loader
Picha

Wachumi: Tanzania sio mbabe kwa wawekezaji

KUUNDWA kwa Kampuni ya Twiga Minerals kumeidhihirishia dunia kuwa Tanzania sio mbabe, wala haifukuzi wawekezaji, bali inasimamia haki za rasilimali za wananchi wake.

Vilevile, hatua hiyo imefungua ukurasa mpya wa kutekeleza Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Umiliki wa Rasilimali (1962), unaotaka rasilimali za nchi yoyote, ziwafaidishe kwanza wananchi wake.

Hayo yalibainishwa katika mahojiano kati ya HabariLeo na wataalamu wa masuala ya uchumi Dar es Salaam jana, kuhusu matokeo ya Kamati mbili zilizoundwa na Rais Dk John Magufuli mwaka 2017 kwa ajili ya kufuatilia na kuchunguza mwenendo mzima wa biashara ya madini nchini.

Rais Magufuli alifikia hatua hiyo, baada ya kutoridhishwa na ugawanaji wa rasilimali hiyo muhimu kati ya Kampuni ya Barrick Gold Mining na Serikali, hivyo kuonekana wananchi wa Tanzania hawanufaiki na tija wala maslahi halisi.

Makubaliano yaliyofikiwa ilikuwa ni safari ndefu, nzito na yenye ushindani na mivutano, hasa ikizingatiwa kuwa Kampuni ya Kampuni ya Barrick Gold Mining, imesheheni watendaji na wajumbe wa bodi wenye utaalam, uzoefu, weledi na heshima kubwa duniani, wakiwemo mawaziri wakuu wastaafu wa nchi kubwa duniani.

Bodi ya Ushauri ya Kimataifa ya Kampuni ya Barrick inaundwa na watu wanne, ambao ni Mwenyekiti, Brian Mulroney ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Canada mwaka 1984-1993.

Wajumbe wa bodi ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa Hispania, Jose Maria Aznar. Alikuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo mwaka 1996-2004. Wengine ni aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada mwaka 2011-2015, John Baird na Gustavo Cisneros, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni za Cisneros.

Kwa upande wake, Kampuni ya Barrick Gold Mining inaongozwa na Mwenyekiti Mtendaji, Profesa John Thornton, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa juu kampuni hiyo, walioonesha utayari wa kuafiki mapendekezo ya Serikali ya Tanzania, kuhusu uendeshaji mpya wa biashara ya dhahabu nchini.

Kiongozi mwingine aliyehusika kwenye kufanikisha makubaliano hayo na kusainiwa kwa mikataba hiyo tisa ni Rais wa Kampuni hiyo kubwa, Dk Mark Bristow.

Akifafanua, Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Abel Kinyondo alisema mapendekezo ya kamati hizo mbili, ndiyo yaliyozaa matunda siku chache zilizopita, baada ya Tanzania na kampuni ya Barrick Gold Mining, kusaini mikataba tisa ya makubaliano ya kufanya biashara hiyo yenye maslahi kwa pande zote.

Dk Kinyondo alisema: “Kutiwa saini hapa nchini kwa makubaliano hayo ya kuanza biashara kwa mwelekeo mpya wa usawa tena kwa kuja kwa Rais wa Kampuni ya Barrick nchini na kuzungumza hadharani walivyoafiki kufanya biashara hiyo, kumeipa dunia ujumbe kwamba Tanzania sio mbabe, wala hainyanyasi wawekezaji, kama baadhi ya watu wanavyoichafua, bali imeonesha msimamo wa nchi kupigania haki yake na kutekeleza Mkataba wa UN kuhusu Umiliki wa Rasilimali za Nchi”.

Katika makubaliano hayo, ambayo Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick wameingia siku chache zilizopita, kwa kusaini mikataba tisa ya kuendesha na kufanya biashara ya madini hayo, baadhi ya makubaliano ni kugawana faida ya asilimia 50 kwa 50, sambamba na Tanzania kuwa na hisa asilimia 16 zisizoshuka thamani.

Akizungumzia hatua hiyo, Dk Kinyondo alisema Tanzania imeidhihirishia dunia, kuwa haifanyi maamuzi, kwa kuwakomoa wawekezaji, bali inasimamia sheria na mikataba ya kimataifa, kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wake, kama ambavyo sheria za ndani na za kimataifa zinavyoelekeza.

“Kilichofanyikwa ni jambo la kihistoria, Rais Dk Magufuli amesimamia haki na amehakikisha Mkataba wa Kimataifa uliofikiwa mwaka 1962 na Umoja wa Mataifa kwenye Umiliki wa Rasilimali za Taifa, unatekelezwa na dunia imesikia na hii imefuta uvumi wa kwamba Tanzania inafanya mambo kibabe, sasa imedhihirisha ni nchi inayofuata misingi ya sheria, hivyo ni sehemu nzuri ya kuwekeza,”alisema.

Mkataba huo ulisainiwa Desemba 14, mwaka 1962 katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambapo mataifa 87 yalipiga kura ya ‘ndiyo’ dhidi ya mataifa mawili. Mkataba huo nataka rasilimali na mali zilizopo kwenye taifa lolote, zimilikiwe na wananchi wa taifa hilo kwanza.

Akizungumzia mafanikio hayo, Dk Kinyondo alisema mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na Sheria ya Madini ya mwaka 2010, yametoa mwanga mpya kwenye sekta ya madini, kwani kamati mbili zilizoundwa na Rais Magufuli, ziliwasilisha ripoti zao zilizoonesha udanganyifu na upotevu mkubwa wa fedha, uliokuwa ukifanywa kwenye biashara hiyo huku nchi na wananchi wake wakikosa faidia stahiki.

“Ukiangalia kwenye sekta ya madini kwa wakati huo kabla ya kuundwa kwa kamati zile mbili, utaona mchango wa sekta hizo kwenye pato la taifa ulikuwa asilimia tatu wakati sekta ya kilimo ilichangia karibu asilimia 30. Hii sio sawa,”alisisitiza.

Alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kuomba makubaliano hayo yafanikiwe. Aliomba serikali ianze mapema kujipanga kwa ajili ya baadaye, kwani biashara hiyo ikianza vizuri, itakuwa na matokeo chanya, ambayo yatahitaji nguvu kazi kubwa zaidi.

“Tumeanza vizuri, ushauri wangu sasa ni kwa serikali kujipanga, tuangalie tunatumiaje hiyo asilimia 16 ya hisa zetu? Tusibweteke nazo, tuje na mipango ya baadaye, kama ni kuongeza tuige wenzetu wa Bostwana, wao walianza kwenye almasi kwa hisa ya asilimia 25 kwa 75 mwaka 1975, leo wako hisa asilimia 50 kwa 50,”alisema.

Alishauri ni vyema kuwa na mipango mizuri ya baadaye, ya jinsi ya kujiimarisha na kuangalia uwezo wa kuongeza hisa na nguvu kazi. Pia kuangalia sasa jinsi ya kuwatumia wataalamu wa ndani na kuwaongezea ujuzi, kwa kupitia nchi zilizofanya vizuri kwenye sekta hiyo.

Hata hivyo, aliwataka Watanzania kuacha kupumbazwa na baadhi ya wanasiasa na watu wanaoichafua nchi kwenye mitandao yao ya kijamii, kwa kuzungumza mambo ya kitaaluma kisiasa, bali wahakikishe wanapotaka kupata ukweli wa mambo, wafuate tovuti rasmi zenye taarifa sahihi.

Dk Kinyondo alishauri serikali isiwe kimya kuwaeleza wananchi ukweli au usahihi wa jambo linapotokea, kwa sababu ikikaa kimya, inatoa mwanya kwa wasiopenda maendeleo ya nchi, kuandika taarifa zisizo sahihi na wananchi kuziamini, kwa vile hakuna taarifa iliyotolewa na serikali juu ya jambo husika.

Aidha, Dk Kinyondo alisema wapo watu wanaodai hisa asilimia 16 ni ndogo, hivyo huenda uundwaji wa menejimenti ya Twiga ukawa umetoa nafasi chache kwa watanzania dhidi ya kampuni ya Barrick. Alifafanua kuwa jambo hizo sio kweli, kwani sheria za kimataifa na zile za ndani, husimamia jambo hilo.

“Unajua unaposema asilimia 16 ya hisa za Tanzania ni ndogo dhidi ya asilimia 84 ya hisa za Barrick, kwenye uundwaji wa menejimenti mambo mengi huangalia. Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na Sheria ya Madini ya mwaka 2017, kuna suala linaitwa ‘Local Content’. Hiyo Local Content ni lazima izingatiwe kwenye uundwaji wa menejimenti hiyo” alisema.

Alisema “Sheria zipo na tutapata uwakilishi nzuri tu na wa idadi nzuri, tuombe watakaochaguliwa wawe wazalendo, watuwakilishe vyema ili nchi na wananchi tufaidike na madini haya”.

Kwa upande wake, Profesa Razack Lokina ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi kutoka UDSM, alisema kuwa sekta ya madini imesimamiwa vizuri kwa sasa na Rais Dk Magufuli na dunia imetambua hilo.

“Tumeona sekta ya madini imesimama sasa vizuri, Rais ameitendea haki amesimamia masoko ya madini na yamefunguliwa kila mkoa na hii kwenye masuala ya uchumi itapandisha sana pato la taifa (GDP),”alisema.

Alisema kwa sasa wananchi hawawezi kuona matokeo yake, kwa vile sio jambo linalotoa tafsiri ya haraka ya kuwajaza fedha mfukoni. Lakini, miaka michache ijayo matokeo yake yataonekana na thamani ya shilingi itaongezeka, kama madini hayo yatauza zaidi nje.

“Ni mwanzo mzuri, tuna kila sababu ya kupongeza na pia wataalamu wetu wameonesha uwezo wao mkubwa wa kubaini upungufu kwenye sekta ya madini na kutoa mapendekezo yaliyozaa matunda haya leo, sasa tujenge tabia ya kuwatumia wataalamu wa ndani wenye uwezo kama hao, kwa sababu maendeleo ya nchi huleta na wananchi wenyewe”,alisema Profesa Lokina.

Itakumbukwa kwamba Machi 29, mwaka 2017 Rais Magufuli aliteua Kamati maalumu ya wajumbe wanane ikiongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma, kuchunguza aina na viwango vya madini yaliyomo kwenye mchanga wa madini uliomo ndani ya makontena, yaliyozuiliwa na serikali kusafirishwa nje ya nchi.

Wajumbe wa kamati hiyo ni wataalam katika fani za jiolojia, kemia, uhandisi kemikali na uhandisi uchenjuaji madini. Chimbuko la kufanyika kwa uchunguzi huo ni kutokana na ukweli kuwa viwango vya madini yaliyopo kwenye makinikia havijulikani na hata mikataba ya uchenjuaji makinikia haipo wazi.

Hali hiyo inaleta hisia kuwa nchi inaibiwa na hainufaiki na uchimbaji wa madini. Katika matokeo ya uchunguzi huo, kamati ilibaini kuwepo kwa viwango vingi vya juu vya dhahabu, shaba, silva, sulfa, chuma, iridium, rhodium, ytterbium, beryllium, tantalum nalithium ndani ya makinikia yaliyofanyiwa uchunguzi. Kwa mujibu wa utafiti huo, jumla ya thamani ya aina zote za metali katika makontena 277 yaliyokuwapo bandarini ni kati ya Sh bilioni 129.5 na bilioni 261.5.

Pamoja na kuwa na thamani kubwa, metali hizo hazikuwa zinajulikana kuwemo kwenye makinikia na hivyo hazijawahi kujumuishwa kwenye kukokotoa mrabaha, hivyo kuikosesha serikali mapato makubwa kwa kipindi chote cha biashara ya makinikia.

Kwa ujumla thamani ya metali/madini yote katika makinikia kwenye makontena 277 yaliyozuiliwa bandarini, ni Sh bilioni 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani na Sh bilioni 1,438.8 kwa kutumia viwango vya juu.

Kamati pia ilichunguza uwezo wa skana inayotumika bandarini, kukagua vilivyomo ndani ya makontena. Katika uchunguzi huo, ilibainika kuwa skana hiyo haina uwezo wa kuonesha vitu vilivyomo ndani ya makinikia, bali inaonesha umbo tu la shehena ya makinikia.

Kutokana na matokeo hayo, kamati hiyo ilitoa mapendekezo kadhaa ikiwemo serikali kuendelea kusitisha usafirishaji wa makinikia, hadi pale mrabaha stahidi utakapolipwa serikalini, kwa kuzingatia thamani halisi ya makinikia na serikali ihakikishe ujenzi wa ‘smelters’ nchini, unafanyika haraka ili makinikia yote yachenjuliwe nchini.

Katika uchunguzi huo, kamati hiyo ilifanya kazi na taasisi mbalimbali ambazo ni vyombo vya ulinzi na usalama nchini, Wakala wa Jiolojia Tanzania, Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania, UDSM na Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro.

Aidha, Rais Magufuli Aprili 10, mwaka 2017 aliunda kamati ya pili iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Profesa Nehemia Osoro kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusu mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi, yakiwemo makontena 277 yaliyozuiliwa na Serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kamati hiyo ilifanya tathmini ya mchakato mzima wa usafirishaji wa makinikia, kwa kupitia mikataba husika na kushauri endapo inazingatia kikamilifu maslahi ya nchi ama inahitaji kuboreshwa, kufanya tathmini ya mfumo mzima wa udhibiti kuhusu biashara ya makinikia na kubaini idadi ya makontena yenye makinikia, yaliyosafirishwa kutoka katika migodi ya dhahabu kuanzia mwaka 1998 hadi sasa.

Kutokana na uchunguzi wake, ilibaini kuwa kuna ukiukwaji wa sheria za nchi na upotevu mkubwa wa mapato ya serikali kupitia biashara ya makinikia na madini yanayosafirishwa nje ya nchi.

Hivyo, kamati hiyo ilipendekeza serikali kupitia Msajili wa Makampuni, ichukue hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya Acacia Mining Plc, ambayo imekuwa inaendesha shughuli zake nchini kinyume na matakwa ya sheria.

Pia ilipendekeza serikali idai kodi na mrabaha kutoka kwa kampuni zote za madini, ambazo zimekwepa kulipa kodi na mrahaba stahiki kwa mujibu wa sheria na serikali iendelee kuzuia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi mpaka hapo makampuni ya madini yanayodaiwa, yatakapolipa kodi, mrahaba na tozo stahiki kwa mujibu wa sheria.

Pia ilishauri serikali kupitia Kamishna wa Madini, iwe inafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kampuni ya madini ili kujihakikishia uzingatiaji au ukiukwaji wa sheria na taratibu za uendeshaji na kuchukua hatua ipasavyo.

Ni kupitia mapendekezo hayo, timu ya majadiliano iliundwa, ikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria kwa wakati huo, Profesa Palamagamba Kabudi na timu ya kampuni ya Barrick, ambao walifanya majadiliano ya muda mrefu, yaliyopitia nyakati ngumu, lakini yakahitimishwa Oktoba 19, mwaka 2017.

Hitimisho ya makubaliano hayo ni kwa Rais Magufuli kutia saini makubaliano hayo, yaliyofikia tamati na kuja na makubaliano ya mwelekeo mpya wa kufanya biashara ya madini nchini Tanzania.

Katika kuonesha nia na kuridhia makubaliano hayo, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Barrick Gold, Profesa John Thornton na timu yake sambamba na timu ya serikali ya Tanzania, walikuwepo siku ya utiliwaji saini makubaliano hayo, ambayo leo yamefungua ukurasa mpya wa kufanya biashara ya madini ya dhahabu, kwa kugawana nusu kwa nusu ya faida itakayopatikana.

Jambo jingine ambalo Tanzania inajivunia ni kutekelezwa kwa makubaliano ya mkataba huo wa kuundwa kwa kampuni ya ubia wa usimamizi wa migodi ya madini, ambapo kampuni ya Twiga Minerals imeshafunguliwa na itakuwa na makao makuu yake Mwanza na ofisi ndogo Dar es Salaam, badala ya nchini Uingereza.

Aidha, Barrick Gold imekubali kuwepo kwa wawakilishi wa serikali katika bodi za migodi yake yote hapa nchini, kazi mbalimbali za kwenye migodi kufanywa na kampuni za Tanzania, migodi kutoa ajira za kudumu kwa wachimbaji, wachimbaji hao kuishi majumbani kwao badala ya kuishi kwenye makambi ya migodi na mashauri yote ya kesi mbalimbali kufanywa hapa nchini.

Mapema baada ya kutia saini makubaliano hayo, Profesa Thornton alimpongeza Rais Magufuli kwa msimamo wake, unaojenga misingi ya biashara ya kuaminiana na uwazi, ambayo ni muhimu na ya namna yake kwa biashara katika karne hii ya 21.

Kauli hiyo pia ilitolewa na Rais wa kampuni ya Barrick, Dk Mark Bristow Ikulu jijini Dar es Salaam siku chache zilizopita, mbele ya Rais Magufuli wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya makubaliano ya kuendesha kwa pamoja kampuni ya Twiga Minerals ya uchimbaji wa madini kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hiyo.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick na Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi