loader
Picha

Wachumi, wanasiasa wampinga Zitto

WASOMI, wanadiplomasia na wachumi, wamepinga shinikizo la baadhi ya wanaharakati na viongozi wa vyama vya upinzani nchini la kuiandikia barua Benki ya Dunia (WB), kuiomba kuahirisha kuipatia Tanzania mkopo wa Dola za Marekani milioni 500.

Wametaka ifike mahali wanaharakati na wanasiasa, wakatambua mipaka yao na kwamba kama kuna tatizo kwenye suala hilo ni vyema njia za majadiliano kwa mujibu wa taratibu za kidiplomasia, zikafuatwa baina ya nchi na taasisi hiyo na halipaswi kushughulikiwa baina ya mtu binafsi au kikundi na taasisi.

Hata hivyo, hivi karibuni wanaharakati na baadhi ya viongozi wa upinzani nchini akiwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto, waliandika barua WB kushinikiza kutotoa fedha hizo kwa madai kuwa mfumo wa elimu unawanyima haki ya kusoma wanafunzi waliopata ujauzito.

Wakizungumza na HabariLEO jana kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Masomo wa Chuo cha Diplomasia (CFR), Profesa Kitojo Wetengere alisema jambo linaloendelea kufanywa na baadhi ya wanaharakati na viongozi wa vyama vya siasa ni kuchafua taswira ya nchi.

“Wahanarakati wanachafua taswira ya nchi, iwapo Benki ya Dunia itaamua kusitisha fedha hizo miradi ya maendeleo itakwama. Lakini pia wanaharakati hao wamevuka mipaka, zipo taratibu za kidiplomasia kuwasiliana baina ya nchi na taasisi kubwa kama hiyo ambazo zina makubaliano na sio ngazi ya mtu binafsi (individual) au kikundi,” alisema Profesa Wetengere.

Akielezea utaratibu huo wa mawasiliano baina ya nchi na taasisi kubwa kama hiyo, Profesa Wetengere alisema katika diplomasia mambo ya nchi na taasisi, yanazungumzwa kwa ngazi ya kitaasisi na sio mtu binafsi na kwamba hilo limewasilishwa isivyo halali.

“Kama wanaharakati hao waliona kuna mambo ya msingi yanapaswa kujadiliwa kwenye barua yao iliyopelekwa WB, walipaswa kufahamu kwamba zipo taratibu kwa kuanza kupeleka malalamiko yao hata bungeni au kuwasiliana na serikali kuona jinsi ya kujadili, ila sio kuvuka mipaka yao,” alisema Profesa Wetengere.

Aliongeza, “pia hao WB kama walipokea malalamiko hayo na kuona kuna mambo yanahitaji kurekebishwa au mazungumzo, walipaswa kuwasiliana na nchi husika kwa sababu wana utaratibu maalumu wa mawasiliano baina ya nchi na taasisi yenye mkataba na wao na sio kufanya uamuzi kutoka kwa madai ya mtu wa tatu (individuals).”

Aidha, alisema jambo hilo pia serikali inapaswa kuliangalia kwa umakini, kwani propaganda zipo na baadhi ya nchi zinazochangia au kutoa misaada, hutumia njia hiyo kupenyeza maslahi yao, kwa kuwatumia baadhi ya wanasiasa au hata wanaharakati.

Mhadhiri wa CFR, Deus Kibamba amesema anapinga hatua iliyofanywa na wanaharakati hao, kwani wamefanya mambo bila kufuata utaratibu. Kibamba alisema ziko njia za kushughulikia mambo kama hayo, yanayofanywa baina na nchi na taasisi kubwa kama hiyo. Kwamba watu binafsi hawawezi kutoa ushauri wa moja kwa moja kwenye taasisi hiyo, bila kufuata mtiririko mzima wa mawasiliano wa ndani ya nchi.

“Kwanza sio utaratibu, mtu wa tatu (third party) hawezi kupeleka malalamiko ya nchi kwenye taasisi kama hiyo. WB ni taasisi kubwa, imeingia mikataba na nchi hivyo kama kuna utata ni vyema taasisi hiyo ikashughulikia suala hilo na nchi husika na sio kusikiliza mtu binafsi,” alisema Kibamba.

Profesa wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Felister Mombo amesema wanasiasa wanapaswa kujitofautisha na joho la wanaharakati.

Profesa Mombo alisema majukumu ya siasa ni tofauti na wanaharakati na kwamba mwanasiasa ni mtu anayefanya mambo ili mradi apate kura kutoka kwa wapiga kura, bila kujali matokeo ya matamshi au jambo analozungumza.

“Wanasiasa wasifikiri kila kitu kinaendeshwa kisiasa ili mradi avute hisia za watu na wampe kura muda mwingine, wajue kuna kesho na waangalie matokeo ya matamshi yao katika uchumi, maendeleo ya nchi na watu wake lakini pia masuala ya usalama na amani,” alisisitiza Profesa Mombo.

Alisema suala la mimba kwa wanafunzi, serikali imeweka sheria na taratibu ambazo kila jamii au taifa, ina utaratibu wake katika kuhakikisha elimu na nidhamu vinakuwepo na hilo lisitumike vibaya, kuinyima nchi fedha za maendeleo kwenye sekta ya elimu.

Mtafiti na Mchumi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Profesa Samwel Wangwe alizungumzia sakata hilo na kusema haungi mkono hatua zilizofanywa na wanaharakati na wanasiasa hao, kwani hakukuwa na haja ya kufika huku.

“Siungi mkono hatua ya wanaharakati hao, sioni haja ya wao kufika huko. Kulikuwa bado kuna nafasi ya kufanya mazungumzo ndani ya nchi na sio kuwasiliana na WB, nchi kama nchi ina utaratibu wake wa makubaliano na benki hiyo na kama makubaliano hayo hayatatekelezwa, mradi huo utamnyima haki mtoto wa kike elimu.”

“Wanasiasa waache Serikali ifanye kazi, sio kila jambo kuleta upinzani tu, maendeleo ya elimu ni kwa faida ya watoto wetu na vizazi vijavyo, kama nchi imeweka taratibu zake, zifuatwe na kama kuna kasoro, zipo njia za kujadiliana kufanya marekebisho na sio kuvuka mipaka,” alisema Profesa Wangwe.

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi la Parole, Augustine Mrema alisema bado kuna watu hawaoni mambo mazuri ya mageuzi nchini ya kimaendeleo, yanayofanywa na Rais Dk John Magufuli, bali wanatafuta kila njia kukwamisha juhudi zake.

“Sasa hili la kuandika barua WB lina maana gani, vyombo vya ndani viliwasilishiwa lalamiko hilo?, utaonania sio njema. Tunaomba wamuache Rais Magufuli afanye kazi na sio kutafuta kumkwamisha, maendeleo anayopigania ni ya Watanzania wote,” alisema Mrema.

Akizungumzia mradi wa elimu ambao fedha hizo za mkopo zilipangwa kutumika kuboresha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema zitasaidia kuongeza idadi ya shule kwa ajili ya watoto wa kike, kwa kujenga shule za bweni 26 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 39,000 na shule za kutwa 1,000.

Pia, zitatumika kwa ajili ya upanuzi wa shule kongwe 50 ili kuongeza nafasi za wanafunzi 100 wa kike kwa kila shule na kukamilisha maabara. Mradi huo wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP) utawanufaisha wanafunzi milioni sita katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi