loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kauli za amani, umoja zatawala mazishi ya Moi

MAELFU ya wananchi wa Kenya wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na viongozi wa mataifa mbalimbali walijitokeza kumuaga aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Daniel Arap Moi katika Uwanja wa Nyayo, Nairobi jana.

Katika salamu zao za rambirambi, viongozi hao walisisitiza umoja, mshikamano na uzalendo na kuwataka Wakenya kumuenzi kwa kudumisha amani kwa maisha yao yote. Moi ambaye alizaliwa mwaka 1924, aliiongoza Kenya kwa miaka 24 kuanzia mwaka 1978-2002 na kupewa jina maarufu la utani la ‘Nyayo’ kwa kuwa mara tu baada ya kuwa rais aliahidi kufuata nyayo za mtangulizi wake Rais Jomo Kenyatta.

Moi alifariki dunia alfajiri ya Februari 4 mwaka huu kwenye Hospitali ya Nairobi. Mbali na wananchi hao, marais saba akiwemo Paul Kagame wa Rwanda, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Yoweri Museveni wa Uganda, Ismail Omar Guelleh wa Djibout, marais wastaafu wa Tanzania akiwemo Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete ambao walimwakilisha Rais John Magufuli pamoja na wajumbe kutoka mataifa 18 walihudhuria ibada hiyo ya kutoa heshima za mwisho.

Rais Kenyatta aliwashukuru wakuu wa nchi, wawakilishi, wajumbe na watu mbalimbali walioungana nao katika kuomboleza kifo cha Rais Moi. Uhuru aliwataka Wakenya maisha yao yaakisi maisha ya Mzee Moi aliyeheshimu na kuamini katika amani, upendo na umoja.

Salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Dk John Magufuli zilizosomwa na Rais mstaafu Mkapa. Dk Magufuli alisema Mzee Moi siyo tu kwamba atakumbukwa kwa kuitumikia vyema nchi yake, bali pia kwa mchango wake wa kuifufua Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kudumisha amani na usalama pamoja na kupigania maslahi ya EAC na Afrika katika nyanja za kimataifa.

“Tunamkumbuka kwa kudumisha udugu na ushirikiano na Tanzania na kwa kipekee kujenga uhusiano usio kifani kati ya nchi zetu hizi mbili, Mwenyezi Mungu awajalie wananchi wote wa Kenya amani, nguvu na faraja,”alisema Rais Magufuli.

Mbali na kutoa ujumbe huo wa Rais Magufuli, kwa upande wake, Mkapa alisema katika kipindi chake cha urais cha miaka kumi, alifanya kazi kwa karibu na Mzee Moi kwa miaka saba.

Alisema kwake yeye Mzee Moi ni kama Mwalimu katika masuala ya uongozi na utawala na ndiyo sababu akaona ni lazima ashiriki mazishi yake na kushirikiana na Wakenya katika kumwombea.

Naye Rais mstaafu Kikwete alisema: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mzee Moi. Namfahamu Mzee Moi tangu nikiwa shule, nimesoma habari zake kuhusu harakati za kudai uhuru wa Kenya, baadaye nilipokuwa Waziri wa Nishati, nilitumwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuja kuzungumza naye kuhusu ushirikiano wetu kwa kuwa tulikuwa na mpango wa kujenga bomba la gesi kutoka Songosongo kwenda Dar es Salaam”.

Kwa kuwa mradi huo ulilenga kuwanufaisha wana EAC wote katika kuzalisha nishati ya umeme kwa maendeleo ya Tanzania na Kenya, Kikwete alisema Mzee Moi alilipenda wazo hilo na kukubaliana nalo, lakini pia alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, alifanya kazi kwa karibu na Wakenya chini ya Uongozi wa Rais Moi katika kuifufua EAC.

Kwa upande wake Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alisema viongozi wa Afrika wanapaswa kuwa kama madaktari kwa kugundua magonjwa au matatizo yanayowakabili wananchi wao jambo ambalo Moi alilifanya.

Museveni alisema kama kiongozi hajui matatizo yanayoikabili nchi yake hawezi kutibu tatizo hilo na matokeo yake nchi inaweza kuingia kwenye matatizo makubwa. Alisema ni jambo zuri kwa kiongozi kukumbukwa kwa mazuri baada ya kumaliza uongozi na siyo kwa mabaya kama alivyofanya Pilato kwa kumnyonga Yesu Kristu kama Biblia Tatakatifu inavyoeleza.

Alisema Mzee Moi atakumbukwa kwa mambo matatu ambayo ni uzalendo kwa nchi yake kwa kuwa mwaka 1964 aliamua kukivunja Chama chake cha Kidemokrasia cha KADU na kujiunga na KANU. Alisema Moi na viongozi wenzake katika KADU waligundua umuhimu wa umoja na kuwataka Wakenya wamuenzi kwa kudumisha amani na umoja maisha yao yote.

Viongozi wengine waliotoa salamu zao za rambi rambi ni Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibout na Makamu wa Rais wa Nigeria. Rais huyo wa Awamu ya Pili wa Kenya atazikwa leo nyumbani kwake huko Kabarak-Nakuru ambapo marais zaidi ya 10 na wajumbe kutoka mataifa zaidi ya 16 wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo.

Moi ndiye aliyeujenga Uwanja wa Nyayo mwaka 1981 wenye uwezo wa kuchukua watu 30,000 baada ya kuona kwamba Uwanja wa City una uwezo wa mdogo wa kuchukua watu 10,000 na baadaye kwa kushirikiana na Wachina alijenga Uwanja wa Kasarani wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, Mwili wa Moi ulichukuliwa na Jeshi kutoka Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Lee jana saa 2:00 asubuhi kwenda Ikulu na baadaye kwenye uwanja wa Nyayo. Wanajeshi 20 wenye cheo cha Kanali wakiongozwa na Brigedia Jenerali Joachim Mwamburi waliongoza jukumu la kuufikisha Mwili wa Moi Uwanja wa Nyayo.

WANAFUNZI wenye ulemavu wanaosoma shule za msingi mkoani Dodoma wameiomba ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi