loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Abbasi- Mkataba na Barrick una manufaa makubwa

MKURUGENZI Mkuu Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbasi amesema mkataba wa madini wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold, ni mkataba bora na wenye manufaa makubwa kwa Tanzania.

Dk Abbasi amesema hayo jana jijini Dodoma kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati akijibu maswali. Akifafanua, Dk Abbasi amesema mkataba huo una mikataba tisa ya madini, iliyosainiwa na Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold kwa mfumo wa 50-kwa 50 hivi karibuni.

Amesema mkataba huo ni bora na una manufaa makubwa kwa Tanzania, ikilinganisha na ule wa awali. Alisisitiza kuwa mkataba huo utainua sekta ya madini na kuongeza mapato kwa kiasi kikubwa.

Amesema katika mkataba wa sasa, umiliki wa mgodi utakuwa sawa kati ya serikali na Kampuni ya Barrick, ikiwa ni tofauti na mkataba wa awali, ambao mmiliki wa mgodi kwa asilimia 100 alikuwa ni mwekezaji. Alisema pia mkataba wa sasa, umerejesha kodi zote na zinatakiwa kulipwa, ambapo awali zilikuwa zimefutwa.

“Tunazozungumzia suala la asilimia 50 kwa 50 ina maana katika maeneo yote kutakuwa na usawa katika uendeshaji, ajira, menejimeni na bodi na kuna maeneo ambayo serikali itanufaika kwa asilimia 100.

“Na ndio maana katika makubaliano haya mapya, wameingia mkataba na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya mafunzo kwa vijana wa Tanzania, ambako kiasi cha dola milioni moja ambazo ni sawa na shilingi bilioni mbili zitatengwa kila mwaka kwa ajili ya mafunzo hayo” alisema Dk Abbasi.

Amesema pia kupitia makubaliano hayo, kutafanyika ujenzi wa mitambo mikubwa ya kuchakata madini hapa nchini, hivyo kuondoa suala kupeleka makinikia nje ya nchi.

“Tunashukuru kwasababu Tanzania ilipeleka wabobezi na wazalendo katika makubaliano hayo. Jambo la msingi ni kuwa katika muundo wa 50 kwa 50 hatuishii kwenye kodi na gawio pekee, bali Tanzania inanufaika katika uendeshaji, usimamizi mpaka huduma za kijamii.

“Hata unapoona serikali imeruhusu makinikia, ina maana kile kilichomo si cha mwekezaji peke yake, ni cha serikali na mwekezaji. Hivyo kutokana na mfumo huu mwisho wa siku Tanzania isipate chini ya asilimia 50 ya manufaa katika kila eneo,” alisema.

Dk Abbasi alieleza kuwa katika majadiliano na kampuni hiyo ya Barrick, Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na wasomi wabobezi na watanzania wazalendo, ambao walifanya kazi hiyo kwa nguvu zao, uwezo wao na akili zao zote kwa maslahi ya taifa.

Mkopo wa Benki ya Dunia

Dk Abbasi alisema hoja ya baadhi ya watu kuwa serikali itatumia mkopo kutoka Benki ya Dunia kwenye uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu, haina mashiko.

Alisema serikali inakopa fedha hizo, kwa sababu ina uwezo wa kulipa na kuwa mkopo huo ni kwa manufaa ya watanzania.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani, zenye sheria nzuri ya uchaguzi na sheria ya gharama za uchaguzi, inaweka uwazi katika gharama za uchaguzi kwa kila chama.

Dk Abbasi alisema mpaka sasa Tanzania tayari imeshaanza mchakato wa uchaguzi mkuu, kwa kuanza na uboreshaji wa daftari za wapiga kura kwa kutumia fedha za ndani.

“Nchi inakopa kwa sababu ya kuwaletea maendeleo wananchi wake na pia ina uwezo wa kulipa. Lakini hii hoja kuwa fedha zinatumika kwenye uchaguzi halina hoja.

“Tanzania ina sheria nzuri na makini ya uchaguzi, ambayo ni sheria ya gharama za uchaguzi, ambapo kila chama kina kiwango ambacho kinapaswa kutumia kwa ngazi ya urais na ubunge na kubainisha vyanzo vya fedha,” alisema.

Dk Abbasi aliongeza: “vyama vyenye sifa vinapewa ruzuku, je fedha hizo ni za mkopo? Tume yaUchaguzi imeanza kuboresha daftari za wapiga kura, fedha hizo ni za mkopo?” Dk, Abbasi aliwashangaa wanasiasa ambao wamekuwa wakihoji serikali kukopa, ambao awali walikuwa wakihoji kwa nini serikali inalipa fedha taslimu kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Hawa hawa walikuwa wanasema kwa nini serikali inalipa cash (fedha taslimu) tulipokuwa tunanunua ndege au kutekeleza miradi mingine ya mendeleo,” alieleza.

Wiki hii Benki ya Dunia (WB) iliahirisha kikao cha kuikopesha Tanzania Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya sekta ya elimu nchini Inadaiwa WB ilichukua hatua hiyo, baada ya kupokea barua kutoka kwa baadhi ya wanaharakati na viongozi wa upinzani Tanzania, wakiongozwa na Zitto Kabwe, waliodai iahirishe kutoa mkopo kwa serikali ya Tanzania.

Wanahakati na wanasiasa hao, wanadai kuwa benki hiyo ikiipatia Tanzania mkopo huo ni kuwanyima haki watoto wa kike, ambao wamezuiwa kusoma wakiwa wajawazito kwenye shule za Tanzania. Wanaharakati na wanasiasa hao wanadai kuwa serikali ya Tanzania, imewanyima haki wanafunzi wajawazito kusoma, na badala yake inawahamasisha wanawake kuzaa kadri ya uwezo wao ili kuongeza idadi ya watu wa Tanzania.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi