loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Magufuli- Hii Wizara ina mapepo

RAIS Dk John Magufuli amemkabidhi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene mafaili ya mkataba uliomuingiza matatani aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Kangi Lugola, huku akimtaka aifanyekazi hiyo kwanza pindi tu atakapoingia ofi sini.

Pia amemtahadharisha waziri huyo juu ya ugumu na maskendo ya wizara hiyo na kumuagiza kufagia watendaji wote wasiofaa na wale wanaostahili kushushwa vyeo pindi watakapoenda kinyume.

Dk Magufuli aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akiwaapisha mawaziri wawili akiwemo Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mussa Azzan Zungu, balozi wa Uswizi Maimuna Tarishi, Balozi wa Japan Hussein Katanga na balozi wa Umoja wa Mataifa Marekani Kennedy Gaston.

“Hii ni wizara ngumu na ukweli imehusika kwenye maskendo mengi, sifahamu kuna mdudu gani pale, nimekupeleka wewe pale nenda kayasimamie,” alisema Dk Magufuli.

Alimkabidhi Waziri huyo mafaili yanayohusika na mkataba mbovu uliosainiwa na kuiingizia nchi hasara na kumtaka pindi atakapowasili ofisini yake mpya aanze kuyafanyia kazi.

“Hili suala la MOU kalisimamie, nakupa mafaili haya ukayasimamie, ukalale nayo mbele, huko nenda kaanze nalo hili. Nakutahadharisha watendaji wako si kwamba hawalijui, Naibu Waziri anajua ingawa hakujihusisha sana,” alisisitiza.

Alisema anafahamu kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni pamoja na kwamba hakushiriki kwenye skendo hiyo, lakini suala hilo alilifahamu kwani alipitishiwa dokezo lake ingawa hakuliwasilisha kwake wakati alitakiwa aliwasilishe.

“Alipewa madokezo alitakiwa aje aseme lakini alikaa kimya sifahamu kwa nini alikaa kimya. Naibu Katibu Mkuu alihusika sana, tangu kuanza kwake mpaka mwisho, na watendaji wengine kwenye zimamoto wamehusishwa wengine walilipwa dola za Marekani 500, na dola za Marekani 300 za safari, pamoja na laptop…,” “…Unajiuliza kwa lugha ya kawaida, umeingia kwenye mazungumzo kwanini huyo mnayejadiliana naye akupe dola 800 au laptop? Kwa akili za kawaida, mtu unaweza ukaelewa hapa kuna kitu cha ajabu kinafanyika,” alisema.

Hata hivyo, alieleza kuwa watendaji hao hawakuliona hilo mpaka ukasainiwa mkataba wakapelekwa nje wakalipiwa, wakaenda kununua drones.

“Sasa zijui drones inazima moto? huko nje mashamba ya wenzetu yanaungua hawatumii drones kuzimia moto,”

“Hii MOU ya kulipa shilingi trilioni 1.2 is for nothing no way, hii ndio inatufanya Tanzania tunalipa madola mengi ya kwenye makesi kwa mambo ya ajabu,” alisema.

Dk Magufuli alisema mikataba kama hiyo ndio inayoliingizia taifa hasara na kuwasababishia watanzania umasikini kutokana na maslahi ya watu binafsi huku ikiwa haina tija.

“MOU hii haikuletwa kwenye baraza la mawaziri, naletewa barua eti nipitishe tu sasa nipitishe kitu gani sielewi,”

Alimfahamisha Waziri Simbachawene kuwa anaenda kwenye wizara yenye mapepo huku akimtahadharisha kuhakikisha mapepo hayo hayamuingii.

Alimtaka awe mkali na kusimamia shughuli za wizara kwani anamuamini endapo atamtanguliza Mungu.

“Yale utakayoweza kuyabadilisha badilisha, watendaji wasiofaa watoe, wanaohitaji kushushwa vyeo shusha, ili kusudi mambo pale yaende vizuri,” alisisitiza.

Aidha, alimtaka Waziri huyo kuvisimamia vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufuata taratibu za wizara hiyo.

“Simbachaene ulizungumza vizuri kuwa huna nyota hapa, umesema vizuri hivi vyombo vya ulinzi vina namna yake ya kuvisimamia, ndio maana Mwinyi (Waziri wa Ulinzi Hussein Mwinyi) yupo pale kwa miaka mingi. Huwezi ukaanza kuwatukana wakuu wa ulinzi. Ndio maana wakuu wa ulinzi wana mandate ya kuripoti kwangu moja kwa moja…,”

“Wewe ni mwanasheria umezungumza hapa nimemuona IGP (Simon Sirro) akitingisha kichwa kukubaliana na unayosema, alishanilalamikia kuwa ameambiwa awatoe watu ilibidi nimuambie awatoe tu ingawa si utaratibu,” alisema.

Aliwataka watendaji serikalini wasiiingie kwenye mikataba ikiwemo inayohusisha mikopo bila kushirikisha wizara inayohusika na kukopa fedha huku akitolea mfano mkataba huo wa MOU ambao ulizungumzia hadi namna ya kukopa fedha kwenye benki za nje huku wakiwa hawajui riba itakuaje.

Wiki iliyopita Rais Magufuli alimvua nafasi ya uwaziri Lugola na Kamishna Jenerali wa Zimamoto, Thobias Andengenye kwa tuhuma za kushiriki kuandaa mkataba ambao Rais huyo aliuita wa hovyo na usio na tija kwa taifa Hata hivyo, Rais Magufuli alimpongeza aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu kwa kujiuzulu mapema kabla sakata hilo halijawekwa wazi na siku moja baadaye alimteua kuwa balozi.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi