loader
Picha

Magufuli amfukuza kazi aliyechana Kurani

RAIS John Magufuli amemfukuza kazi Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Daniel Maleki, kwa kosa la kuchana na kutemea mate kitabu kitakatifu cha Kurani.

Tayari mtumishi huyo, mkazi wa mtaa wa Mbumi “B, alishasimamishwa kazi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, kwa kosa hilo, huku akifunguliwa mashitaka na jeshi la polisi ya kukashifu dini.

Akizungumza baada ya kuzindua jengo la manispaa na Jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni katika eneo la Gezaulole, Kigamboni jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli amesema kamwe Serikali yake haiwezi kukaa na wafanyakazi wa aina hiyo.

“Nakushukuru (Jafo) umechukua hatua ya kumsimamisha kazi, mimi namfukuza kazi kabisa, muandikie barua ya kumfukuza, akitoka huko kwa adhabu atakayoipata atajua mwenyewe atakapoyatafuta maisha,” alisema Rais.

Alisema pamoja na kwamba mtumishi huyo kesi yake inaendelea, ashinde asishinde, si mfanyakazi tena wa serikali yake.

Mtumishi huyo amekumbwa na dhahama hiyo, baada ya kusambaa kwa picha katika mitandao mbalimbali ya kijamii, zikimuonesha akichana na kutupa kitabu cha Kurani.

Jafo alisema amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ya Kilosa, kumsimamisha kazi mtumishi huyo na hatua nyingine zichuliwe dhidi yake.

“Nayasema haya kwa kuwa mimi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi na huyu mtumishi yupo katika wizara yangu. Halmashauri ya Kilosa ni moja ya maeneo yangu, hivyo natoa maagizo haya na yatekelezwe mara moja,”amesema Jafo.

Alisema kuwa kitendo kilichofanywa na mtumishi huyo, hakipaswi kufumbiwa macho, hivyo Mkurugenzi wa Kilosa anatakiwa kuchukua hatua mara moja ya kumsimamisha kazi.

Agizo la Jafo lilitolewa siku moja, baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, kumkamata mtumishi huyo.

Baada ya upelelezi kukamilika, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa na kusomewa mashitaka ya kuudhi na kukashifu dini.

Video fupi iliyosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ilimuonesha kijana huyo ambaye anadaiwa kuwa ni Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, akichana kitabu cha Dini ya Kiislamu, Juzuu Amma ambayo ni sehemu ya Kurani Tukufu.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa wiki moja kwa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Manispaa ya Kigamboni, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Sara Msafiri, wawe wamehamia kwenye majengo ya NSSF Kigamboni.

Alisema haiwezekani watumishi hao, wawe wanaishi Temeke, ambayo ni wilaya jirani, wakati wao wanafanya kazi Kigamboni, huku majengo hayo ya NSSF yakiwa wazi.

“Naagiza wakae bure kwa muda wa mwaka mmoja. Hatuwezi kuacha nyumba zinakaa bure wakati watu wapo hawana pa kukaa,” alisema Rais.

Aidha, alimuagiza Waziri Jafo kutafuta popote kiasi cha Sh bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi hao katika eneo ambalo zimejengwa ofisi za halmashauri.

Aliagiza kuwa mkandarasi atakayepatikana, ahakikishe ujenzi huo unakamilika ndani ya miezi sita.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Ngw’ilabuzu Ludigija alisema serikali iliipatia halmashauri hiyo Sh bilioni 4.3 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri, lenye uwezo wa kuchukua watumishi 450.

Alisema jengo hilo tayari limeshakamilika na kuanza kutumika. Jengo la ofisi ya mkuu wa wilaya, limegharimu Sh bilioni 1.6. Nalo pia limeanza kutumika tangu Agosti mwaka jana. Awali, Kigamboni ilikuwa ni sehemu ya wilaya ya Temeke.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi