loader
Picha

Magufuli awakosha madaktari

RAIS John Magufuli ametangaza kutoa ajira 1,000 kwa madaktari nchini, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha maboresho ya sekta ya afya, ikiwemo ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, yanaendelezwa kwa kupatiwa wataalamu wa afya wa kutosha.

Pia, amebainisha kuwa kutokana na kasi ya uboreshaji wa sekta ya afya nchini, tayari hayo ni maandalizi ya kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazotoa utalii wa afya Afrika, ambao pia utaingizia nchi mapato.

Rais alieleza hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na madaktari pamoja na watumishi wa sekta ya afya katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Madaktari nchini na kusherehekea miaka 55 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).

“Nafahamu kuna madaktari takribani 2,700 bado hawajaajiriwa.

Hili nitalifanyia kazi. Nafikiri tunaweza tukaanza na kuajiri hata kidogokidogo, eti Waziri wa Utumishi (George Mkuchika) tunaweza kuajiri hata 1,000, hela si zipozipo kidogo basi tunaajiri madaktari 1,000,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wanaanza kutoa ajira hizo 1,000 na endapo hapo baadaye mambo yatakuwa mazuri, wengine pia wataajiriwa ili kutimiza vyema mzunguko wa ajira kwa wataalamu hao.

Alisema kupitia serikali yake hiyo kuanzia Desemba mwaka 2015 hadi Januari 2020, imetoa ajira kwa watumishi wapya wa sekta mbalimbali 62,498, ambao mishahara yao katika kipindi hicho ni Sh trilioni 4.169.

Alieleza kuwa watumishi hao wapya, wamefanya kuwa na jumla ya watumishi wa serikali 526,146, ambao kwa mwezi wanalipwa kiasi cha Sh bilioni 577.

“Hapa hatujawajumuisha watumishi ambao ni askari wala hatujajumuisha fedha zinazotumika kwenye madeni tuliyokopa tangu tupate Uhuru, fedha zinazolipia miradi ya maendeleo reli, barabara, hospitali na vituo vya afya. Kila mwezi shilingi bilioni 577 ni za mishahara ambayo ni sawa na shilingi trilioni saba kwa mwaka,” alieleza.

Alisema kupitia ajira hizo mpya katika sekta ya afya, wapo watumishi wapya 13,479. Idadi hiyo ni kubwa kuwahi kuajiriwa katika kipindi cha miaka minne nchini. Watumishi hao hulipwa kiasi cha Sh bilioni 109.947.

Alisema kada za watumishi hao wapya walioajiriwa ni madaktari bingwa 22, madaktari 1,984, madaktari wa meno 63, madaktari wasaidizi wanane, daktari mmoja wa meno msaidizi, tabibu 1,295, tabibu wa meno 63, tabibu wasaidizi 1,130, maofisa wauguzi 475, wauguzi wasaidizi 127, wauguzi 2,469, wauguzi wasaidizi 1,119, wahandisi vifaa tiba saba na mafundi sanifu vifaa tiba 53.

Wengine ni wakemia sita, makatibu afya 100, ofisa afya mazingira 111, wasaidizi wa afya mazingira 1,115, wateknolojia katika fani mbalimbali 1,196, wateknolojia wasaidizi katika fani mbalimbali 656, wataalamu wa mionzi 55, wa mazoezi ya viungo 76, na wafamasia 205.

Watumishi wengine ni watalaamu wa macho watano, watalaamu wa mifupa watano, watalaamu wa viungo bandia 16, watalaamu wa maabara 192, ofisa ustawi wa jamii 63, wasaidizi wa kumbukumbu za afya 166 na madobi wa vitu vya afya watatu.

Alifafanua kuwa baada ya ajira hizo mpya 13, 479, sasa Tanzania ina jumla ya watumishi wa afya 98,987, ambao wanalipwa mishahara ya jumla ya Sh bilioni 830.

“Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo watumishi wa afya walioajiriwa na sekta binafsi hivi sasa ni 18,094,” alisisitiza.

Alisema kwa kutambua hilo pamoja na kwamba fedha bado ni tatizo, serikali itajibana ili iajiri madaktari hao 1,000, ambao watasambazwa nchi nzima ili kufikia malengo ya serikali. Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka hiyo minne, Serikali ya Awamu ya Tano imeboresha sekta ya afya, ambapo mwaka 2015 kulikuwa na zahanati 6,044, lakini mwanzoni mwa mwaka huu, kulikuwa na zahanati 6,467.

Vituo vya afya vilikuwa 718 mwaka 2015 wakati mwaka huu vimefikia 1,169.

“Kati ya vituo hivi vya afya kulikuwa na vituo 15 tu vyenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji, lakini sasa vimefikia vituo 400 vinavyotoa huduma hiyo,” alifafanua.

Aidha, alisema mwaka 2015 kulikuwa na hospitali za wilaya 186, lakini hadi mwaka huu zimeongezeka na kufikia 321 ambazo zimejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 293.7. Hospitali za rufaa mpaka sasa 23 zimekarabatiwa kwa gharama ya Sh bilioni 89.5.

“Lakini pia tumeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 hadi shilingi 270 mwaka huu. Pia tumeboresha zaidi huduma za matibabu ya magonjwa makubwa kama vile figo, moyo, ubongo, mifupa na saratani,” alisema.

Alisema ndio maana kwa hali ilivyo, nchi imeanza kupokea wagonjwa kutoka nchi za jirani.

“Huu ni mwanzo mzuri wa kujiendeleza zaidi ili kuanzisha medical tourism. Nchi za wenzetu zinaingiza dola za Marekani milioni 14 hadi 16 kwa mwaka kupitia utalii huu wa afya ikiwemo India. Na sisi tunaweza kufika huko,”

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi