loader
Picha

Tanesco wapewa mwezi mmoja kufunga umeme Mtwara

WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani ametoa mwezi mmoja kwa wataalamu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) mkoani Mtwara kuhakikisha wananchi wa kijiji cha Nagaga wilayani Masasi mkoani humo wanapata huduma hiyo ili kuharakisha shughuli za maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo.

Agizo hilo lilitolewa hivi karibuni na waziri huyo wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.

Ziara hiyo ililenga kuwasha na kukagua hali ya umeme kijiji cha Nagaga na Matogoro na pia kusikiliza kero za wananchi hao juu ya suala hilo la umeme kwani umeme ni fursa lakini pia unaleta usalama.

Waziri Kalemani pia alikemea suala la wananchi kununua nguzo au transfoma za umeme kwani suala hilo haliwahusu na badala yake walipie huduma ya umeme tu na si kusubiri nguzo ndipo walipie kufungiwa.

Alisema serikali imepeleka fedha nyingi katika maeneo hayo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi hao na umeme ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo na mkoa kwa ujumla hivyo kila mwananchi ahakikishe anaweka umeme katika nyumba yake ili kuwezesha kukuza uchumi wao.

“Ndugu zangu si kusudi langu kufanya mkutano huu bali nimefanya mkutano kwa ajili ya kujiridhisha kama kweli maagizo ya serikali ya kuona kila kijiji kinapitiwa na umeme yanatekelezwa kama inavyotakiwa na nimeona kazi ni nzuri lakini niombe tu wananchi ni lazima kila mwananchi alipie. Serikali inataka kuona kila mwananchi anatumia umeme katika nyumba yake,” alisema Kalemani.

Mkazi wa Nagaga, Arafati Mangochi alipongeza kitendo cha waziri huyo kutembelea kijijini hapo kufanya kitendo cha kihistoria kwa wananchi hao cha kuwawashia umeme na kuzungumza na wananchi.

Alisema ni faraja kubwa kwao kwani inaonesha wazi namna ambavyo serikali inajali maendeleo yao huku akiahidi kulipia umeme ili siku za mbele aweze kutumia nishati hiyo kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.

Mkazi wa Kijiji cha Matogoro, Yusufu Mitole alisema “mimi ni mjasiriamali, nina duka la vyakula lakini kama bidhaa nyingine hizi zinahitaji ubaridi, maji, soda au juisi sasa kwa vile hakuna umeme nalazimika kuuza vitu vya moto lakini sasa serikali ilivyotuletea umeme kijijini, nitalipia haraka ili niweze kuboresha huduma zangu. Nitanunua friji, nitakuwa nauza vitu vya baridi na kufanya shughuli za maendeleo”.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arumeru imewafutia mashitaka washitakiwa ...

foto
Mwandishi: Sijawa Omary, Masasi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi