loader
Picha

Waziri aridhishwa wingi viwanda Kibaha

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa ametembelea viwanda na kuridhishwa na Halmashauri ya Mji Kibaha namna inavyotekeleza sera ya uwekezaji wa viwanda kwa vitendo.

Bashungwa aliyeambatana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Riziki Shemdoe kwa pamoja wamempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Jenifa Omolo, kwa kutenga maeneo maalumu ya viwanda huku akiweka utaratibu rafiki kwa wawekezaji wao, na pia kutenga maeneo ya uwekezaji pasipo kuwa na urasimu.

Mkurugenzi wa Kampuni ya BM Motors inayounganisha mabasi makubwa yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 50, Jonas Nyagawa alimsifu Omolo kwa wepesi wa kuwamilikisha maeneo ya uwekezaji mara tu wanapokamilisha taratibu za kiserikali na kwamba hiyo inawapa motisha wawekezaji wote.

“Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara mimi eneo langu lina ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 1,800, lakini tayari nina hati miliki na sibughudhiwi na mwingine kwenye eneo langu,” alisema Nyagawa.

Bashungwa alimpongeza mwekezaji huyu wa Kitanzania kwa uzalendo wake wa kuamua kuwekeza nchini kiwanda hicho kikubwa na chenye tija kwa taifa. Alibainisha faida zitakazopatikana kuwa ni kuilipa kodi serikali, kutoa ajira kwa Watanzania na kuvinufaisha viwanda vingine kwani asilimia 45 ya malighafi zinazotumika kwenye kiwanda hicho zinapatikana nchini.

Awali, Bashungwa aliitembelea kampuni nyingine ya wawekezaji wa Kitanzania ya GF Vehicle Assemblies eneo la TAMCO inayotarajiwa kuweka kiwanda cha kuunganisha magari mchanganyiko yenye uzito usiozidi tani 8 na kwamba uzinduzi wake utafanyika Mei mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Imran Karmali alimweleza Bashungwa kuwa kiwanda hicho zaidi ya kutoa kodi kwa serikali, pia kitatoa ajira nyingi kwa Watanzania na zitaendelea kadri ya uzalishaji unavyoongezeka.

Bashungwa akitoa kauli ya serikali aliwapongeza wawekezaji nchini kwa uamuzi wao wa kuwekeza Tanzania huku akitoa rai kwa mamlaka na taasisi zinazohusika na viwanda likiwemo Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa karibu na wawekezaji kwa ajili ya ushauri wa kitaalamu na kimazingira.

Halmashauri ya Mji Kibaha imetenga eneo mahsusi la viwanda vikubwa lenye ukubwa wa ekari 1,246 eneo la Zegereni umbali wa kilometa 4.5 kutoka barabara kuu iendayo Morogoro kutokea Dar es Salaam.

MKURUGENZI wa Wakala wa Misitu Tanzania, TFS, Santos Salayo ameonya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalum, Kibaha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi