loader
Picha

Mrema- Huyu Waziri awekeze kwa watu

MAWAZIRI wanaoteuliwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wamepewa siri ya namna ya kuongoza wizara hiyo, bila kuendelea kumtesa Rais Dk John Magufuli kubadilisha mawaziri mara kwa mara.

Siri hiyo imetolewa jijini Dar es Salaan na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, aliyewahi pia kuwa Naibu Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Pili, Augustino Mrema alipozungumza na gazeti hili.

“Mawaziri wanaoteuliwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hawana budi kutambua kwamba wizara hiyo ni nyeti inayohitaji ubunifu, kuwekeza kwa watu na isiyohitaji kukaa ofisini pekee “alisema.

Mrema aliyeongoza wizara hiyo tangu mwaka 1990 hadi 1994 chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya kubadilishwa kwenda Wizara ya Kazi na baadaye kujiuzulu, amesema akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, ameshuhudia baadhi ya mambo yakienda isivyo na kuthibitisha kuwa wizara hiyo inasumbua.

Alisema hayo alipoulizwa maoni yake, kuhusu utendaji wa mawaziri katika wizara hiyo na matarajio yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mpya, George Simbachawene aliyeteuliwa hivi karibuni, kumrithi Kangi Lugola, aliyetenguliwa wadhifa huo mwishoni mwa wiki.

Rais Magufuli alitengua nafasi ya Lugola, kwa kuhusishwa kwenye kashfa ya kuingia mkataba tata, ulioandaliwa na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye.

Akizindua nyumba mpya za askari Magereza, Ukonga, Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema, kati ya wizara zinazomtesa ni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kutokana na madudu yanayofanyika huko na kueleza kisa cha mkataba huo tata, uliosainiwa Italia wa Euro 4000 sawa na Sh.trilioni 1.5 za Tanzania. Rais Magufuli alisema alitegemea watendaji wa serikali, watakuwa wanajifunza kuhusu matumizi mazuri ya mali za umma, lakini alichobaini watu wanakosa uadilifu.

Alisema pamoja na kuwapenda, Waziri Lugola na Kamishna Jenerali Andengenye, hawana budi kuondolewa madarakani, kulikotangazwa rasmi baadaye.

Amfunda Simbachawene

Akizungumza na gazeti hili jana kwenye mahojiano maalumu, Mrema alisema anachokiona katika utendaji wa viongozi wa sasa serikalini ni tabia ya baadhi ya viongozi, kutoguswa na shida za watu, jambo ambalo amesisitiza waziri mpya, afanye kwenye mambo yanayogusa wananchi, kama anavyofanya Rais Magufuli.

“Hata huyu anayekuja ajue na yeye tunamwangalia, taifa linamwona… aangalie mambo yanayogusa wananchi. Mfano nikiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole yapo mambo mengi ambayo nimeyaona na kuyaainisha, lakini yanakosa watekelezaji,” alisema.

Aliwahi kulalamika kwa Rais Magufuli kuhusu hilo. Mrema alisema wizara hiyo ni nyeti na mama wa wizara zote, ambapo uhalifu wowote unaofanyika nchini waziri mwenye dhamana, anapaswa kuufuatilia na waziri anatakiwa kutoa ufumbuzi. Kwamba waziri anatakiwa kuwa mbunifu, kama alivyokuwa akifanya wakati wa uongozi wake hadi watu wakamshutumu anaingilia wizara nyingine.

Alimtaka Simbachawene kuwekeza kwa watu, kwa kusikiliza shida zao, akijua si kila kitu kimeandikwa, bali yapo mambo ya kutumia ubunifu na akili ya kuzaliwa, akifuata nyayo za Rais kuleta maendeleo ya watu.

Alisema kinachowatoa mawaziri wengi ni ubabe, kutojali, kutosikiliza shida za watu na kukosa ubunifu. Alisema viongozi wakiwekeza kwa watu, watamjengea Rais sifa naye atawapenda na hatawaondoa haraka.

Alitoa mfano alipoteuliwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole mwaka 2017, alitembelea Gereza Kuu la Isanga, Dodoma, ambako alibaini baadhi ya wafungwa, wanatumikia vifungo vya miezi sita, kwa kukosa faini ya Sh 50,000.

Alisema alienda kwa majaji, kuwauliza endapo watu hao wakilipa faini wangeweza kuachiwa huru, akajibiwa kuwa inawezekana. Mwenyekiti wa huyo wa Chama cha TLP alisema alimfuata Askofu wa Kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni B, Getrude Rwakatare aliyetoa Sh milioni 10 kuwalipia faini hizo.

“Nilienda kuwalipia wafungwa 42 na risiti ninazo, lakini Magereza hawakuwatoa. Risiti zilipokewa na Mahakama Dodoma lakini wafungwa hao waliendelea kushikiliwa Magereza hadi muda wao ukaisha.

“Ndipo niliona kweli Rais Magufuli ana kazi na watu hawa (Wizara na Magereza). Watendaji wake wanaona Rais Magufuli anahangaika usiku na mchana akitaka msongamano wa wafungwa ukome. Unajiuliza, waziri kazi yake ni nini au huyo anayeangalia magereza kazi yake ni nini? Watu ni wababe na jeuri, hakuna anayekusikiliza. Katika mazingira kama hayo utaachaje kufukuzwa?,” amehoji Mrema.

“Malalamiko ya Rais ni ya kweli. Wanamtesa, hawamwelewi ndio maana huwa hawachukui maamuzi magumu. Wanampa mzigo na kazi ya kufukuza mara kwa mara, ionekane kazi ya Rais ni kufukuza,” alisema.

Mbali ya kashfa iliyomwondoa Lugola, Rais Magufuli alimsema pia Kamishna Jenerali wa Magereza, Faustine Kasike amekuwa hamwelewi Rais na alishindwa kusimamia utendaji, licha ya kumweleza mara tatu abadilishe utendaji wa jeshi hilo uakisi kazi nzuri ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lililojenga nyumba zao.

Alihoji vipi Magereza hadi siku hiyo, walikuwa hawajaingiza maji kwenye majengo waliyojengewa na JKT, licha ya JKT kuvuta maji hadi eneo la ujenzi na wanashindwaje kujifunza kwa JKT mbinu zinazowasaidia.

Kasike alitangazwa kuondolewa, lakini baadaye alipangiwa kazi kama Balozi na atapangiwa kituo baadaye.

Kasoro katika wizara

Akiainisha kasoro za wizara, Mrema alisema Bodi ya Parole anayoiongoza, katika kipindi cha kwanza (miaka mitatu), ilifanya vikao vinane badala ya 12, baada ya Waziri kuchelewa kuteua wajumbe wawili.

“Baada ya Rais kuniteua mwaka 2017, ili bodi ikutane kuna wajumbe wawili wanatakiwa wateuliwe na waziri lakini hakuwateua, akachukua miezi sita. Nimekaa kijiweni miezi sita bila ile bodi kukutana. Sasa waziri unashindwa kuteua wajumbe wawili hadi miezi sita. Huo si uzembe. Simbachawene asifanye haya”

Mrema aliyeongezewa muda na Rais Magufuli hivi karibuni kuongoza bodi hiyo, alisema Machi 2019, bodi iliridhia wafungwa 400 watoke, ambapo waziri alitakiwa asaini, lakini hakusaini hadi miezi mitatu.

Siri ya mafanikio

Akieleza siri ya kuongoza wizara hiyo hiyo kwa miaka minne akiwa ameacha rekodi ya kukamata dhahabu kilo tisa uwanja wa ndege, Mrema alisema alikuwa mbunifu na mikakati yake ililenga moja kwa moja kuhudumia wananchi.

Alitoa mfano alivyoanzisha ulinzi wa jadi (sungusungu), baada ya kuona idadi ya polisi ni ndogo. Mrema pia aliacha rekodi ya kujenga vituo vingi vidogo vya polisi maeneo ya mitaani mijini na vijijini.

Pia, aliruhusu polisi waliokamata rushwa, wapewe fedha na wanaokamata mali za magendo wapate asilimia ya thamani ya mali husika.

Alikomesha ujambazi katika maeneo mengi nchini na alitoa fursa majambazi wanaorudisha silaha kusamehewa.

“Nilienda kwa Rais (Ali Hassan Mwinyi) nikamwambia kwamba kwa nini mtu akirudisha silaha asisamehewe? Rais alikubali. Kuna vitu vingi tulivifanya kama motisha kuhamasisha umma,” alisema.

Mrema ni kati ya mawaziri 26 walioongoza wizara hiyo tangu nchi ipate uhuru hadi sasa. Ni mmoja wa mawaziri watano, waliodumu katika wizara hiyo kati ya miaka minne na sita.

Mawaziri wengine walioongoza kwa muda mrefu kidogo wa zaidi ya miaka minne ni Saidi Maswanya (1967-1973) na Muhidin Kimario (1983-1988), walioongoza kwa miaka sita.

Wengine walidumu chini ya miaka mitatu. Baada ya Mrema kuongoza wizara hiyo kwa miaka minne, aliyemfuatia ambaye ni Ernest Nyanda, hakumaliza mwaka, kwani aliingia mwaka huo na kuondoka mwaka huo.

Katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, wizara hii imeongozwa na mawaziri watatu, ambao ni Charles Kitwanga (2015-2016), Dk Mwigulu Nchemba (2016-2018), Lugola (2018-2020) na sasa wanne, Simbachawene.

Mawaziri wengine waliowahi kuongoza wizara Tangu nchi ilipopata Uhuru mwaka 1961, mawaziri wengine waliowahi kuongoza wizara hiyo nyeti na ngumu ya Mambo ya Ndani ni: Sir George Kahama 1961-1962, Oscar Kambona 1962-63, Lawi Sijaona 1963-65, Job Lusinde 1965-67, Omari Muhaji 1973-74, Mzee Ali Hassan Mwinyi 1975-76, Hassan Nassoro Moyo 1977- 78, Salmin Omary 1979-80, Abdallah Natepe 1980-83, Nalaila Kiula 1988-90, Ali Ameir Mohamed 1994-99, Mohamed Khatib 2000-2002, Omari Ramadhan Mapuri 2003-05, Kapteni mstaafu John Chiligati 2006-08, Lawrence Masha 2008-2010, Shamsi Vuai Nahodha 2010- 12, Dk Emmanuel Nchimbi 2012-13 na Mathias Chikawe 2014-15.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi