loader
Picha

Serikali yataka ripoti moto uliochoma soko

RAIS John Magufuli ametoa pole kwa wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) waliounguliwa bidhaa zao kwenye tukio la ajali ya moto lilitokea Februari 2, mwaka huu kwenye Soko la Makoroboi jijini hapa.

Pole hizo za Rais Magufuli zimetolewa leo jijini Mwanza kwa niaba yake na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwita Waitara aliyetembelea soko hilo na kuzungumza na wamachinga.

“Mheshimiwa Rais anawasalimia na anawapa pole nyingi kwa tukio hilo lililowakuta, anasema yuko pamoja na ninyi,” alisema Waitara.

Pamoja na kuwasilisha pole hizo za Rais, Waitara aliutaka uongozi wa Wilaya ya Nyamagana kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza kuhakikisha kuwa taarifa ya mkoa ya jeshi hilo inatolewa ndani ya wiki hii ili kubaini chanzo cha soko hilo kuchomwa moto na wahusike wachukuliwe hatua.

Kwa upande wa maeneo wanayofanyia biashara wamachinga, ametoa maelekezo kwa viongozi wa halmashauri zote, wilaya, mikoa majiji na manispaa wanapokuwa wanawahamisha wamachinga wahakikishe kuwa wanawapeleka kwenye maeneo yaliyoandaliwa vyema na yenye miundombinu iliyokamilika.

Alitoa maelekezo hayo baada ya Mwenyekiti wa Shirika la Wamachinga (Shiuma) Kata ya Pamba, Fredy Charles kueleza kuwa waliokuwa wafanyabiashara wa Kata ya Pamba waliondolewa kinyemela katika eneo hilo, hoja iliyopingwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk Philis Nyimbi kwamba wafanyabiashara hao wametengewa eneo la kufanyia biashara katika Kata ya Mbugani, ambalo lina miundombinu tayari lakini wamegoma kwenda.

Katika hatua nyingine, Waitara aliutaka uongozi wa Wilaya ya Nyamagana na Halmashauri ya jiji la Mwanza kukaa na viongozi wa makundi mawili ya wamachinga, likiwemo kundi linalowakilishwa na Shiuma na lile linalowakilishwa na Muungano ili kujua uhalali wa makundi hayo kisheria katika utekelezaji wa shughuli zao na changamoto yanayokabiliana nazo, badala ya kila kundi kujitambulisha kivyake kuwa linawaongoza wamachinga, akisisitiza kuwa serikali haiwezi kusajili vyama viwili vyenye majukumu yanayofanana.

Kwa wale waliounguliwa na bidhaa, aliwataka wajiunge kwenye vikundi ili wakopeshwe mikopo isiyo na riba ili waendelee na biashara zao.

Akisoma risala yao, Makamu Mwenyekiti wa SHIUMA Mkoa wa Mwanza, Joseph Samwel alisema kipo kikundi cha watu kinachowasumbua kwa kuwaomba rushwa kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema hatua hiyo inakatisha juhudi zao za kufanya biashara kwa uhuru na kuomba serikali kuingilia kati. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SHIUMA Taifa, Ernest Masanja aliomba serikali ichukue jukumu la haraka la kuwasaidia wamachinga hao mikopo kwa madai kuwa wengi wameunguliwa bidhaa zao na hawana pa kushika.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk Philis Nyimbi alisema uongozi wake unafanya kazi ili kuhakikisha kuwa wamachinga wanaotii sheria hawaonewi na mtu yeyote, isipokuwa alisema wapo baadhi ya wamachinga ambao wametengewa maeneo ya kwenda kufanyia biashara na yako karibu na mji lakini wanakaidi maelekezo ya serikali.

Katika hatua nyingine, moto huo katika soko la wafanyabiashara wa nguo na bidhaa nyingine la Makoroboi umesababisha hasara ya Sh 246,179,000, ambao wamachinga 159 mali zao ziliteketezwa na vibanda 65 viliteketea.

Dk Nyimbi alizishukuru taasisi za majeshi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), viongozi na wananchi ambao waliwahi kwenye tukio na kufanikiwa kuuzima mto huo ambao ungesababisha madhara makubwa.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy, Mwanza

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi