loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ni ushindi mkubwa

TANZANIA imeandika historia kwa kumaliza mazungumzo kati yake na kampuni ya madini ya Barrick baada ya kusainiwa mikataba tisa ikihusu uendeshaji wa kampuni mpya ya madini ya Twiga ambayo serikali ni mbia.

Mikataba hiyo ilisainiwa jana Ikulu, Dar es Salaam katika hafla ambayo Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick, Dk Mark Bristow amethibitisha kuandikwa kwa historia hiyo kwa kueleza kuwa kilichofanyika jana si historia kwa Tanzania pekee bali Afrika nzima.

Katika hafla hiyo, Rais John Magufuli alitumia maneno ya kiingereza ‘The Game is Over’ akimaanisha mvutano na mazungumzo ya muda mrefu baina ya Barrick na Serikali yamefikia mwisho kwa ushindi mkubwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mazungumzo kwa upande wa Serikali ya Tanzania, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Balamagamba Kabudi alieleza ugumu wa mazungumzo hayo yaliyoanza mwaka 2017 na namna alivyoandika barua ya kujiuzulu lakini ikachanwa kabla ya kumfikia Rais.

Mikataba iliyosainiwa ni Mkataba wa Msingi wa Makubaliano na Mkataba wa Menejimenti na Utoaji wa Huduma na Mkataba wa Wanahisa wa Kampuni ya Twiga. Mingine ni Mkataba Wanahisa wa Kampuni ya North Mara, Mkataba wa Wanahisa wa Bulyanhulu, Mkataba wa Wanahisa wa Kampuni ya Pangea Buzwagi, Mkataba wa Maendeleo wa North Mara, Mkataba wa Maendeleo wa Bulyanhulu na Mkataba wa Maendeleo wa Pangea.

Rais Magufuli aeleza ni ukurasa mpya Akizungumza baada ya utiaji saini wa mikataba hiyo, Rais Magufuli alisema kilichofanyika jana ni matokeo ya Watanzania wazalendo na Barrick wazalendo walioamua kutovunjika moyo kwa maneno ya kuudhi na kukatisha tamaa yaliyosemwa wakati mazungumzo yakiendelea miaka mitatu iliyopita.

“Leo ni siku muhimu sana si tu kwa Tanzania bali kwa Afrika nzima kwa suala linalohusu soko la madini. Nawashukuru Watanzania wazalendo walioanza tangu 2017 leo ni karibu miaka mitatu nawapongeza lakini zaidi namshukuru sana Mungu kwa kufamikisha hili.

“Kwa ndugu zangu Barrick nawahakikishia ‘Game is Over’. Kachapeni kazi sababu ninyi Barrick mna wataalamu na mtaji, sisi tuna malighafi. Dhahabu iliwekwa Tanzania si kwingine, aliyeiweka ambaye ni Mwenyezi Mungu ana makusudi nayo, ikisombwa tu bila Watanzania kupata faida kutoka kwa wale wanaosomba ndicho kinachoumiza, ndicho kilichoniumiza sana mimi,” alisema Magufuli.

Alisema mengi yamezungumzwa tena kwa hisia kali na waliotoa salamu kabla ya kusainiwa kwa mikataba hiyo na kubainisha kuwa, Profesa Kabudi mengine hakueleza, alivyokuwa akipata misukosuko na kuteseka na alimpongeza sana kwa kazi kubwa na ngumu aliyoifanya yeye na kamati nzima. Katika hilo la kujitoa kwa maslahi ya Taifa, Magufuli alisema,

“Mimi ni shahidi kwamba Watanzania wa kweli bado wapo nchini, wenye moyo kama wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, wanaotanguliza maslahi ya taifa kwanza kabla ya yao binafsi”.

Magufuli alisema kazi ya kuzungumza na kampuni kubwa duniani kama Barrick si ndogo huku akifafanua kama ingekuwa ni mchezo wa kushindana, ni kati ya tembo na sungura na ulihitaji nguvu ya Mungu zaidi.

Aliwashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuliombea taifa. Akieleza wakati wakishikilia kontena za mchanga zilizokuwa zikisafirishwa, Magufuli alisema kuwa waliambiwa kuwa ni mchanga na Watanzania wengi waliamini hivyo.

“Tukajiuliza kama ni mchanga, kwanini usafirishwe? kwa logic (mantiki) ya kawaida unaelewa kwamba haukuwa mchanga. Ni kweli mimi nimechukua chemistry (kemia) na mathematics (hesabu), ........najua pia kujumlisha na kutoa. Kama alivyosema Profesa (Kabudi) haya mambo yanahitaji kujitoa, bila hivyo haya yasingetokea,” alisema Dk Magufuli na kuongeza.

“Ndio maana ilinisumbua, wanasomba wanasema ni mchanga na Polisi wanasindikiza, sasa kama ni mchanga si bora usiende tu na uchukuliwe popote”. Akiwashukuru kampuni ya Barrick Magufuli alisema;

“Nawashukuru watu wa Barrick........., fikiria kutoka kwenye hisa ya ‘zero’ (sifuri) mpaka asilimia kumi na sita (16) na faida ya hamsini kwa hamsini ni ushindi kwa Barrick na kwa Serikali ya Tanzania,” alisema.

Akifafanua zaidi, Rais Magufuli alisema kihistoria ushirikiano wa awali uliokuwepo baina ya kampuni hiyo na Serikali haukuwa wa ‘win to win situation’ (kufaidika kwa pande zote mbili). “Ukiwa na ng’ombe ameshikiliwa na simba ukitaka kumtoa, Simba atakuua na wewe badala ya kukusamehe, huu ni ushindi mkubwa.

“Napenda kuwahakikishia Barrick na wawekezaji wote ulimwenguni Tanzania ‘is the best place’ (ni mahali pazuri) kwa uwekezaji, tuna utajiri mkubwa tunaotaka kushiriki kwa faida ya pamoja (win to win situation). Makubaliano haya yamemaliza mabishano pande zote,” alisema Magufuli.

JPM aipa neno kampuni ya Twiga kontena za makinikia Magufuli hakusita kuipa kazi kampuni mpya ya Twiga iliyoanzishwa Oktoba mwaka jana kwa kuwaeleza kutafutia wateja kontena za makinikia zilizokamatwa bandarini zilizokuwa zikishikiliwa na Serikali.

“Yale makontena tulioyashikilia bandarini mkatafute wabia muuze kwa faida ya Twiga, leo ni siku mpya na ukurasa mpya. Kwa kuwa tumesaini makubaliano haya. Mungu wetu anatuona na viongozi wa dini wameshuhudia, mkasimamie makubaliano haya.

“Kwa wale watakaowekwa kwa upande wa Watanzania, msiende kununuliwa. Watakaoteuliwa kwenda pamoja na majadiliano makubwa yaliofanyika wanaweza wakanunuliwa. Watakaochaguliwa wawe ‘vetted’ (wahakikiwe) na wasainishwe mahali commitment (makubaliano) maana wanabeba jukumu la Tanzania,” alisema Magufuli.

Rais alisema katika maeneo ya machimbo ya madini kuna watu wana njaa, hawana dawa, elimu na mengineyo hivyo aliwashukuru Barrick na wenye hisa kwa kutumia busara kuendelea na uwekezaji ila alionya kuwa hata wangegoma, wasingechimba dhahabu.

“Ila sina uhakika kama mngeichimba hiyo dhahabu ila kweli mmetumia busara kubwa. Serikali yangu itatoa ulinzi ili mchimbe mpate faida na maisha yaende,” alisema Magufuli na kusisitiza kuwa ndio maana amesema hata kontena zile zitafutiwe wateja.

Alisema anajua kuna utaratibu ulishataka kufanyika wa kuyauza na kusafirisha ili kuyeyusha jambo alilosema haikuwa kweli na kueleza kuwa anamjua mteja aliyetaka kununua na kama anataka kuja kununua sasa, anunue maana faida ni kwa wote. Magufuli aliomba ushirikiano uliooneshwa kufanikisha tukio hilo la kihistoria uendelee.

“Picha iliyooneshwa na Dk Mark ni ya upendo. Kama alivyosema Profesa Kabudi (awali akitoa salamu), mwaka 1978 alitumwa kaka yako kuja kuipiga hii Ikulu.

“Uvumilivu wa kaka yako kutokuja kuipiga umetuweka hapa leo, naye pengine angepigwa kabla hajaipiga. ‘The past is always history’ (yaliopita siku zote ni historia). Sasa tumeanza ukurasa mpya na tutasonga mbele kwa faida ya pande zote mbili,” alisema Rais.

Magufuli aliwashukuru pia kamati iliyoshiriki kwenye mazungumzo hayo na kuwaombea Mungu awalipe. “Nina uhakika Mungu atawalipa, wengine mmetoa machozi, malipo yenu mtayapata sababu mmetimiza lililo jema. Nawapongeza sana sana sana. Tulitakiwa tuwatafute wanasheria wakubwa tuwalipe madola lakini tukasema tutatafuta Watanzania wazalendo waongee na Wana Barrick Wazalendo”.

Magufuli aliwaomba Barrick waitangazie dunia kwamba Tanzania tunataka biashara ya faida kwa pande zote mbili, ni sehemu salama ya uwekezaji.

“Fanyeni kazi huko mkijua kuna Watanzania wanaotamani kuona faida inawarudia. Mkazingatie mazingira wananchi wasiathiriwe na chochote. Ukikuta watu wanahitaji maji, si vibaya kuwapatia hilo, ndio faida ya kuwepo huko,” alisema Rais Magufuli.

Salamu za Rais wa Barrick Awali kabla ya kusaini mikataba hiyo, wawakilishi wa kamati kwa upande wa Serikali na kampuni ya Barrick walipata nafasi ya kutoa salamu zao. Salamu za Barrick zilitolewa na Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Dk Mark Bristow. Dk Bristow aliyekulia katika jamii ya Wazulu nchini Afrika Kusini, alisema,

“Tumezoea kulalamika sisi Waafrika, tupunguze maneno, tufanye kazi. Unajua ukiwa Mwafrika wa kweli lazima uipende Tanzania, Tanzania inawakilisha kila kitu ambacho katika Afrika tunakipenda. Rais ni furaha yetu kurejea nyumbani”.

Alisema Profesa Kabudi ameelezea safari ndefu waliokuwa nayo tangu mwaka 2017 na leo hatima ya safari hiyo imefika katika nafasi ambayo safari ya maisha bado inaendelea.

“Kabudi amezungumza kuhusu mradi wa ushirikiano kupitia kampuni ya Twiga, leo tumeanza ushirika mpya. Ushirika ambao utakuwa 50 kwa 50. Twiga Mineral inawakilisha muundo unaoruhusu Serikali na Watanzania kushiriki maamuzi yote katika kila kitu ndani ya kampuni,” alieleza Dk Bristow.

Alimweleza Rais Magufuli kuwa, wanapokuja katika nchi kama Tanzania, wanabeba jukumu kubwa sana la kuvuna rasilimali za taifa si tu kwa ajili ya faida yao bali wadau wote katika nchi husika ambao ni pamoja na Watanzania na vizazi vyao vya baadae.

Dk Bristow alisema katika migodi yao kuna jamii ambayo lazima washiriki katika shughuli za kiuchumi.

Alisema kulikuwa na ukosoaji mwingi na maneno mengi katika safari hii. “Sisi tunaamini katika ushirika wa kweli na leo ni siku ya kihistoria kwa Afrika nzima.

Watu walikosoa msimamo wako kwamba unafukuza wawekezaji lakini safari imetulazimu kuamini kwamba hufukuzi wawekezaji bali unataka uwekezaji wenye faida kwa pande zote mbili,” alisema.

Alisema katika Afrika kuna tabia ya kulalamika sana, lakini 50 kwa 50 ina uhakika kwamba uamuzi unafanywa kwa pamoja na kusisitiza kuwa inapoamuliwa kwenda mbele kuna mengi ya kujifunza kutokana na makosa ya nyuma.

“Kama hujifunzi kwa yaliyopita hasa ya miaka 10 ya nyuma, haustahili kuwepo hapa. Mimi ni mtoto wa Kizulu, nimezaliwa jamii ya Kizulu, kuna msemo tunasema huwezi kuosha mkono mmoja bila kutumia mkono mwingine. Ninachotakiwa kufanya hapa ni kukupa mkono huo,” alisema Dk Bristow huku akimpa mkono wa shukurani Rais Magufuli.

Profesa Kabudi atoa ya moyoni Mwenyekiti wa kamati ya mazungumzo, Profesa Kabudi jana alipokuwa akitoa salamu kwa Serikali kwa niaba ya kamati, alieleza ya moyoni kwamba, kutokana na ugumu wa kazi hiyo, aliandika barua ya kujiuzulu lakini Kasmir Simbakuki alimnyang’anya na kuichana.

“Nilifikia hatua nikafanya dhambi ya kukata tamaa, nikasema jambo hili haliwezekani, niliona ni bora aibu na fedheha hiyo niibebe lakini barua niliyoiandika sikufanikiwa kuileta kwako,” alisema Profesa Kabudi.

Kabudi alisema kipindi hicho alikuwa katika hali ngumu kwani Rais Magufuli alikuwa mara kwa mara akimpigia kumuuliza maendeleo yalikofikiwa huku Bungeni, wabunge waliuliza majadiliano yalikofikiwa wakati hayakuwa yakienda vizuri.

Alisema kuna wakati walikuja Wachina kuwekeza lakini waliingia mitini, wakati ambao Rais naye alihitaji majibu ya kinachoendelea, bungeni akipigwa mijeledi na kuona kuna aibu kubwa italikumba Taifa lakini alimshukuru Mungu kwa ushindi uliofikiwa.

Profesa Kabudi alisema jitihada walizofanya ni za kusafisha takataka zilizokuwa zimesalia na kuwataka Watanzania wavumilie kupata nyumba mpya safi. Alisema hata hivyo uchafu hauwezi kuisha wote mara moja.

Alitumia nafasi hiyo kuomba radhi kwa Watanzania kwa mapungufu yoyote na kueleza huo ni mkataba wa mwisho usiostahili lawama kwa Serikali ya Magufuli lakini mingine yote ijayo chini ya uongozi huu, wabebeshwe lawama.

Safari ya Mazungumzo

Profesa Kabudi alisema safari ya mazungumzo iliyoanza mwaka 2017 ilifanikisha kuanzishwa kwa kampuni ya pamoja ya Twiga Minerals Corporation, Oktoba, mwaka jana ili kusimamia migodi ya madini ukiwamo wa North Mara na kufungwa kwa Acacia London na Johannesburg, Afrika Kusini.

Alisema kampuni ya Barrick waliahidi kufikia hamsini kwa hamsini na wamelisimamia hilo pamoja na mvutano na majadiliano marefu na kufanikisha Tanzania kupata faida ya asilimia 16 za hisa kwa mfumo wa ‘undiluted’ ya mtaji mpya na kila ikiongeza mtaji inabaki hivyo.

“Iliingia awamu ya pili ya mkataba huu Toronto na London. Hawakutaka mikataba hii isainiwe, mkikubaliana leo, kesho wanageuka. Luteni Richard Williams akijitahidi na kupingwa na wenzake. Hapo ndipo nilipoandika barua ya kujiuzulu kuja kwako,” alisema.

Alisema ni mwaka mmoja na siku kadhaa tangu mafanikio haya yaanze kuleta nuru na alimweleza Rais Magufuli kuwa, wawekezaji hao wa sasa ni watu wa kweli, wagumu, ving’ang’anizi lakini ukikubaliana, ni makubaliano ya uhakika.

Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, hiyo ndio mikataba ya mwisho na kueleza kuwa leseni za wawekezaji wa madini sasa zitakuwa zinafanana na zitatolewa na Kamisheni ya Tume ya Madini kwa ruhusa ya Baraza la Mawaziri.

Alisema katika kampuni kuna asilimia 16 na asilimia hiyo ipo katika kila mgodi unaohusika na Barrick nchini na wawekezaji hao wamekubali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi