loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mtoto wa Moi: Baba yangu hakuogopa kifo

MTOTO wa Marehemu Daniel Arap Moi, Gideon Moi (pichani) amesema baba yake hakuogopa kifo wakati wa uhai wake. Gideo alisema kuwa siku zote Mzee Moi alikuwa akimwambia kuwa kukubali uhai ni lazima pia kukubali kifo.

Alisema baba yake alitoa kauli hiyo kwa sababu aliamini kuwa kuna maisha mengine baada ya kifao. “Kamwe hakuogopa kifo, nina hakika na hilo… nimeridhishwa kwamba Wakenya wameonesha upendo na mapenzi ya dhati wakati huu, kwa unyenyekevu natoa shukrani zangu kwenu nyote, Baba ameenda kwa amani. Nilikuwa naye muda wote na nilifanya kila niwezalo katika kumuuguza,”alisema Gideon.

Kwa upande wake, aliyekuwa Msemaji wa Rais Moi, Lee Njiru, alisema kuwa Mzee Moi alikuwa kama baba kwake kwa muda wote mpaka alipoaga dunia juzi. Njiru ambaye alihudumu katika nafasi hiyo kwa miaka 42, alisema mara baada ya Rais Mwai Kibaki kuwa Rais wa Kenya, yeye aliendelea kufanya kazi na Mzee Moi hali iliyomfanya kuwa karibu naye zaidi.

“Uhusiano wetu ukahama kutoka kuwa uhusiano kati ya mwajiri na mtumishi na kuwa uhusiano kama wa baba na mtoto. Alikuwa mshauri wangu na aliamini katika kufanya kazi kwa bidii,” alisema Njiru.

Alisema anadhani alimjua Mzee Moi vizuri zaidi kuliko mtu mwingine yeyote kwa kuwa alifanya naye kazi kwa karibu na alimhudumia kwa muda mrefu. Njiru alisema katika kufanya kazi na Moi aliweza kutembelea maeneo mbalimbali ya Kenya na kujuana na watu wengi.

Njiru alizaliwa mwaka 1949 na alisoma masomo ya uandishi wa habari ngazi ya diploma katika Taasisi ya Mawasiliano ya Umma Kenya baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari mwaka 1968. Baada ya hapo alikuwa Ofisa Habari huko Kakamega mwaka 1975 na mwaka 1976 alipelekwa kuwa Ofisa Habari katika kitengo cha habari cha Rais Ikulu.

foto
Mwandishi: NAIROBI, Kenya

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi