loader
Picha

Magufuli- Nimewateua mlete mabadiliko

RAIS John Magufuli ameeleza sababu zilizomfanya awateue viongozi 15, aliowaapisha jana Ikulu jijini Dar es Salaam akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi.

Sambamba na hilo, amewataka viongozi na watumishi wa umma, kushirikiana katika kuijenga nchi kwa manufaa ya Watanzania wote, huku akiwataka makamanda katika Jeshi la Magereza na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, kushirikiana na makamishna jenerali wapya ili kufanya mambo mengi ndani ya majeshi hayo yaende vizuri.

Mbali na Dk Abbasi, Rais Magufuli jana aliwaapisha Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Zena Saidi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Leonard Masanja.

Wengine ni Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, William Masunga, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Steven Mashauri, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Judica Omari, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Tutuba na Kamishna wa Ardhi, Nathaniel Nhonge.

Kwa upande wa Mahakama, walioapishwa ni Msajili Mkuu wa Mahakama, Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Kelvin Mhina, makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambao ni Jaji Gerald Ndika, Julius Kalolo na Genoveva Kato, wakati Msajili wa Mahakama Kuu, Sharmillah Sarwatt aliapishwa na Jaji Kiongozi Dk Eliezer Feleshi. Rais Magufuli alisema sababu iliyomfanya kumteua Dk Abbasi ni kutokana na kazi nzuri, aliyoifanya ya kuisemea serikali katika mambo mbalimbali.

Alisema kutokana na umahiri huo, aliamua kumpandisha cheo na kumfanya kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo wakati huohuo akiendelea kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali hadi atakapoteua mtu mwingine kujaza nafasi hiyo.

Mbali ya kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Abbasi alikuwa Mkurugenzi Mkuu Idara ya Habari (MAELEZO) na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).

Kuhusu Katibu Mkuu Zena, alisema kitaaluma ni mhandisi na aliwahi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga.

Kutokana na kazi nzuri ya manunuzi aliyoifanya Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na kuwabana wakandarasi wasiokuwa waaminifu, ndiyo sababu iliyomfanya amteue katika nafasi hiyo.

“Wengine sijawahi kuwaona kwa macho lakini taarifa zenu ninazo. Shemdoe aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafinga, alifanya kazi nzuri ya kukusanya mapato makubwa na baadaye akapelekwa kuwa RAS Ruvuma, wakati Makondo alikuwa Kamishna Wizara ya Ardhi na alikuwa hapendwi kutokana na misimamo yake, nilikuwa naambiwa hafai, alichafuliwa kwa meseji na kutaka kumchonganisha na mume wake, Wizara ya Ardhi ina madudu mengi,” alisema Rais Magufuli.

Akiendelea kueleza sababu za kuwateua viongozi hao, Rais Magufuli alisema aliamua kumteua Mzee kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza kutokana na kazi nzuri aliyoifanya akiwa Mkuu wa Kamandi ya JWTZ Pangawe.

Alisema Mzee alifanikiwa kujenga nyumba na kununua magari.

Alisema kutokana na utendaji huo, aliamua kumpeleka Jeshi la Magereza ili nako alete mageuzi.

Alisema haiwezekani nyumba za Magereza, zijengwe na JKT wakati wafungwa wapo.

Lakini, pia mradi wa Sh bilioni 9 wa Kiwanda cha Karanga Moshi uliopo chini ya Magereza, haujakamilika kwa wakati.

Kuhusu Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, alisema alimteua Masunga kushika nafasi hiyo kwa sababu kama angemweka kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza, angeweza kusumbuliwa kama alivyofanyiwa Kamishna Jenerali Mstaafu Phaustine Kasike.

Alisema Kasike hakupata ushirikiano mzuri kutoka kwa wenzake, kwa kuwa licha ya kufanya ziara mbalimbali mikoani, lakini maagizo yake yalikuwa hayatekelezwi, hivyo alimtaka Masunga kulisimamia Jeshi hilo vizuri na ikiwezekana awatumie hata wafungwa, ikitokea moto unateketeza mashamba.

Mashauri alikuwa akifanya kazi katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kama mtafiti na mchunguzi, ingawa ana shahada mbili za kilimo na baadaye alikuwa DED Kishapu.

Kwa sasa anaenda kuwa RAS Ruvuma ili akashirikiane na Mkuu wa Mkoa, Chiristine Mndeme katika kuinua sekta ya kilimo huko.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, alimteua Judica kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, kutokana na kufanya kazi nzuri akiwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), baadaye alienda Wizara ya Fedha na Mipango na kisha alikuwa RAS Msaidizi Njombe, ambako alifanikiwa kuzuia wizi wa fedha za umma.

“Tutuba alikuwa Wizara ya Fedha na alisimamia vizuri fedha ya serikali iliyowekwa kwenye ‘Fixed Account’ na hakutaka iliwe, wakati Masanja aliongoza vyema timu za mashauriano ya kujenga Mradi wa Umeme wa Mto Rufiji; aliongoza timu iliyokwenda Ethiopia na baadaye Misri hadi kutangazwa kwa zabuni; Sarwatt alikuwa imara na madhubuti na alishawahi kutishiwatishiwa sana,” alisema Rais Magufuli.

Baada ya kuapishwa na Rais jana, Kamishna Jenerali wa Magereza, Mzee na Kamishna Jenerali mstaafu Kasike, walifanya makabidhiano ya ofisi katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya Magereza yaliyopo Dar es Salaam.

Mzee alisema atashirikiana na makamanda wenzake na askari kuhakikisha wanafanikisha mipango ya maendeleo ya jeshi hilo ili liweze kujitegemea.

Miongoni mwa mikakati yake ni kuanzisha miradi na viwanda, lakini pia kuhakikisha Jeshi la Magereza linajitosheleza kwa chakula na kuboresha makazi ya maofisa na askari.

“Nampongeza Kamishna Jenerali Mzee kwa kuteuliwa kushika wadhifa huu; naondoka nikiliacha Jeshi likiwa pamoja na nidhamu, changamoto iliyokuwepo ambayo naamini Kamishna Jenerali mpya ataifanyia kazi ni kuhakikisha Magereza linajilisha, linakuwa na makazi mazuri ya askari kwa sababu tayari kuna maandiko mazuri ya kitaaalamu tulikuwa tumeshayaandaa,” alisema Kasike ambaye ni Balozi Mteule.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi