loader
Kinana, Makamba wahojiwa Dar

Kinana, Makamba wahojiwa Dar

MAKATIBU wakuu wawili wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Yussuf Makamba, wameitikia mwito wa chama hicho wa kwenda kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Usalama na Maadili.

Wakongwe hao wa siasa nchini, walifika katika Ofisi Ndogo za CCM Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam jana, saa chache baada ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ali kusema hakuna mpasuko ndani ya chama hicho na kwamba wale wote wanaotakiwa kwenda mbele ya kamati kujieleza, watakwenda.

Baadaye picha ziliwaonesha Kinana akiwa katika mavazi ya kawaida na Makamba akiwa amevalia sare za CCM – suruali nyeusi na shati la kijani pamoja na baraghashia yake, wakizungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu, Dk Bashiru, katika moja ya vyumba vya ofisi Lumumba.

Wawili hao walifika Lumumba muda wa saa nane mchana jana, na baadaye wakati wa kutoka, Dk Bashiru alionekana akizungumza na Mzee Makamba kwenye gari la mstaafu huyo.

Si Kinana wala Makamba aliyekuwa tayari kuzungumza na gazeti hili kuhusu yaliyojiri jana katika kikao hicho, hasa baada ya kuwapo kwa maneno mengi kuhusu wastaafu hao, ambayo Dk Bashiru aliyapuuza jana, wakati akimpokea aliyekuwa kada wa chama hicho, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyerejea CCM.

Hata hivyo, katika taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alithibitisha kuwa Makamba na Kinana jana walifika katika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba, kuitikia wito wa Kamati Ndogo ya Usalama na Maadili inayoongozwa na Mangula.

“Makatibu wakuu hao Ndugu Abdulrahman Kinana na Ndugu Yusuf Makamba wamefika katika Ofisi hizo majira ya mchana na kupokelewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Ndugu Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Bashiru Ally Kakurwa,” ilieleza taarifa ya Polepole.

Akimpokea Sumaye jana Lumumba, Katibu Mkuu huyo alisema anasikitishwa na maneno yanayodai kuwa chama hicho kina mpasuko wakati hali ni shwari ndani ya CCM.

“Hakuna kiongozi yeyote ambaye amepelekewa wito na akakataa kuitikia wito, uongo. Huyo anayejipenda, hajipendi? Maana yake mambo ya kuitana hayajaanza leo. Mama Anna Abdallah yameanza leo haya? (Anamuuliza Anna Abdallah –Mdhamini wa CCM). Watu huitwa, wengine kukaripiwa, wengine onyo kali, wengine kusamehewa, wengine kufukuzwa,” alisema Dk Bashiru.

Aliongeza kuwa mambo hayo, yalianza tangu enzi za TANU na kutoa mfano wa Mzee Abdulaziz Mtemvu (marehemu), aliyesema alikimbia TANU na kutangaza kujiuzulu, kabla ya chama hicho kukaa na kumfukuza.

“Sijazaliwa mie, Magufuli (Rais John Magufuli – Mwenyekiti wa CCM Taifa) hajazaliwa, kuna jipya gani?” alihoji.

“Kama walitarajia iwe hivyo, kipindi hiki halipo na halitakuwepo,” alisema Dk Bashiru.

Hivi karibuni, chama hicho kilimhoji kwa saa tano Membe jijini Dodoma, ambaye baada ya kutoka alibainisha furaha yake juu ya kikao hicho, huku akibainisha kuwa walizungumzia mambo mazito ya kitaifa.

Uamuzi wa makada hao kutaka kuhojiwa, ulifikiwa Desemba 13, mwaka jana baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kukaa na kuagiza waitwe baada ya kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya kimaadili.

Jaji Warioba alibainisha kuwa kinachoendelea kwa sasa ndani ya CCM kuhusu kuwahoji wanachama wake wakongwe ni jambo la kawaida kwa chama hicho na wala si kitu kipya.

Jaji Warioba aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akihojiwa na televisheni ya ITV kupitia kipindi chake cha Konani.

Alisema kitendo cha CCM kwa sasa kuwaweka kiti moto makatibu wakuu wa chama hicho wastaafu, Abdulrahaman Kinana na Yusuf Makamba pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ni jambo la kawaida kwa chama hicho, “Kuna viongozi walihojiwa na kufukuzwa hata kipindi kile cha TANU, hiki si kitu kipya ndani ya CCM,” alieleza.

Aidha, katika kipindi hicho, Jaji Warioba alizungumzia Katiba na kueleza kuwa lazima itakuja tu, kwani mchakato mzima uliofanyika ikiwemo maoni ya wananchi yaliyokusanywa upo na umehifadhiwa vizuri.

“Ninachojua ni kwamba Katiba itakuja, lazima mtambue kuwa mchakato wa Katiba unachukua muda. Katiba ya mwaka 1977 mchakato wake ulianza tangu mwaka 1965. Tulifanya mchakato, wananchi wametoa maoni yao, najua Katiba itakuja tu, kusiwe na wasiwasi” alisisitiza.

Alizungumzia pia namna alivyotupiwa maneno katika kipindi cha mchakato huo wa Katiba na kueleza kuwa aliyachukulia kawaida tu, kwa kuwa kiongozi yeyote lazima akutane na hali hiyo.

“Kilichotokea wakati ule yalisemwa maneno mengi na mengine mazito kidogo, lakini nilichukulia kama changamoto, kwa kuwa najua ukiwa kiongozi mambo kama hayo ni ya kawaida. Hata zile taarifa kama nilipigwa, sikupigwa, hayo ni mambo ya media (vyombo vya habari),” alisisitiza

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8c65568ffd844cfc264fd6beb3a9a98b.jpeg

MWENGE wa Uhuru unaendelea ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi