loader
Picha

DC- Msitegemee mafuta, fanyeni kazi

RAIS John Magufuli amesema shughuli za kidini ama kiimani, hazipaswi kufungwa kutokana na maafa ya vifo vya watu 20 mkoani Kilimanjaro, yaliyosababishwa na watu kukanyagana, wakiwahi kukanyaga mafuta ya upako, badala yake yashughulikiwe mapungufu yaliyojitokeza.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ametoa ujumbe huo wa Rais Magufuli jana wakati wa mazishi ya kitaifa ya watu 19, kati ya 20, yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa mjini Moshi. Watu hao walikufa baada ya kukanyagana walipokuwa wakifuata mafuta ya upako ya Mtume Boniface Mwamposa.

“Asubuhi wakati nazungumza na Rais kuhusu tukio hili, alisisitiza tushughulikie mapungufu yaliyojitokeza, badala ya kufunga shughuli za kiimani…mimi nasema tuzingatie vibali vyetu ili kuepusha maafa kama haya,” amesema Mghwira.

Alisema tayari Jeshi la Polisi, linafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo, ambapo pia viongozi waandamizi wa Mtume Mwamposa, wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Mghwira alisema pia baadhi ya watu, wanaodhaniwa ni vibaka, walikuwa miongoni mwa vyanzo vya watu kupata maafa hayo, kutokana na kitendo cha kujaribu kuwaibia waumini waliokuwa wakitoka mlangoni.

“Ninyi vibaka ambao ni sehemu ya maafa haya, lazima mjue damu ya watu iliyopotea na iliyomwagika, itakuwa juu yenu na malipo yenu yanakuja,” alisema mkuu wa mkoa.

Alisema tukio hilo limegusa pia wananchi wa mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Kwa upande wao, viongozi wa madhehebu ya dini, walisema wanapinga mfumo wa maombezi ya kidini, unaofanywa sasa kwa kasi, kwa kigezo cha kuleta uponyaji kwa waumini wao.

Aidha, viongozi hao waliomba serikali kutazama baadhi ya madhehebu, yanayotumia mgongo wa dini na ufahamu mdogo wa waumini katika kuwarubuni na kuwasababishia maafa.

Askofu Mkuu na Mwakilishi wa Umoja wa Makanisa ya KKKT, Moravian na Anglikana (CCT), Stanley Hotae alisema, “Hata Yesu hakuna mahali katika Biblia alielekeza waumini wapate utajiri bila kufanya kazi, baadhi ya viongozi wa dini wanasababisha waumini waangamie kwa kukosa maarifa.”

Alitaka waunini kutoyumbishwa na imani zao za asili, bali wamkiri Yesu katika kupata uponyaji wa kweli, huku pia akiwataka waumini kuongeza juhudi katika kazi na siyo vinginevyo.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya za mkoa huo, alitaka viongozi wa dini, kujitathmini na matendo na kauli zao, kabla ya kunyooshea vidole wengine.

“Viongozi wa dini wamekuwa wakiionya serikali katika baadhi ya mambo, lakini leo kabla hamjamulika tochi kuwaangalia wenzenu, angalieni katika miguu yenu kama kuna nyoka asije kuwagonga,” amesema.

Alitaka wananchi kuepuka mafanikio ya mkato na badala yake wafanye kazi ili kukabili maisha ya kila siku.

“Wengi wa watu waliofariki hapa ni wanawake na watoto. Najua wanawake mnakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo matatizo ya ndoa, Vicoba, matatizo ya familia na nyinginezo, lakini mkumbuke Yesu hakuweka mafanikio katika matunda, maji au mafuta,” amesema Sabaya.

Sabaya alitaka baadhi ya viongozi wa dini, kutotumia ufahamu mdogo au matatizo ya waumini, kama mitaji ya kuwatapeli na kuwaingiza katika matatizo, kama ambayo yametokea Februari Mosi, mwaka huu.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro, Patrick Boisafi alitaka serikali kufuatilia madhehebu ya dini ili kujua aina ya mafundisho yanayotolewa.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Nakajumo James, Moshi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi