loader
Picha

Viuadudu kutumika kutibu malaria

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limetamka kuwa dawa ya viuadudu kutumika katika harakati za kupambana na ugonjwa wa malaria katika nchi mbalimbali duniani.

WHO iliyasema hayo katika kongamano lililofanyika mwishoni mwa wiki jijini Geneva nchini Uswisi, na kueleza ni badala ya kutumia dawa zenye kemikali ambazo zimeonesha kushindwa kuondoa tatizo hilo la malaria na kuwa na athari kubwa kiikolojia, kiafya pamoja na kimazingira.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na WHO, matumizi ya dawa zenye kemikali katika kupambana na malaria zimeonesha kushindwa kufanya kazi sawa sawa huku ikibaininisha baadhi ya dosari za kutumia dawa hizo katika vita vya kupambana na malaria.

Miongoni mwa dosari hizo ni kuwa zinachangia kuharibu ikolojia ya wanyama na mimea kwa kuwa kemikali haifi pamoja na baadhi ya mbu kujenga usugu wa dawa hizo na hivyo kushindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa.

Akizungumza na gazeti hili, Meneja Udhibiti Ubora wa Kiwanda cha Viuadudu cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) kinachomilikiwa na Serikali chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Samwel Mziray alisema mbu jike ndiye anayeeneza malaria kitaalamu huitwa Anofelesi.

Mziray ambaye alikuwa mwakilishi wa Tanzania katika kongamano hilo la WHO, aliongeza kwamba mbu huyo ana uwezo wa kutaga mayai 200 kila baada ya siku tatu na muda wake wa kuishi ni siku 21 na hivyo ana uwezo wa kutaga mara saba na kufikisha idadi ya mayai 1,400.

Mziray alisema katika kongamano hilo, Tanzania ilitajwa kuwa nchi ya saba duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha ugonjwa huo wa malaria. Kufuatia hali hiyo, Mziray aliwataka wananchi kubadili mtazamo na kuanza kutumia viuadudu katika kukabiliana na suala la Malaria kwa kuwa ni njia ambayo ina ufanisi mkubwa ikilinganisha na matumizi ya kemikali.

Alisema kwa mujibu wa ripoti ya WHO, ubora wa matumizi ya dawa za viuadudu unatokana na namna ulivyokuwa rafiki kwa mazingira pamoja na kiafya kwa kuwa matumizi yake huharibu kabisa mazalia ya mbu na kuwafanya mbu kushindwa kuzaliana na hakuna ripoti zozote zinazoonesha kuwa matumizi ya viuadudu yameonyesha usugu tofauti na ilivyo katika kemikali.

Mziray pia alibainisha kuwa licha ya tatizo kuwa kubwa tayari NDC imejipanga katika kuhakikisha dawa za viuadudu zinawafikia wananchi popote walipo katika kuhakikisha wanazitumia kwaa kuondoa kabisa tatizo la ugonjwa malaria nchini. Tanzania ni nchi pekee Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa na teknolojia ya kiwanda cha kutengeneza viuadudu ambacho kimejengwa wilayani Kibaha mkoani Pwani ambacho kinamilikiwa na serikali kwa asilimia 100 na husimamiwa na kuendeshwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).

“Ni neema kubwa kwa nchi katika wakati huu ambapo WHO inaona kuwa njia pekee ya kupambana na malaria ni kupitia matumizi ya dawa za viuadudu,” alisema Mziray.

Alisema Tanzania iliipata teknolojia hiyo kutoka nchini Cuba ambao wao walianza kutumia siku nyingi na imewasaidia kuondosha suala la malaria nchini humo, ambako awali ugonjwa wa malaria ulikuwa ni miongoni mwa magonjwa yaliyokuwa tishio nchini Cuba.

NTAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) mkoa ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi