loader
Picha

Wizara yaanzisha grupu kukabili vikwazo

TANZANIA imedhamiria kukabiliana na vikwazo, vinavyowakabili wafanyabiashara mipakani, kwa kuanzisha mfumo wa kupokea taarifa kuhusu kikwazo chochote, kinachotokea na kukipatia ufumbuzi haraka.

Katika kuwasaidia wafanyabiashara mipakani, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), imeanzisha kundi (grupu) maalum katika mtandao, linalounganisha wataalamu na watendaji wakuu wa taasisi zote husika ili kurahisisha upatikanaji wa haraka wa taarifa kuhusu kikwazo chochote, anachokumbana nacho mfanyabiashara wa Tanzania mpakani na kutafuta ufumbuzi wa haraka.

Akizungumza na HabariLeo Afrika Mashariki kuhusu vikwazo vya biashara mipakani, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema wizara hiyo imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuhusu vikwazo wanavyokutana navyo, wanapopeleka bidhaa zao katika masoko ya nchi za jirani.

“Hii inaondoa maana ya soko huria ambalo viongozi wa mataifa ya Afrika akiwamo Rais wetu Dk John Magufuli, wamekuwa wakipigania liwapo ili kuondoa utegemezi wa bidhaa za nje ya Bara na kujenga uchumi wa mataifa yetu,” alisema.

Waziri huyo alisema Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wizara na taasisi nyingine, wanawasiliana na nchi jirani kushughulikia vikwazo vinavyojitokeza na kuzitaka hizo kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara wa Tanzania.

“Nawasihi wafanyabiashara wa Tanzania kuwasiliana nasi kupitia mfumo huo pale mnapopata vikwazo mipakani ili tuchukue hatua stahiki na haraka.

“Tunachotaka ni wafanyabiashara wetu kupanua wigo wa kibiashara kwenye nyanja za kimataifa bila vikwazo kwa kuanzia na masoko ya nchi majirani wetu,” alisema.

Bashungwa alisema kipindi cha nyuma wafanyabiashara wa Tanzania, walikuwa hawapati fursa ya kukaa na wizara husika na kueleza aina ya vikwazo wanavyovipata, lakini sasa kuna utaratibu wa kuwasiliana na wizara mara wanapopata vikwazo.

Akizungumzia mawasiliano na wafanyabiashara katika mipaka yote ya Tanzania, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa TanTrade, Twilumba Mlelwa alisema wameunda kundi (grupu) katika mtandao wa kijamii lenye wafanyabiashara, maofisa watendaji wa taasisi za kibiashara kama TanTrade, Mamlaka ya Mapato, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na nyinginezo.

Alisema katika kundi hilo, wamekuwa wakipata taarifa za vikwazo vya biashara katika mipaka yote nchini na kuvitafutia suluhisho la haraka na kisha mhusika kupewa taarifa.

Alisema tangu kuanzishwa kwa kundi hilo, wamefanikiwa kutatua vikwazo mbalimbali hasa katika mpaka wa Tunduma.

Mlelwa alisema vikwazo vingine mipakani, husababishwa na watendaji kutotimiza wajibu wao, hivyo kwenye kundi hilo wataalamu waliopo hutoa njia muafaka kwa watendaji ili kutatua suala hilo kwa kupeleka taarifa haraka na kupata muafaka kwa wakati.

WAFANYABIASHARA wa mchele mkoani hapa wameomba kuwepo kwa soko la ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi