loader
Picha

EU yaachia mabilioni ya fedha iliyoyazuia

UMOJA wa Ulaya (EU) umekamilisha mazungumzo na Tanzania, yaliyoruhusu kuendelea kwa mpango wa umoja huo, kuchangia bajeti ya maendeleo na Sh bilioni 132 zilizozuiwa zimeruhusiwa.

Aidha, kwa sasa EU pamoja na Tanzania, wanaandaa mpango mwingine wa miaka saba, unaotarajiwa kuanza mwaka huu. Hayo yalibainishwa Ikulu jijini Dar es Salaam jana na Balozi wa EU nchini, Manfred Fanti alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli.

Pamoja na Fanti jana, Dk Magufuli pia alikutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), Dk Stergomena Tax na Balozi wa China nchini, Wang Ke.

Balozi Fanti alisema mazungumzo yake na Dk Magufuli, yamekuwa na manufaa makubwa, ambapo wamejadili maendeleo mazuri ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na umoja huo.

Alisisitiza kuwa katika siku za karibuni, EU na Tanzania zimekamilisha mazungumzo yaliyoruhusu kuendelea kwa mpango wa EU, kuchangia bajeti ya maendeleo ya Tanzania.

Alisema Sh bilioni 132 zilizokuwa zimezuiwa, zimeruhusiwa na sasa wanaandaa mpango mwingine wa miaka saba, utakaoanza mwaka huu. Balozi Fanti alisema kwa jinsi anavyoyaona maendeleo ya Tanzania, ana matumaini makubwa kuwa EU itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na nchi hii ili kufanya vizuri zaidi. Kwa upande wake, Dk Magufuli alimshukuru balozi huyo kwa juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa Tanzania na EU.

Alimhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na EU katika masuala mbalimbali, yenye maslahi kwa pande zote mbili. Dk Stergomena alisema alikuja kutoa taarifa ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya SADC, ikiwemo uendelezaji wa viwanda na kanda huru ya biashara.

Aliipongeza Tanzania kwa hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa, ikiwemo ujenzi wa barabara na reli na kuongeza uzalishaji wa umeme. Katika mazungumzo yake na Balozi wa China nchini, Wang Ke, Rais Magufuli alimkabidhi barua aliyomwandikia Rais wa China, Xi Jinping akimpa pole kwa janga la homa ya virusi vya Corona, lililolikumba Jiji la Wuhan nchini humo na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Pamoja na kukabidhi barua hiyo, Rais Rais Magufuli alisema Tanzania imeguswa na kulipuka kwa janga hilo na ipo tayari kutoa ushirikiano wowote, ambao Serikali ya China itahitaji katika jitihada za kukabiliana na homa hiyo.

“China ni ndugu zetu ni marafiki zetu, tunatoa pole kwa Mheshimiwa Rais Xi Jinping na Wachina wote, waliopatwa na madhara ya homa hii, daima Tanzania tupo pamoja na China na katika hili tupo pamoja pia” alisisitiza Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Ke alimshuru Rais Magufuli kwa kuguswa na janga hilo na kuungana na China katika kipindi hiki kigumu. Alitumia nafasi hiyo kueleza hali ilivyo nchini China.

Alisema serikali ya China imeanza kupata mafanikio katika kukabiliana na homa hiyo, ili kuzuia isienee katika nchi zingine kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) na nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Alimhakikishia Rais Magufuli kuwa licha ya Tanzania kutokuwa na mtu yeyote aliyethibitika kuambukizwa homa ya corona, Watanzania 400 waliopo katika Jiji la Wuhan, ambao wengi wao ni wanafunzi, hawajaambukizwa homa hiyo. Kwamba jitihada za kuhakikisha wanakuwa salama, zinafanyika.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi