loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mambo mazito uzimaji laini

LAINI zaidi ya milioni 20 za simu, zilizokuwa zinatumiwa na wananchi zenye usajili tata, zimeanza kuzimwa usiku wa kuamkia leo. Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la serikali la kutaka laini zote za simu zisajiliwe kwa kutumia kitambulisho cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Akizungumzia uzimaji wa laini za simu, ambazo hazijasajiliwa kwa Kitambulisho cha Taifa au Namba ya NIDA, Dar es Salaam jana, Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala hadi jana laini milioni 28.42 sawa na asilimia 58.2 za laini zote zilikuwa zimesajiliwa.

“Hadi sasa laini zilizosajiliwa ni milioni 28.42 sawa na asilimia 58.2 ya laini zote zaidi ya milioni 40 za simu zinazotumika nchini, hii ina maana kuna laini nyingi ama zinatumika au la lakini usajili wake wa alama ya kidole haujakamilika hadi leo,”alisema Mwakyanjala.

Akizungumzia utata wa laini uliojitokeza, ambapo zaidi ya laini milioni 16,187,616 usajili wake haueleweki hadi sasa kama ziko hai au laha, yaani kama zinaendelea kutumiwa au la. Kwamba kinachofanywa sasa ni uhakiki wake, ili kubaini zinazotumika na kufuta zisizotumika.

“Kwenye hili unaona laini ipo ila haina kumbukumbu yoyote, sasa unashindwa kutambua huyu mtu laini inatumika au la, ndio maana uhakiki unafanywa sasa ili kuondoa zile zisizotumika au labda wanaozitumia wamekufa,”alisema Mwakanjala.

Alisema katika utata huo, yapo makundi manne, moja ni hilo na la pili ni wale waliosajili laini kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa, lakini hawajathibitisha usajili wao kwa alama ya kidole, ambao idadi yao hadi sasa ni 318,950.

Alisema katika kundi hilo, laini hizo zitazimwa na kuwataka wananchi kama hawajui kama laini zao zimesajiliwa ipasavyo au la, wapige namba *106#OK kuangalia usajili wao ili wajitambue.Kama hawajakamilisha, basi waende kukamilisha. Kundi la tatu lenye utata ni la wananchi ambao majina yao matatu na tarehe na mwaka wa kuzaliwa, vinafanana ambao idadi yao wako 332,095.

Kwamba usajili huo ni tata, kwa sababu haiwezekani kila taarifa ifanane . Kundi na nne lenye utata ni la wananchi milioni tatu, ambao majina yao mawili yanafanana. Hilo nalo ni suala tata .

“Kuna hayo makundi niliyotaja hapo juu yana utata katika usajili wa laini za simu sasa kama simu yako hujui usajili wake umekamilika, ni vyema ukatumia namba hiyo *106#OK kuhakikisha kama umesajiliwa sahihi. Iwapo kuna dosari ni vyema uende kufanya marekebisho, vinginevyo laini tunazizima,”alisema Mwakyanjala.

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dk Arnold Kihaule, alisema zaidi ya asilimia 80 ya watu waliojiandikisha, kupata Kitambulisho cha Taifa wameweza kusajili laini zao, baada ya kupata namba ya utambulisho.

Alisema hayo ni mafanikio makubwa kwa NIDA, japo wanakabiliana na baadhi ya changamoto, kwani baadhi ya waombaji, uraia wao unatiliwa shaka. Wengine wana viambatanisho vinavyotofautiana.

Hivyo, NIDA inalazimika kujiridhisha kwa kushirikiana na mamlaka zingine ikiwemo Idara ya Uhamiaji, kabla ya kumpatia mwombaji Namba au Kitambulisho kamili.

Dk Kihaule alisema Namba zote za Utambulisho ambazo NIDA inazizalisha, zinatumwa wakati huo huo kwenda kwa wananchi kupitia namba zao simu, walizoweka kwenye fomu zao za maombi.

“Kuna changamoto tuliyoibaini kwamba baadhi ya wananchi walitumia namba ama za watendaji wao kata au serikali za mitaa, hivyo tunapowatumia namba za utambulisho zinakuwa haziwafikii kwa urahisi au hawazipati kwa sababu namba za simu walizotumia siyo za kwao. Kwa hiyo kama walitumia namba za watendaji wa kata au mitaa, wanatakiwa waende huko kufuatilia namba zao,”alisema Dk Kihaule.

Kwamba Vitambulisho vya Taifa vinawahusu raia na wageni. Kwa wageni, vitambulisho hivyo vinatolewa kwa wageni wakaazi, wanaoishi nchini kwa muda wa zaidi ya miezi sita, wakiwemo viongozi wa dini au wataalam mbalimbali. Lakini, wanaoishi chini ya miezi sita, hawapaswi kupewa vitambulisho hivyo.

Kwa mujibu wa Dk Kihaule, baadhi ya mikoa iliyofanya vizuri katika utoaji wa Vitambulisho vya Taifa ni Tanga na Morogoro. Mikoa ambayo ina changamoto ni ile ya mipakani hususani Kigoma, Katavi, Rukwa, Songwe na Kagera.

“Mkoa wa Kigoma ndiyo wenye changamoto zaidi kutokana na mwingiliano mkubwa kati ya wenyeji na wageni pamoja na walowezi, kwa hiyo lazima tujiridhishe kwa kushirikiana na mamlaka zingine ili vitambulisho visitolewe kwa wasiohusika, ndiyo maana maombi ya wananchi kwenye mikoa hii lazima yapitie kwenye Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya, Mkoa hadi Taifa na majibu yao yanarudishwa kwa njia hiyo hiyo,”alisema Dk Kihaule.

Makonda anena

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema amesikitishwa na wananchi kulichukulia kwa mzaha suala la kupata Kitambulisho cha Taifa na kusajili laini zao kwa alama za vidole.

Aliema hayo jana alipotembelea Ofisi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Wilaya ya Temeke na Viwanja vya Mnazi Mmoja Wilaya ya Ilala.

Makonda alisema, kabla ya Desemba 27, Rais Dk John Magufuli alipoongeza muda wa kusajili laini hadi kufikia jana Januari 20, watu walikuwa wakimiminika kusajili laini zao.

Lakini baada ya Rais kuongeza muda, wengi wao walipuuza na kuendelea na shughuli zao na matokeo yake wakajikuta muda umeisha na laini zao kuwa kwenye hatari ya kufungwa.

Aliwataka wananchi kuwa makini na mambo ya kitaifa, yakiwemo ya vitambulisho vya taifa, kusajili laini kwa alama za vidole, kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura, kubadilisha pasipoti na kupata pasipoti mpya za kielektroniki.

Alisema mambo hayo ni muhimu kwao, lakini pia yanaisaidia serikali kutoa huduma stahiki kwa wananchi wake.

“Wangapi kati yenu mnatumia mitandao ya kijamii kupeana taarifa za hovyo, lakini linapokuja jambo la maendeleo, jambo linaolohusu nchi na maisha yenu, hamna mpango, cha kusikitisha jambo la kitaifa kama hili la vitambulisho vya taifa kuna watu wanatumia mitandao kufanya mzaha, badala ya kuhamasishana, tunafanya maisha yetu yote kama ya zimamoto,”alisema Makonda.

Wakati huo huo, jana ikiwa ni siku ya mwisho ya usajili wa laini za simu, mitandao ya simu katika kampuni mbalimbali, ilikuwa ikisumbua kwa kushindwa kupata mawasiliano ya kimtandao kutoka Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA).

Habari Leo lilishuhudia wananchi wakisubiri kwa muda mrefu kutokana na kukatika kwa mawasiliano hayo ya kimtandao nchi nzima na kukaa wakisubiri urudi ili wasifungiwe laini zao.

Mkazi wa Goba, John Joseph alisema amefika tawi la TTCL, lililopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, saa mbili asubuhi na kuondoka saa tano na nusu kutokana na tatizo hilo la mtandao.

Wafanyakazi wa TTCL, walisikika wakisema kuwa wamekuwa wakiwasiliana na wenzao toka kampuni nyingine za simu nao wameelezea kupata changamoto hiyo ya kimtandao.

Juzi usiku katika maeneo ya Goba kwa watu binafsi waliokuwa wakisajili laini hizo, kulikuwa na misururu mirefu ya wananchi wakisubiri kusajiliwa, inasemekana wapo waliokuwa kwenye foleni kuanzia saa 10 hadi saa tano usiku.

Mkoani

Tanga kumeibuka changamoto nyingine ya kimtandao ambayo watu wengi wameendelea kusota kwenye vituo na mawakala wa kusajili laini za simu.

Tatizo hilo ni kuwa licha ya watu kupata namba za Kitambulisho cha Taifa kutoka NIDA, watu wengi waliojitokeza kwenye vituo vya mawakala wa mitandao ya simu kusajili laini za simu walikumbana na changamoto ya mitandao kusumbua.

Gazeti hili lilitembelea baadhi ya vituo na mawakala wa mitandao ya simu kuanzia jana na juzi na kukuta watu wakiwa kwenye foleni wanasubiri kusajiliwa laini zao hadi majira ya saa 4:00 usiku wakiambiwa kuwa mtandao unasumbua.

Mkazi wa Mwakidila Kata ya Tangasisi jijini hapa, Juma Ally (54) ambaye alikuwa akisubiri huduma ya kusajiliwa laini zake tatu za mitandao ya Vodacom, Tigo na Halotel alisema kuwa kila kituo anachokwenda anaambiwa kuwa mtandao unasumbua.

“Nimekwenda Tigo kule mjini nimekuta foleni kubwa ya watu na kuambiwa mtandao unasumbua, nimekuja hapa Stendi Barabara 12 kwenye ofisi za Vodacom na Halotel pia nimeambiwa hivyo hivyo, sasa sijui nifaye nini?,”alihoji.

Halidi Mohamed ambaye ni dereva wa teksi anayefanya shughuli zake mitaa ya Posta, alisema kuwa tangu juzi alitumiwa kwenye mtandao wa Vodacom kiasi cha Sh 50,000, lakini kila alipojaribu kutoa, alikuwa anaambiwa kuwa mtandao unasumbua aendelee kusubiri.

Wakala wa usajili wa mtandao wa Tigo jijini Tanga, Christopher Makundi alisema hali hiyo imesababishwa na msukumo mkubwa wa watu uliotokea hivi karibuni kwa watu kutaka kusajiliwa laini zao za simu kwa alama za vidole, kwa kuogopa kufungiwa, hivyo mtandao unazidiwa.

Mkoani Dodoma, usajili huo umekumbwa na changamoto nyingi zikiwemo za mitandao ya simu, kukosa mawasiliano kwa urahisi.

Changamoto nyingine ni baadhi ya wananchi hasa wa vijijini, kutokuwa na elimu ya kutofautisha usajili wa laini za simu na upatikanaji wa vitambulisho vya taifa, wakiamini kwamba kuzimwa kwa laini za simu kunakweenda pamoja na kutopatikana kwa namba za vitambulisho vya Nida.

HabariLeo ilitembelea jana Viwanja vya Nyerere jijini Dodoma na kukumbana na misururu mirefu ya watu, wanaotaka kusajili laini zao, lakini wanashindwa kusajili kutokana na mitandao ya simu, kutofanya kazi kwa haraka kutokana na kuzidiwa na idadi kubwa ya wasajili.

“Tunahangaika kusajili laini lakini mitandao ya simu haipatikani kwa urahisi na kutufanya tupoteze muda mrefu kusubiri,” alisema Hamis Ali(40). Mwananchi mwingine Mwajuma Hamad (42) alisema tangu juzi alikuwa wakisumbuka kusajili simu baada ya kupata namba ya Nida, lakini kutokana na mitandao ya simu kusumbua ni vigumu kupata mawasiliano.

Juma Ali kutoka Wilaya ya Chamwino alisema watu wengi hasa vijijini, hawasajili laini zao wamekataa tama, kwamba zitazimwa. Lakini, pia wamekataa tamaa kufuatilia namba za Nida wilayani, bila kujua kwamba kuzimwa kwa laini, si kusimamisha upatikanaji wa namba za Nida.

Mwanahamisi Ali (58) akizungumza baada ya kupiga picha kwenye banda la Nida, alisema anatakiwa kufuatilia namba yake kutoka Bahi baada ya wiki tatu, kwani wakati huo simu zake zitakuwa zimezimwa kwani ameshindwa kusajili kutokana na kukosa namba ya Nida.

Kwa wilaya ya Tarime mkoani Mara, watu 162,000 kati ya 164,000 wamesajiliwa katika vitambulisho vya taifa sawa na asilimia 99 kufikia Januari 19.

Ofisa NIDA Wilaya ya Tarime, Michael Msoke alisema kuwa changamoto ambazo zimejitokeza na kufanya uandikishaji kuchukua muda ni wananchi kutokuwa na kumbukumbu sahihi ya majina yao matatu walioandikisha siku za awali. Hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa, kuchelewesha upatikanaji wa majina katika mashine zao.

Kutoka Morogoro, Wananchi waliokuwa hawajasajili laini zao kwa njia ya alama za vidole kwa kutumia namba ya kitambulisho cha taifa, wamekabiliwa na usumbufu wa mitandao kushindwa kutoa mrejesho wa kuthibitisha usajili wao.

Mbali na changamoto hiyo, pia kundi la wazee na watu wengine wachache, walikumbwa na changamoto za vidole vyao kuwa na usugu, kiasi cha mashine ya kuchukua alama hizo, kushindwa kuwatambua.

Mkazi wa Mwenyesongo , Zainabu Msumi ambaye alikuwa bado katika mchakato wa kurejesha fomu yake ili aweze kupigwa picha, alisema hakupata elimu ya kutosha juu ya namna ya ujazaji wa fomu na viambatanisho vinavyohitajika ili kuwezesha kusajiliwa na kupata namba ya NIDA ili aweze kusajili laini yake kwa njia ya alama za vidole.

Ofisa Msajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA ) Mkoa wa Morogoro, James Malimo alisema kuanzia Januari mosi mwaka huu hadi jana, wafanyakazi wa ofisi hiyo walikuwa vijijini katika halmashauri zote tisa za mkoa huo kuendesha zoezi la usajili wa namba za Nida.

Wakati huohuo, Chama cha ACT- Wazalendo kimesema leo kitaishitaki serikali mahakamani, iwapo laini za simu zisizosajiliwa kwa alama za vidole, zitafungwa.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alisema kuwa iwapo leo simu hizo zitazimwa, basi wataifungulia kesi serikali, kuitaka kubadilisha uamuzi wa kuzifungia laini hizo.

Ado alibainisha kuwa sababu kubwa ya watanzania wengi, kushindwa kusajili laini zao inatokana na Nida kushindwa kuwapatia namba za kitambulisho. Alisema kushindwa huko kunatokana na mamlaka hiyo, kutowezeshwa kikamilifu.

Alisema iwapo kama NIDA ingekuwa katika kila wilaya, basi kila Mtanzania anayestahili kuwa na

kitambulisho cha taifa angekuwa nacho, hivyo usajili ungefanyika kirahisi. Alisema maisha ya watanzania wengi, yapo kwenye simu, kwa kuwa wengi wanafanya biashara na kuendesha maisha yao kupitia simu hizo.

Hivyo, alisema kuzizima ni kuwakosesha haki ya msingi ya mawasiliano, ambayo ni muhimu kwa kila mwanadamu.

Alisema pia simu zikizimwa, serikali inaweza kukosa mapato kwa asilimia kubwa, kwa kuwa inategemea kodi kutokana na miamala inayofanywa kupitia simu hizo.

Alisema “Kuna fedha nyingi zinazopitia kwenye miamala ya simu mfano kwa kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka jana takribani trilioni 16 zilizunguka nchini katika miamala ya simu na hivyo hata serikali ilipata kodi hapo” alisema.

Katika hatua nyingine, Ofisa Msajili Msaidizi wa Nida Mkoani Shinyanga, Haroon Mushi na Wakala wa usajili laini za simu za mkononi, Victor Isack Vicent, wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kutoza wananchi Sh 30,000 ili wawapatie namba za Nida na kwenda kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole.

Tukio hilo ni la jana majira ya saa 7:00 mchana wakati Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, alipofika ofisi za mamlaka hiyo Shinyanga mjini na kupata taarifa hizo za wananchi, kuombwa fedha ili wapate namba za Nida.

Mboneko alisema wakati akiwa kwenye ofisi hizo za Nida, alipata taarifa hizo za uombwaji fedha wananchi kutoka kwa wakala wa usajili la laini za simu za mkononi, ambaye alikuwa akifanya mawasiliano na ofisa huyo wa Nida.

Mara baada ya kumkamata wakala huyo wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama ya vidole, walipomfikisha Polisi na kuanza kumhoji kwa nini anatoza fedha wananchi ili awapatie namba za Nida, wakati yeye siyo mtumishi wa Nida, ndipo alisema huwa anashirikiana na mmoja wa maofisa na Nida na kumtaja kwa jina.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Joseph Paulo, alithibitisha kuwakamata watu hao wawili.

Alisema upelelezi bado unaendelea na wamewakabidhi Takukuru. Kwamba upelelezi ukikamilika, watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Imeandikwa na Ikunda Erick, Evance Ng’ingo, Lucy Ngowi na Matern Kayera, Dar, Kareny Masasy, Shinyanga, Magnus Mahenge, Dodoma, John Nditi, Morogoro, Samson Chacha, Tarime na Cheji Bakari, Tanga.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi