loader
Picha

Wapelelezi wamkera Magufuli

RAIS Dk John Magufuli amesema katika kipindi cha miaka minne, Serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa, kushughulikia kero zinazoukabili mhimili wa Mahakama, ili kuboresha mfumo wa utoaji haki.

Amekerwa na tabia ya wapelelezi kuchelewesha kesi na kusababisha mateso kwa watuhumiwa na familia zao, hivyo kusababisha mlundikano wa mahabusu magerezani na kuikwaza Mahakama.

Lakini, pia amekasirishwa na mabaraza ya ardhi, kwa kusababisha migogoro ya ardhi nchini.

Amebainisha hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria Tanzania, ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi.

Dk Magufuli aliyataja baadhi ya mafanikio ambayo serikali yake imeyafanya kwenye sekta ya sheria na mahakama kuwa ni kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa kupiga vita rushwa, ucheleshaji wa kesi, ucheleshaji wa upelelezi na mlundikano wa mahabusu magerezani.

Kuhusu ucheleweshwaji wa kesi, alisema katika kipindi cha mwaka 2019, mahakama iliweza kusikiliza mashauri yote kwa asilimia 100, wakati mwaka 2016 mlundikano wa mashauri mahakamani ulipungua kutoka asilimia 12 hadi kufikia asilimia 5. Katika Mahakama za Mwanzo mlundikano wa mashauri, ulipungua hadi kufikia asilimia 0.

Awali, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, alimweleza Rais kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari Mosi hadi Desemba 31,2019, mashauri 272,326 yalifunguliwa katika mahakama zote nchini na kati ya hayo, mashauri 271,214 yalisikilizwa. Jaji Mkuu alisema kuwa asilimia 70 ya mashauri hayo, yalisikilizwa katika Mahakama za Mwanzo.

Alisema mashauri yote yaliyofunguliwa kwenye mahakama hizo za mwanzo, yalisikilizwa.

“Katika kupunguza tatizo la ucheleweshwaji wa kesi, Serikali ya Awamu ya Tano iliajiri majaji wapya 11 wa Mahakama ya Rufaa, majaji 39 wa Mahakama Kuu na Mahakimu 396. Mahakimu wengine 195 walipewa mamlaka na serikali ya kusikiliza mashauri katika Mahakama Kuu mwaka 2019 ambapo mahakimu 98 waliweza kumaliza jumla ya mashauri 1,132. Nakuomba Waziri wa Katiba na Sheria uniletee majina ya mahakimu hawa,”alieleza Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Rais, mafanikio mengine ambayo mahakama imeyapata katika kipindi cha miaka minne ya serikali yake ni kuanzishwa kwa Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mwaka 2016.

Alisema mahakama hiyo iliweza kusajili mashauri 119 na mashauri 89 sawa na asilimia 64, yalimalizika na kuingiza Sh bilioni 13.6 kutokana na faini na Sh bilioni 30.6 kutokana na fidia.

Aliyataja mafanikio mengine katika sekta ya sheria na mahakama kuwa ni kuanzishwa kwa mahakama zinazotembea na kuanzishwa kwa mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ambao umerahisisha usajili wa mashauri na kusikiliza mashauri kwa njia ya video.

Kuanzishwa kwa mfumo wa Tehama, pia kumeongeza maduhuri ya serikali kutoka Sh bilioni 1.6 mwaka 2017 hadi Sh bilioni 2.5 mwaka 2019. Jambo jingine ambalo serikali yake imefanikiwa kulifanya ni kusaini hati mbili mwaka 2018, ambazo zilisaidia kuitenganisha Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) kujitegemea kutoka kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), hali iliyopunguza tatizo la watu kubambikiwa kesi.

Rais Magufuli alisema kabla ya Ofisi ya DPP kujitegemea, baadhi ya vyombo kama vile Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), vilikuwa na mamlaka ya kukamata, kupeleleza na kumfikisha mtuhumiwa mahakamani, ambapo watumishi wasiokuwa waaminifu, walitumia fursa hiyo kuwabambikia watu kesi.

Kwamba baada ya DPP kuanza kufanya kazi zake kwa uhuru, aliweza kuwaachia huru watuhumiwa 1,422 katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana, ambao miongoni mwao wapo waliobambikiwa kesi. Kwamba katika kipindi cha miaka minne, serikali yake imesamehe wafungwa 38,801 huku wafungwa 5,533 aliwasamehe wakati wa sherehe za miaka 58 ya Uhuru, zilizofanyika jijini Mwanza.

Magufuli alisema washitakiwa 335 waliokiri makosa yao kwa DPP, walisamehewa. Alisema majadiliano kuhusu kuwarudisha nchini kwao raia wa kigeni 1,415 wa Ethiopia, walioko kwenye magereza nchini, yanaendelea.

“Pia tumeshughulikia maslahi ya watumishi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya mahakama. Katika kipindi cha miaka minne tumejenga Mahakama Kuu mbili moja mkoani Mara na nyingine Kigoma, tumekarabati Mahakama Kuu nne ikiwemo ya Dar es Salaam, Mbeya na Shinyanga, tumejenga mahakama za wilaya 15 na mahakama za mwanzo 11, pia nitatoa shilingi bilioni 10 ili muanze ujenzi wa Mahakama Kuu Dodoma,”alisema Rais Magufuli.

Changamoto Mbali na mafanikio hayo, Rais Magufuli alikerwa na tabia ya wapelelezi kuwa chanzo cha ucheleweshaji wa kesi na kuwataka wabadilike kwani jambo hilo linawanyima haki watu na kuwapa shida mahakimu kwa kuwa wanalaumiwa wao kuwa wanachelewesha kesi wakati kosa ni la wapelelezi.

Alisema kutokana na hilo kumekuwa na msongamano magerezani ambako kuna jumla ya wafungwa na mahabusu 32,208 takwimu ambayo inathibitisha kuwa kuna tatizo kwa upande wa wapelelezi kwa kuweka mazingira yanayotaka watu watoe hongo ili kesi zao zisikilizwe mahakamani.

Sambamba na hilo Magufuli alikerwa na tabia ya mabaraza ya ardhi ambayo yako chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kusababisha migogoro ya ardhi na dhuluma kwa wananchi hususani wanawake na wajane.

Kutokana na hilo, alimweleza Jaji Mkuu kwamba iko haja ya mabaraza hayo kuwa chini ya mhimili wa mahakama, kwa kuwa matendo yao yanaichafua mahakama.

“Nilikuwa Wizara ya Ardhi na kuna majina niliyaweka kwenye orodha ya watu waliotakiwa kufukuzwa kazi, lakini nashangaa mpaka leo bado wapo,” alisema Rais Magufuli.

Jaji Mkuu

Pamoja na mambo mengine, Jaji Mkuu Profesa Juma alimweleza Rais kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau Kuweka Mazingira Wezeshi ya Uwekezaji,” inawakumbusha wadau wa mahakama, kutokuwa kikwazo na kizuizi katika kufanikisha shughuli za biashara na uwekezaji nchini ili taifa liweze kufikia uchumi wa kati, shindani na wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

“Nadharia ya sheria na falsafa ya sheria inazungumzia mambo mawili, kwanza ni Falsafa Kuu ambayo inataka sheria ziambatane na maadili kama ilivyo sheria zetu zinavyopinga ushoga, hivyo sheria inatakiwa kusimamia maadili katika biashara na uwekezaji, jambo la pili ni Falsafa Tanzu ambayo inataka sera zinazotungwa zilete furaha na mafanikio kwa watu, mambo haya mawili ndiyo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano,”alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alifurahishwa na hotuba ya Rais wa Chama cha Mawikili wa Tanyanyika (TLS), Dk Rugemeleza Nshalla na kuahidi kuifanyia kazi hotuba hiyo.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi