loader
Picha

Bashe aonya kuingiza siasa ununuzi wa pamba

WAKATI takribani asilimia 20 ya pamba ambayo imelimwa msimu uliopita bado haijanunuliwa hadi sasa, serikali imeonya kuingizwa siasa katika zao hilo.

Pia serikali imetaka mikoa inayolima zao hilo kujipanga vyema kwa msimu huu kwa kuwa kilimo hicho ni cha biashara.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akizungumza na wakuu wa mikoa inayolima zao la pamba nchini.

Wakuu hao wamekutana mjini hapa kupokea na kujadili taarifa ya kamati ndogo kuhusu changamoto zinazokabili kilimo cha pamba na kutoa mapendekezo ya utatuzi wake. Kamati hiyo ndogo ya wadau iliundwa Oktoba mwaka jana jijini Mwanza kwa lengo la kuja na mapendekezo ya utatuzi wa changamoto za zao hilo hapa nchini.

Akifungua kikao hicho mjiniDodoma, alisema kikao hicho ni muhimu ili kutengeneza mustakabali mzuri wa tasnia ya pamba kwenye mikoa 17 inayolima zao hilo.

Bashe alisema msimu ujao wa kilimo cha pamba unapaswa uwe mzuri na usiwe na matatizo. “Pamba na kilimo ni biashara tusipeleke siasa. Msimu huu ulikuwa mgumu. Tumekubaliana serikalini kuwa biashara hii ifanywe kwa uwazi zaidi ili mkulima apate manufaa ya jasho lake,” alisema.

Naibu Waziri Bashe alisema Wizara ya Kilimo imetengeneza mkakati wa miaka mitano kuhusu sekta ndogo ya pamba ili kukidhi mahitaji ya soko na upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima nchini. Bashe aliongeza kusema tayari wizara imefanya majadiliano na wizara za Viwanda na Biashara na ya Fedha na Mipango juu ya mustakabali wa zao hili msimu ujao.

“Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025-2020 imeelekeza ushirika kusimamia sekta ya pamba kwa manufaa ya wakulima nchini, hivyo lazima tutafute suluhu ya changamoto za masoko “ alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara na Mwenyekiti wa kamati ndogo ya wadau wa pamba, Adam Malima alisema ni wakati sasa Wizara ya Kilimo ikaweka mikakati mahususi ya upatikanaji wa bei nzuri ya pamba ya wakulima kupitia mfumo wa ushirika.

“Ushirika nchini lazima uwe na takwimu sahihi za wakulima, kiasi cha pembejeo kinachotakiwa na eneo linalolimwa ili kuepusha hasara kwa wakulima kubebeshwa madeni yasiyowahusu,” alisema.

Malima amebainisha kuwa suala la utafiti na ugani kwenye zao la pamba ni muhimu lipewe kipaumbele, lakini Wizara ya Kilimo haioneshi jitihada. Alisema Wizara ya Kilimo inatakiwa pia kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo za pamba kwa wakati na zenye ubora kuhakikisha zinawafikia kwa wakati na bei nafuu.

Kikao hiki maalumu cha wadau kinahudhuriwa na Wakuu wa Mikoa ya Mara, Simiyu, Morogoro, Kagera, Kigoma,Singida, Mwanza, Geita, Shinyanga, Kilimanjaro na Katavi

SHULE ya Msingi Kawe B, Dar es Salaam imeahidi kufanya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Dodoma

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi