loader
Serikali yagawa mashine 7,200 ukusanyaji mapato

Serikali yagawa mashine 7,200 ukusanyaji mapato

SERIKALI imeandika historia mpya ya Mkakati wa Kukusanya Mapato kwa kugawa mashine 7,227 za kukusanyia Mapato (POS) katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 185 ili kuongeza makusanyo ambapo halmashauri zenye makusanyo madogo zimepewa mashine nyingi zaidi.

Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri wametakiwa kwenda kutumia vizuri mashine hizo ambazo zimenunuliwa kutoka kwa mtengenezaji kwa Sh bilioni 2.3 na kuokoa Sh bilioni 4.2 kama zingenuliwa kwa wakala kwa Sh bilioni 6.5 zilivyonunuliwa za awali.

Akizungumza kabla ya kugawa mashine hizo zilizonunuliwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway jijini hapa jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo aliwaagiza Ma- RAS na Ma-DED kwenda kuongeza makusanyo ya mapato katika halmashauri.

Jafo alimpongeza Balozi wa Norway, Elisabeth Jacobson na akaomba apeleke salamu kwa serikali yake kwa kutoa ufadhili huo wa mara moja wa mashine 7,227 kuliko mashine 10,100, ambazo zilitolewa kwa muda mrefu.

Aliwataka watendaji hao kuongeza mapato ya serikali kwa kutumia mashine hizo bora na akawaonya watakaochezea wajue Tamisemi itakuwa inaona na haitasita kuwachukulia hatua watakaofanya hivyo.

Jafo aliahidi kwamba wiki ijayo atatoa ripoti za halmashauri zinazofanya vizuri katika makusanyo, zinazofanya vibaya na zinazotumia fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo likiwemo jiji la Dodoma ambalo mwaka jana 2018/19 lilitumia Sh bilioni 54 kwa ajili ya miradi.

Alisema mkakati wa serikali ni kuongeza makusanyo na kufikia lengo katika mwaka 2019/20 la kukusanya Sh bilioni 765 ambapo hadi Desemba mwaka jana zimekusanywa Sh bilioni 356 sawa na asilimia 46.53 tu.

Alizitaja baadhi ya halmashauri ambazo hadi Desemba mwaka jana zilikuwa na makusanyo chini ya asilimia 20 zikisemo za Gairo, Korogwe, Mafia na Ukerewe akasema zikatumie mashine hizo kuongeza mapato lakini akaonesha hofu kama zitafikia asilimia 60 ifikapo Juni mwaka huu.

Alisema tangu mashine zimeingia mwaka 2017/18 mapato yaliongezeka kufikia asilimia 81, mwaka 2018/19 yalifikia asilimia 90 na hivyo katika mwaka 2019/20 baada ya kupata mashine halmashauri zinatakiwa kuvuka lengo la mwaka jana.

Naye Katibu Mkuu- Tamisemi, Joseph Nyamhanga alisema mashine hizo zimenunuliwa Sh bilioni 2.327 sawa na Sh 320,000 kila moja kutokana na kununua kwa mtengenezaji moja kwa moja tofauti na zile za awali zilizokuwa zikinunuliwa kwa Sh 900,000.

Mashine hizo zilizokabidhiwa kwa Ma-RAS kupitia Mwenyekiti wao, Rehema Madenge wa Lindi na DED wa Jiji la Mwanza, Kilomoni Kibamba zimegawiwa kwa halmashauri zilizopangwa katika makundi A hadi E kwa kutumia fomula ambapo halmashauri kumi zinazofanya vizuri kila moja ilipata mashine 10 kila moja.

“Kundi B lina halmashauri nane ambazo zina mapato kati ya Sh bilioni tano hadi 10, hizo zitapewa mashine 15 kila mmoja. Wakati halmashauri 29 zenye mapato pungufu ya hapo zitapewa mashine 25 kila mmoja,” alisema.

Alisema kundi la halmashauri 101 ambazo zina mapato chini ya bilioni tato zitapewa kila moja mashine 47 ili kuongeza makusanyo zaidi, wakati kundi la halmashauri za mwisho lenye mapato chini ya Sh bilioni moja kwa mwaka zitapewa mashine 50 kila moja.

Nyamhanga alisema mashine hizo zimeboresha na tofauti na za zamani, zimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa haziruhusu kupiga na kupokea simu, zinaonesha rangi na nembo ya taifa na haziruhusu kutumia mifumo mingine na kubadili tarehe na zinafanya kazi ya makusanyo tu.

Naye Naibu Waziri Tamisemi, Josephat Kandege alisema serikali imenunua mashine hizo kwa Sh 320,000, halmashauri zinatakiwa zitakazoongeza mashine hizo zinatakiwa zisinunue mashine hizo kwa mawakala kwa bei kubwa ya zaidi ya Sh 900,000.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi