loader
Marais wamlilia Moi

Marais wamlilia Moi

VIONGOZI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waliopo madarakani na wastaafu, wanaomboleza kifo cha Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Kenya, Daniel Arap Moi kilichotokea jana saa 11 alfajiri katika Hospitali ya Nairobi alikokuwa akipatiwa matibabu. Moi ambaye aliitumikia Jamhuri ya Kenya kwa miaka 24 kama Rais, amefariki akiwa na umri wa miaka 95 na kuacha historia iliyotukuka kwa uongozi wake ndani na nje ya Kenya.

Akilitangazia taifa na dunia nzima, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alisema maombolezo ya kitaifa, yatadumu kwa muda wote kuanzia jana mpaka siku ya kukamilika kwa mazishi yake.

Aliagiza bendera ya taifa, kupepea nusu mlingoti nchi nzima na kwenye Balozi na ofisi zote Kenya na nje ya nchi. Rais Uhuru alisema mazishi ya kitaifa ya Mzee Moi, yatapewa heshima zote za kijeshi na za kiraia.

Alituma salamu za rambirambi kwa watoto wa marehemu, ndugu na jamaa wa karibu.

“Taifa letu na Bara la Afrika lilinufaika na uongozi wa Mzee Moi. Alitumia maisha yake yote ya utu uzima kuwatumikia Wakenya na Afrika katika mambo mbalimbali. Baada ya kustaafu, aliendelea kuwa mshauri kwa viongozi wa Kenya na nje ya Kenya. Alishiriki katika miradi ya maendeleo, kazi za hisani na kupigania amani, umoja na upendo Afrika na duniani kote,”alisema Rais Uhuru.

Alisema kutokana na kuwa kiongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa Kenya na kuwa Mwanamajumui madhubuti, Moi ameacha alama iliyotukuka na kumfanya kuwa miongoni mwa viongozi wakubwa barani Afrika.

Alisema kutokana na kifo cha ghafla cha Rais Jomo Kenyatta, Moi alichukua hatamu za uongozi mwaka 1978 na kufanikiwa kuleta utulivu nchini humo, kutokana na mshituko uliolikumba taifa.

Alisema Moi aliiongoza vyema Kenya katika kurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa na aliamua kung’atuka madarakani kwa amani mwaka 2002. Pamoja na mambo menginie, Mzee Moi atakumbukwa kwa falsafa yake ya ‘Nyayo’ akimaanisha kufuata nyayo za mtangulizi wake Jomo Kenyatta.

Falsafa hiyo ilibeba mambo matatu muhimu, ambayo ni ‘Amani, Upendo na Umoja’ wakati wote wa uongozi wake.

Salamu za rambirambi

Viongozi mbalimbali akiwemo Rais John Magufuli wameungana na wananchi wa Kenya, kuomboleza kifo cha Mzee Moi kwa kutuma salamu zao za rambirambi.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais Magufuli alisema “Kwa niaba ya Serikali na Watanzania, nakupa pole Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na Wakenya wote kwa kuondokewa na Rais Mstaafu Daniel Toroitich arap Moi. Watanzania tutamkumbuka kwa uongozi wake mahiri, jitihada za kuimarisha uhusiano wetu na Kenya na kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete kupitia Kituo cha Utangazaji cha KTN cha Kenya, alisema Moi alikuwa chachu ya kufufua tena Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) akishirikiana na marais wenzake Ali Hassan Mwinyi wa Tanzania na Yoweri Museveni wa Uganda.

Kikwete alisema suala la kufufuliwa kwa EAC, lilishika kasi zaidi kipindi cha uongozi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa wakati yeye akiwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Alisema alipochaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, Moi alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuja kushuhudia kuapishwa kwake.

“Mzee Moi alijitoa sana katika kutatua migogoro katika ukanda wetu huu ikiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Lakini pia alisaidia kupatikana kwa uhuru wa Sudan Kusini.

Alijali amani ya EAC na tutamkumbuka kwa mema mengi ikiwemo kujenga uhusiano mzuri kati ya Kenya na Tanzania na nchi zingine na alikuwa mshauri mzuri,”alieleza Kikwete.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alisema Afrika imempoteza mtu muhimu, aliyejitoa kwa ajili ya taifa lake na Afrika kwa ujumla, aliyehamasisha zaidi masuala ya upendo na amani.

Alisema pamoja na kushirikiana lakini pia alifanya naye kazi kwa ukaribu zaidi, hasa katika kipindi ambacho wote wawili walikuwa ni marais katika nchi zao.

Anamkumbuka kwa mchango wake wa kurejesha EAC pamoja na kuhimiza amani na mshikamano kwenye nchi za Maziwa Makuu.

“Sote tuliofanya kazi naye kwa karibu, tutamkumbuka kiongozi huyu aliyetambulisha mfumo wa vyama vingi na kuumudu na kuliongoza taifa la Kenya kwa miaka 10 bila kutegemea msaada wowote kutoka nje,” alisema Mkapa.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema alikutana na Rais Moi kwa mara ya kwanza mwaka 1979 baada ya kupinduliwa kwa utawala wa Idi Amin. Pia aliendelea kukutana naye katika mikutano mbalimbali mjini Arusha na Mombasa.

Museveni alisema Moi alikuwa Mwana Afrika Mashariki mwenye bidii, aliunga mkono kwa dhati Umoja wa Afrika Mashariki na alikuwa tayari kuunga mkono kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki.

 

“Wakati tuliposaini makubaliano ya ushirikiano wa Afrika Mashariki tulikuwa watatu; nilikuwepo mimi, Moi na Mwinyi wa Tanzania ... Mzee Moi alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wazi sana katika kuunga mkono Shirikisho la Afrika Mashariki,” alisema Museveni.

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kupitia ukurasa wake wa Twitter alisema “Kwa niaba ya Watu wa Burundi na kwa niaba yangu mwenyewe, naungana na Wakenya na wananchi wote wa Afrika katika kutoa salamu za pole kwa familia kutokana na kifo cha Rais mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi.”

Familia yazungumza Akizungumza kwa niaba ya familia, Gideon Moi ambaye ni mtoto wa marehemu, aliwashukuru Wakenya kwa kuwafariji katika kipindi hiki cha msiba wa baba yao.

Gideon ambaye ni Seneta wa Kaunti ya Baringo, alisema alishuhudia baba yake akiaga dunia kwa utulivu, kwani alikuwa pembeni yake.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/51933d6d9eb9a116b73128dbb74f2f74.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi