loader
Dstv Habarileo  Mobile
Alibaba na hofu ya corona kudodesha uchumi wa China

Alibaba na hofu ya corona kudodesha uchumi wa China

KAMPUNI ya Alibaba Holding Ltd ya China imeonya kwamba virusi vya corona ambavyo vimeshaua zaidi ya Wachina 1,300 vimeleta athari kubwa kwa walaji na wafanyabiashara wa nchi hiyo, na kwamba hali hiyo itaumiza vibaya ukuaji wa uchumi wa China katika robo hii ya mwaka.

Alibaba, shirika kubwa la teknolojia nchini China, limekuwa la kwanza kuripoti jinsi lilivyoathirika na hali mbaya ya mwenendo wa uchumi tangu janga hilo la ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo kuripotiwa kwa mara ya kwanza Januari mwaka huu.

Kampuni hiyo imesema virusi hivyo vinadhoofisha kwa kiwango kikubwa uzalishaji katika uchumi kwa sababu wafanyakazi wengi sasa hawawezi kufika kazini. Ugonjwa huo pia umebadilisha mifumo ya ununuzi kutokana na walaji/watumiaji kurudisha nyuma sana katika kununua mahitaji, pamoja na kushindwa kusafiri huku migahawa ikiathirika zaidi.

Kampuni hiyo inayoongoza kwa kuuza bidhaa kupitia mtandao wa kompyuta (e-commerce) nchini China ilitoa maoni hayo ikiwa ni wiki chache baada ya kuripoti matokeo mazuri ya kibiashara robo ya mwisho wa mwaka uliopita iliyoishia Desemba mwaka jana.

Katika kipindi hicho mapato ya kampuni hiyo kubwa yaliongezeka kwa asilimia 38 kuliko ilivyotarajiwa. Lakini Ofisa Mkuu Mtendaji, Daniel Zhang na Ofisa Mkuu wa Fedha, Maggie Wu waliweka wazi juu ya mafanikio hayo kuharibiwa vibaya na ugonjwa huo hatari unaosababishwa na virusi vya corona kutokana na kuathiri mwenendo wa wafanyakazi kufika kazini, wasambazaji na hata wanunuzi.

Wauzaji wengi wanaofanya kazi na kampuni hiyo, tangu Januari hawajaweza kurudi kwenye shughuli zao za kawaida kwa sababu ya uhaba wa wafanyakazi. Hisa zilizoorodheshwa za Marekani za Alibaba zimeanguka kwa asilimia 2.4 Alhamisi iliyopita.

“Janga hilo limeathiri vibaya uchumi wa Uchina kwa ujumla, hususani sekta za mauzo ya rejareja na huduma,” anasema Wu baada ya kuhojiwa kutokana na kuanguka kwa hisa za kampuni hiyo kwenye soko la hisa.

“Wakati mahitaji ya bidhaa na huduma yapo pale pale, njia za uzalishaji katika uchumi zimezuiliwa huku ofisi zikichelewa kufunguliwa, viwanda na shule zikiwa zimefungwa,” anasema.

Anapoulizwa kuhusu namna Alibaba ilivyoathirika, anasita kutoa takwimu za namna kampuni ilivyoathirika akisema bado robo ya mwaka inayoishia Machi haijakamilika wakati watakapofanya tathmini ingawa anasema lazima kampuni itakuwa imeathirika sana.

Zhang anasema wanaona kuna mabadiliko makubwa katika mifumo ya ununuzi. Wakati usambazaji wa chakula unaongezeka, bidhaa kama mavazi na vifaa vya kielektroniki vimekuwa havinunuliki. Anasema biashara ya kupitia mitandao (e-commerce) ambayo ndio biashara kubwa ya Alibaba imeumia kwa kiasi kikubwa sana hususani katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.

“Hali hii italeta changamoto kubwa kwa karibu biashara zote zinazofanywa na Alibaba duniani kote,” anasema katika mahojiano ya simu lakini akasema kwamba pengine pale ugonjwa huu utakapodhibitiwa kuna fursa nyingine zitafunguka.

Kampuni ya Alibaba inashughulikia mipango maalumu wa kuwasaidia wafanyabiashara kwa kupunguza ada ambayo inatoza na kutoa ruzuku kwa wasambazaji. Zhang anasema kampuni hiyo inajaribu kuhakikisha wafanyakazi wake wanakuwa salama dhidi ya virusi vya corona, pamoja na kuwawezesha kufanya kazi wakiwa majumbani mwao.

Zhang, hata hivyo, anasema wafanyakazi wao wengi wameanza kurudi kazini hususani katika majiji ya Beijing, Guangzhou na Shenzhen. Kampuni nyingi za usambaji anasema zimeanza pia kufanya kazi kuanzia siku chache zilizopita.

Kampuni hilo linaloaminika kuwa na thamani ya juu sana nchini China limekuwa likijitahidi kudumisha viwango vya ukuaji wake hata katika kipindi ambacho nchi hiyo inapita katika shida mbalimbali za kiuchumi. Hata hivyo, kutokana na janga la corona, Alibaba limekuwa pia halina uhakika wa kesho yake kama litaendelea kufanya vizuri kwenye soko kama ambavyo limekuwa likifanya au la.

Ingawa hatua ya watu kujifungia nyumbani inaongeza uhitaji zaidi wa huduma za kimtandao kwa ajili ya manunuzi mbalimbali yakiwemo ya vyakula, ugonjwa unazuia pia usafirishaji nchi nzima na hivyo wengi kushindwa kufikiwa na mahitaji.

Kudorora kwa biashara ya Alibaba kutokana na mlipuko wa virusi vya corona “inaweza kuwa mbaya kuliko ilivyokadiriwa awali,” waliandika wachambuzi wa Bloomberg Intelligence, Vey-Sern Ling na Tiffany Tam katika ripoti yao.

“Uuzaji wa bidhaa kupitia Alibaba unaweza kupata shida katika soko lake kuu la rejareja la China na biashara ya huduma za mitaa katika robo mwaka ijayo hata kama milipuko ya virusi vya corona utapungua.”

Wiki hii, kampuni hiyo ilitangaza kupunguza ada ya huduma kwa wafanyabiashara ili kusaidia wale walioathirika kimtaji na janga hili wapate ahueni ya kufanya biashara. Kadri janga la corona linavyozidi kusumbua, kampuni hiyo inaweza kulazimika kupunguza zaidi ada zake na hivyo kuathiri pia mapato yake. Alibaba imekuwa pia ikitoa pia sehemu ya pato lake katika kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona.

Virusi vipya vya corona ambavyo vimeambukiza maelfu ya watu vimesababisha baadhi ya miji ya China kupiga marufuku kabisa usafiri wa sehemu moja hadi nyingine. Mji wa Wuhan uliopo Hubei ambako ndiko chanzo cha mlipuko wa virusi umeendelea kufungiwa kabisa.

Serikali ya China imekuwa ikiongeza juhudi maradufu za kudhibiti virusi hivyo ambapo wanyama wote wa porini wamepigwa marufuku kuuzwa. Virusi hivyo vinaaminika kwamba vimetokana na wanyama na vimesambaa kwa haraka kati ya wanadamu.

Virusi vya corona vinasababisha matatizo ya kupumua. Dalili zake ni pamoja na homa, kikohozi kikavu kisha baada ya wiki moja, mwathirika anakuwa na matatizo ya kupumua na kuhitaji matibabu kwa haraka.

Virusi hivyo vipya vinafananishwa na vile vya sars, ambavyo vilisababisha vifo vya mamia ya watu nchini humo mwaka 2003. Hadi kufikia sasa, bado hakuna tiba maalumu au chanjo dhidi ya virusi hivyo. Chanzo: BBC Magazine

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a054ce9a6ee47b971fccdd633107ffe7.png

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: BBC Magazine

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi