loader
Picha

Enzi za usafiri wa meli inavyorudi Ziwa Victoria

MIAKA ya 1970 na 1980, usafi ri wa uhakika wa majini ulikuwa maarufu sana kwa wakazi wa kanda ya Ziwa. Majina kama Mv Victoria, Mv Serengeti, Mv Bukoba (iliyopata ajali), Mv Umoja na Mv Butiama yalikuwa yakitajwa sana.

Usafiri huu ulikuwa ukiwasaidia sana wananchi na hususani wafanyabiashara kutokana na kuunganisha miji ya Musoma, Mwanza, Nansio (Ukerewe) na Bukoba. Kutokana na meli kuwa mithili ya nyumba, wafanyabiashara walipokuwa wanakwenda katika mojawapo ya miji walifanya kazi ya kukusanya au kuuza bidhaa zao mchana, kisha usiku wanaingia kwenye meli.

Kunapopambazuka wanakuwa tayari wamefika katika miji yao. Yaani wanafanya kazi mchana na usiku wanaenda kulala kwenye meli huku wakisafiri. Usafiri huu pia uliwaunganisha wananchi wa mikoa ya kanda ya Ziwa na wenzao wa nchi za Kenya na Uganda.

Mwishoni mwa mwaka jana, Mtendaji wa Kata ya Bakoba ilipo bandari ya Kemondo Bay mkoani Kagera, Godian Gwabunga, alisema wakati bandari hiyo inafanya kazi zake sawia miaka ya sabini na themanini, wakazi wa Kemondo na maeneo ya jirani walikuwa wakinufaika sana kiuchumi.

“Tulikuwa tukiagiza mizigo Mwanza hususani biashara za madukani na pia tukisafirisha mizigo yetu, kama vile ndizi kwenda Mwanza na maeneo mengine kwa gharama nafuu. Lakini baada ya usafiri wa meli kulegalega hali ikawa ngumu,” alisema.

Mbaruku Hussein, mfanyabiashara wa zamani wa mbao mjini Musoma alisema kwamba miaka ya sabini na themanini alipokuwa akifanya biashara hiyo na baba yake, walikuwa wakifuata mbao Tabora au Mpanda na kuzisafirisha zikiwa kwenye mabehewa hadi Musoma Mjini kwa gharama nafuu sana. “Yaani, behewa linakuja kutoka Tabora kwa njia ya reli hadi Mwanza.

Likifika Mwanza linaingia kwenye meli ya Mv Umoja hadi hapa bandari ya Musoma. Sisi tunakwenda pale kupakua mbao kwa malori kuleta kwenye magodauni yetu ya kuuzia mbao,” alisema. Katika mahojiano na gazeti hili, Mbaruku alisema baada ya usafiri huo kulegalega kuanzia shirika la reli ambalo awali ndilo lilikuwa pia likimiliki meli hizi za umma pamoja na bandari, wakaanza kulazimika kusafirisha mbao kwa kutumia malori.

“Hali hii iliongeza gharama sana za mbao na hivyo kufanya samani kuwa ghali. Hali hii ilichangia pia kuachana na biashara ya mbao na kufanya mambo mengine,” alisema Mbaruku ambaye kwa sasa anajihusisha na biashara ya asali kutoka Tabora.

Manufaa ya usafiri wa majini hayakuwa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa pekee, bali pia wakazi wa mwambao wa ziwa Tanganyika na Nyasa. Kwa zaidi ya miaka 20, usafiri huu wa majini ulidorora sana katika maziwa hayo makuu kutokana na meli zilizokuwa zikifanya safari hizo kuharibika na kusimama kabisa. Hizi ni meli ambazo zinamilikiwa na serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL).

Katika kipindi hicho, sekta binafsi imejaribu kuanzisha usafiri wa majini lakini imeshindwa kukudhi haja na matarajio ya wananchi. Ni katika muktadha huo, serikali ya awamu ya tano tangu iingie madarakani, imeamua kuifufua MSCL kama ambavyo imefanya kwenye Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL).

Lengo ni kuhakikisha inahuisha shughuli zake, inakarabati na kutengeneza meli mpya na hivyo kuanza kutoa huduma bora za usafiri wa meli katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya MSCL, Eric Hamissi anasema awali MSCL ilikuwa inamiliki meli 14 na boti moja iliyopo ziwa Tanganyika lakini hadi mwaka 2015 meli iliyokuwa ikifanya kazi kati ya hizo ni moja tu. Anasema katika ziwa Victoria, MSCL ilikuwa inamiliki meli tisa, ziwa Tanganyika meli tatu na boti moja na katika ziwa Nyasa kampuni hiyo ilikuwa inamiliki meli mbili.

“Jitihada za kuiokoa MSCL zilianza kwa kufufua baadhi ya meli zetu za awali ambapo hadi sasa meli za kampuni zinazofanya kazi ni nne,” anasema Hamissi.

Anasema serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani iliona umuhimu wa kufanya biashara na nchi zinazotegemea huduma za meli kupitia maziwa hayo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii kama vile Uganda, Kenya, Sudan Kusini, Burundi, Kongo-DRC, Zambia na Malawi.

Anasema kudhoofu kwa usafiri wa meli pia kulisababisha bidhaa nyingi za Uganda kupitia Kenya tofauti na miaka ya nyuma ambapo baadhi zilipita Tanzania hasa kwa kuzingatia kwamba nchi hiyo haipakani na bahari.

Anasema kutokana na dhamira ya Rais John Magufuli kuinua uchumi wa Tanzania, ufufuaji wa MSCL ni moja ya miradi ya kimkakati katika kukuza uchumi wa nchi. Ni katika muktadha huo, Hamissi anasema serikali ilitenga Sh bilioni 152, fedha za ndani ili kuanza kutekelezwa kwa miradi mikubwa minne katika ziwa Victoria, kati ya miradi 11 ya kampuni hiyo. Anasema mikataba ya miradi hiyo minne ilisainiwa tangu Septemba 3 mwaka 2018.

Anasema mradi wa kwanza unaotekelezwa ni wa ujenzi wa meli mpya, kazi inayofanyika katika bandari ya Mwanza Kusini, chini ya mkandarasi, kampuni ya Gas Entec inyaoshirikiana na kampuni ya Kangnam zote za Korea ya Kusini. Anasema kampuni hizo pia zinashirikiana na Suma JKT ya Tanzania katika ujenzi huo.

“Ujenzi wa hii meli mpya utakaochukua miaka miwili unatarajia kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2021 kwa gharama ya Sh bilioni 89,” anasema Hamissi ambaye katika mahojiano na gazeti hili mwaka jana alisema MSCL pia inajipanga kuanzisha usafiri wa meli katika bahari ya Hindi.

Anasema mradi wa pili ni ujenzi wa chelezo kinakachotumika wakati wa ujenzi wa meli hiyo mpya. Anasema chelezo hicho baada ya ujenzi wa meli kitaendelea kutumika kama karakana kwa ajili ya kuifanyia meli hiyo ukarabati na pia kutumika kujengea meli nyingine kukiwa na haja hiyo.

Anafafanua kwamba chelezo hicho kinachojengwa kwa ustadi mkubwa, kitakuwa cha kudumu kitakachotumika kwa miaka mingine ijayo. Anasema ujenzi huo wa chelezo mkataba wake ni mwaka mmoja na unatarajia kukamilika mwezi Machi mwaka huu kwa gharama za Sh bilioni 36. Kinaundwa na kampuni ya STX Engine kwa kushirikiana na kampuni ya Saekyung, zote za Korea Kusini.

Anaitaja miradi mingine inayoendelea kuwa ni ukarabati wa meli ya Mv Victoria kwa gharama ya Sh bilioni 22.8 na ukarabati wa Mv Butiama kwa gharama ya Sh bilioni 4.9.

“Meli hizo zote mbili zinakarabatiwa na kampuni ya KTMI ya Korea Kusini ikishirikiana na Yukos Enterprises Ltd ya Tanzania,” anasema.

Anasema MSCL ndiye msimamizi mkuu wa utekelezaji wa miradi yote hiyo. Hamissi anasema ipo miradi mingine mikubwa ambayo tayari wakandarasi wamepatikana na kinachosubiriwa ni utiaji wa saini wa mikataba hiyo inayohusisha pia ziwa Tanganyika.

Anafafanua kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali kupitia MSCL imeendelea na utaratibu wa manunuzi ili kuwapata wakandarasi watakao tekeleza miradi mingine mitatu ikiwemo miradi ya ujenzi wa meli mbili mpya za mizigo, moja kwa ziwa Tanganyika na nyingine ziwa Victoria.

Meneja Mradi wa MSCL, Abel Gwanafyo anasema ujenzi wa mradi wa chelezo umefikia asilimia 89 wakati ule wa meli mpya umefikia asilimia 52 na asilimia 20.8 kwa upande wa uunganishaji na uchomoleaji wa mitambo.

“Kazi ya ukarabati wa meli ya Mv Butiama imefikia asilimia 81 na Mv Victoria asilimia 84.7,” anasema na kuongeza kuwa kwa miradi ya chelezo na ukarabati wa meli hizo mbili inatarajia kukamilika mwezi Machi mwaka huu.

Anasema MSCL inashirikiana vyema na wataalamu ili kuona kazi inakuwa bora na inakamilikuwa kwa wakati lakini anasema kumekuwa na changamoto ya kukatika katika kwa umeme na mvua zinazoendelea kunyesha.

“Pamoja na changamoto hizo, ninaamini miradi hii itakamilika na kukabidhiwa serikalini kwa muda uliopangwa,” anasema.

WIKI iliyopita tulianza kuangalia kasumba miongoni mwa jamii kudhani kwamba ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi