana aliandika ujumbe mwingine kwenye mtandao huo akionesha kujutia kitendo hicho.

Ujumbe huo ulisomeka hivi: “Kilichotokea kwenye akaunti zangu jana (juzi) kilikuwa ni bahati mbaya, tuko pamoja, tunarudi kwenye ligi tukiwa na nguvu, tunajipanga kwa ajili ya ligi, nawapongeza Mtibwa Sugar kwa kuchukua kombe, mimi ni Simba damudamu, nitabaki kuwa Simba,” Kabla ya kuandika ujumbe wa pili, baadhi ya wadau waliguswa na ujumbe huo na kutoamini kama kweli ni yeye mwenyewe aliyefanya hivyo, huku wakiwatia moyo mashabiki na wanachama kuwa watulivu.

Mmoja wa wadau hao ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyeandika ujumbe huu: “Matokea ya mpira huleta furaha na huzuni kwa wanaofungwa. Natoa pole kwa timu yangu ya Simba pamoja na mashabiki wote na wanaoitakia mema Simba. “Sina uhakika na kinachoendelea kwenye akaunti ya MO kama ni Mo Dewji mwenyewe. Nawaomba wanasimba tutulie tutapata ukweli muda si mrefu. Tusisahau kuwa wapo watu pia wabaya hutumia mwanya huu kuvuruga amani na utulivu wa timu zetu. Simba nguvu moja.”

Mdau mwingine wa soka, Ridhiwan Kikwete aliandika ujumbe huu baada ya MO kutangaza kujiuluzu: ”Naheshimu sana maamuzi ya mtu lakini kaka sina hakika kama kafanya busara katika hili. Hela hazinunui ushindi, ni haki yao kulipwa kwa kazi wanayoifanya. Tafadhali usifanye hasira. Huu ni mpira tu na matokeo yako matatu. Ninaamini utalifikiria tena uliloamua,” Kuhusu mchezo wa juzi, Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema licha ya kushinda mchezo huo, Simba walikuwa ni bora mwanzo mwisho isipokuwa walichofanya ni kuzima mbinu zao.

“Simba walikuwa bora mwanzo mpaka mwisho, siwezi kusema walikuwa dhaifu. Mimi niliwabana kwa mbinu wala sisemi kama nilikuwa bora, nilikuwa nacheza na timu bora ndio maana nilikuwa makini kuangalia mbinu zao ambazo walikuwa wanajaribu lakini yote yote tukashinda,” Alisema ushindi huo kwao ni historia kwani mara ya mwisho kuchukua ni mwaka 2010. Nahodha wa Simba, John Bocco alisema:

“Tunashukuru Mungu tumemaliza salama, tunawapongeza Mtibwa kwa kucheza vizuri. Tunajipanga na michezo ya ligi iliyoko mbele yetu,”alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/438cbda061951412212139fe29edbfe3.jpg

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi