loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Daktari aliyewahi kumtibu JPM atoa ya moyoni

DAKTARI aliyetajwa na Rais John Magufuli, kumtibu akiwa naibu waziri alipougua hadi kulazwa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, amesema yeye anaamini kuwa sekta ya afya, inashirikisha wanataaluma wengi na wengi wamegusa mamia ya Watanzania hata zaidi yake.

Dk Zainabu Chaula (pichani), ambaye alitajwa na Rais Magufuli juzi alipozungumza na madaktari katika maadhimisho ya miaka 55 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kuwa alichangia kutetea uhai wake kwa huduma aliyompa kama daktari alipolazwa ICU katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, alisema safari yake ya kitaaluma haipaswi kueleza aliyofanya kwani ni wajibu wake.

Gazeti hili jana likizungumza kwa simu na Dk Zainabu, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya binadamu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

“Unajua daktari anahudumia watu wengi na kwa wakati na majira tofauti tofauti. Huduma yetu ni kwa ajili ya watu, sasa Rais anapenda kuthamini taaluma za watu ndio maana alijisikia kusema yeye mwenyewe alichosema jana (juzi) kama moyo wa shukrani,” alisema Dk Zainabu

Alisema moja ya maadili ya udaktari ni uadilifu, unaowazuia wasitangaze wema au tiba yoyote wanaoifanya kwa mgonjwa, bali kubaki nayo moyoni, kama sehemu ya huduma.

Alisisitiza kuwa mgonjwa anapotibiwa na kupona, hazuiwi kueleza furaha yake. Dk Zainabu alimshukuru Rais Magufuli, kwa kuendelea kuwaamini madaktari nchini na Watanzania wengine wenye taaluma mbalimbali, kwa kuwapa fursa kudhihirisha kwa vitendo taaluma zao na kugusa maisha ya Watanzania, akiwamo ya kwake mwenyewe Rais bila hata kutarajia. Alisema Rais Magufuli amekuwa na upendo mkubwa na utu kwa wataalamu na sekta nzima ya afya.

“Naamini anapendezwa na kazi zetu na wachache kati ya wengi tunaonekana tukibeba taaluma kwa ajili ya wote. Kazi yetu ni ya lawama nyingi, kubwa kwa kuwa mgonjwa ana matarajio yake ya kupona anapokutana na daktari na si vinginevyo”.

“Mimi nilikuwa natekeleza majukumu yangu kwa mujibu wa taaluma. Na ukumbuke nimekuwa daktari wa Bunge kwa kuwa Hospitali niliyofanya kazi kwa muda mrefu ni ya Mkoa Dodoma. Nimehudumia wabunge na mawaziri wengi na sehemu ya familia ya wanasiasa wengi,” alifafanua Dk Zainabu.

Alipoulizwa alimtibu lini Rais alipokuwa naibu waziri, Dk Zainabu alisema; “Siwezi kusema ilikuwa lini maana sisi kitaaluma tunatibu, nahudumia watu wengi sana, huo ndio wito wetu,” alisema Dk Zainabu.

Rais alimtaja Dk Zainabu Akizungumza na madaktari juzi, Rais Magufuli alisema, “Mimi nina historia nzuri na madaktari, kwa sababu nimehudhuria na kushughulikiwa na madaktari, nakumbuka siku moja nikiwa naibu waziri nafikiri, nilienda kutolewa jino Muhimbili (Hospitali ya Taifa), niliamka baada ya siku mbili nikiwa ICU...kwa hiyo ninafahamu wasingekuwa madaktari nisingepona.

“Lakini nakumbuka pia niliwahi kuwa ICU Dodoma, nilipoamka nikakuta na hudumiwa na Dokta Zainabu, kwa hiyo Dokta Zainabu ananijua kila kitu ingawaje mimi simjui kila kitu,” alisema Rais Magufuli na kusababisha kicheko kwa hadhara yote.

Historia ya Dk Zainabu Kabla hajateuliwa na Rais Magufuli mapema mwaka jana kuwa Katibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Zainabu alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) akishughulika na Afya. Dk Zainabu, Chaula akiwa mume wake, alisoma Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Mwaka 1993 alifanya kazi Hospitali ya Taifa Muhimbili na mwaka 1994 alihamishiwa Hospitali ya Mkoa Dodoma kama daktari wa kawaida. Mwaka 2003 hadi 2008 aliongeza elimu na kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya binadamu na mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Ndani, Hospitali ya Mkoa Dodoma.

Aliteuliwa kuwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Dodoma mwaka 2015 hadi Septemba 2016, alipoteuliwa na Rais kuwa Naibu Katibu Mkuu (Afya) Tamisemi, anakoeleza alishiriki kufanya maboresho ya vituo vya afya kote nchini chini ya Waziri Selemani Jafo.

UZALISHAJI wa chakula umeimarika na hivyo kuwezesha nchi kujitosheleza kwa ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi