loader
Picha

Magufulification of Africa’; Macho yao yanaona kama sisi?

“ MACHO yako yanaona kama mimi... Wanaoteseka wako wapi?”

Hayo yalikuwa maneno ya mtangazaji mmoja wa televisheni wakati timu ya Simba ilipofunga goli muhimu sana dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia. Lilikuwa goli la tatu muhimu kwa Simba kwani ndilo liliihakikishia timu hiyo kuitupa nje Nkana na kuingia hatua ya makundi mwaka juzi.

Maneno hayo yanaweza kusadifu ukweli huu kwamba kuna mambo makubwa anayofanya Rais John Magufuli ambayo yamewashinda viongozi wengi wa Afrika mintarafu kulinda rasilimali za nchi na kutotumia madaraka kujitajirisha, lakini wanatokea watu wanaobeza kama vile hakuna la maana analofanya.

Mtu unakaa unajiuliza hivi hawa macho yao hayaoni kama sisi wengine tunavyoona? Unajiuliza pia kwa nini wanateseka, ni kwa sababu ya kutaka madaraka au nini? Unafikia kujiuliza hivyo kwa sababu wao ni kupinga kila kitu hata yale ambayo kabla Magufuli hajaingia madarakani walikuwa wakiyapigia makelele yafanyike! Lakini wanaoona kama sisi hawako Tanzania pekee, bali hata nje ya Afrika.

Mwaka 2017, nilibahatika kuwa miongoni mwa waandishi wa habari waandamizi 35 kutoka nchi 10 za Afrika waliokuwa wakishiriki semina ya wiki mbili nchini China katika Jiji la Beijing.

Baada ya kujitambulisha kwamba ninatoka Tanzania, mwandishi mmoja kutoka Sudan Kusini, Tekajwok Obongo, alinifuata na kusema maneno haya ambayo niliwahi kuyaandika katika kona hii. “Imani ambayo wengi tumekuwa nayo ni kwamba ni vigumu kupata kiongozi wa Kiafrika ambaye hatatumia madaraka yake kujitajirisha binafsi na genge lake la watu wachache.”

“Lakini Tanzania mmepata bahati sana kwa kumchagua (John) Magufuli. Amekuwa rais tofauti kabisa. Nikisoma habari zake, nafurahi sana.”

Akaongeza: “Unajua, kiongozi anaweza akawa na sera nzuri sana mdomoni, lakini akishaingia madarakani anabadilika. Anawasahau wananchi wenzake, anaanza kupora rasilimali za nchi au kushindwa kuzisimamia.”

Takribani washiriki wote nilioongea nao, kila wakisikia ninatoka Tanzania, walitaka kujua mengi kuhusu Rais Magufuli na hata wengine wakatamani kuzuru Tanzania, si kwa ajili ya kutalii katika vivutio vya utalii kama Mlima Kilimanjaro au kwenye mbuga za wanyama, bali kuiona ‘Tanzania ya Magufuli.’

Hata kwenye michango na maswali yao wakati wa semina hiyo ya wiki mbili, washiriki walionesha kwamba Afrika imekuwa ikisalitiwa na viongozi wake na hivyo kushindwa kutumia rasilimali zake katika kujiletea maendeleo. Waandishi hao wakawa wanatamani hata nguvu kutoka nje ziwe zikitumika katika kusaidia kuwadhibiti viongozi wanaopora au kushindwa kusimamia rasilimali za nchi zao.

Kwa mfano, wakati akiwasilisha mada iliyohusu Mahusiano ya Maendeleo baina ya China na Afrika, Balozi Ren Xiaoping aliulizwa swali na mmoja wa wanasemina kwamba ni kwa nini China haiweki masharti yanayohusu utawala bora wakati inapotoa misaada kwa nchi za Afrika ambazo nyingi zina tatizo hilo, mintarafu suala zima la ufisadi.

Akijibu swali hilo, Ren ambaye aliwahi kuwa Balozi wa China nchini Namibia alisema sera za China ndizo zinaelekeza taifa hilo kutoingilia kabisa masuala ya ndani ya nchi nyingine. Hapo kwa majirani zetu wa Kenya, kuna mwanasheria, mhadhiri, mchambuzi wa mambo ya siasa na mwanamajumui wa Afrika, Profesa Patrick Lumumba (pichani), amekuwa akikiri kwamba Rais Magufuli ni kiongozi wa kuigwa Afrika.

Siku chache baada ya kuingia madarakani mwaka 2015, Profesa huyo ambaye bila shaka anaijua historia yake tangu akiwa waziri, alimtabiria makubwa Magufuli. Katika mjadala mmoja unaopatikana katika (www.youtube.com/ watch?v=9VunShPDovY) Lumumba, anakaririwa akisema kuwa Magufuli ni “real deal”, akimaanisha aliyoyafanya baada ya kuingia madarakani hayakuwa maigizo wala ‘nguvu za soda,’ bali ndivyo alivyo.

Katika klipu hiyo, Lumumba anasema: “Ninaweza kukuhakikishia kwamba taswira na mtazamo wa Mwalimu Nyerere sasa unajitokeza dhahiri kwa Rais Magufuli.”

Anaendelea: “Na wale wanaodhani kwamba, haya anayoyafanya ni nguvu ya soda wakidhani yanayotokana na msukumo wa uchaguzi, watakuja kushangaa sana. Huyu ni mtu ambaye ndani ya miaka 10 ataonesha njia kuhusu uongozi bora na uliotukuka katika eneo hili la Afrika Mashariki.”

Siku chache baadaye, Profesa Lumumba, ambaye aliwahi kuongoza Kamati ya Maadili na Kupambana na Rushwa ya Kenya, (EACC), alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi wake wakati akihojiwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC).

Akasema Magufuli hatua ya Rais Magufuli kupambana na ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma ni jambo ambalo wananchi wengi wa kawaida wanatazamia kuliona kwa rais wao na kwamba hilo litaisaidia sana Tanzania kupiga hatua kimaendeleo. Alirudia kusema katika mahojiano hayo na BBC kwamba, hatua anazochukua Rais Magufuli siyo za kujionesha bali anafuata nyayo za marais waliofanya kazi ya kutukuka barani Afrika.

“Rais Magufuli ameonesha Unyerere na Unkrumah na nina hakika kwamba atawadhihirishia watu kuwa yeye ni mtu mwenye azma njema na Tanzania itakuwa nchi ya kupigiwa mfano katika siku za usoni,” akasema.

Wakati fulani, Profesa Lumumba alikuwa katika mkutano katika nchi inayoonekana kuwa ni Ghana ambapo, video fupi inayopatikana katika Michuzi Blog, inamwonesha akisema: “Miongoni mwenu wapo ambao wanatarajia kuwania uongozi wa kisiasa, lakini swali la msingi la kujiuliza ni hili: “Kwa nini unataka kuongoza?”

Anaendelea: “Katika Afrika, njia nyepesi ya kupata utajiri wa harakaharaka ambao huwezi kuutolea maelezo namna ulivyopatikana ni kuingia katika uongozi wa kisiasa... “Huo ndio ukweli, nenda kila mahala Afrika isipokuwa kwa watu wachache sana. Mtu pekee anayeonekana kwa sasa mintarafu suala zima hilo (la kutumikia wananchi na siyo kutafuta utajiri) ni Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.”

Mwaka 2017 alipokuja Tanzania na kuzungumzia umuhimu wa usafi katika siasa safi za Afrika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kuna umuhimu wa ‘kumagufulify’ siasa za Afrika akimaanisha Afrika kumwiga. Juzi Jumatatu, mwanamajumui huyo wa Afrika alikutana na Rais Magufuli Ikulu Dar es Salaam, ikiwa ni mara yao ya kwanza kukutana na kumwelezea kwamba ni mfano wa kiongozi wa kuigwa kutokana na uongozi wake wa kupigania raslimali za nchi ikiwemo madini, kujenga nidhamu ya utumishi na kuimarisha uchumi. Juzi, Lumumba alisema Rais Magufuli ameweza kupambana vyema na wizi wa mali za umma, rushwa na ufisadi.

Mkenya huyo akasisitiza kuwa nchi zote za Afrika hazina budi kujifunza yanayofanyika Tanzania kwa sasa na kwamba, ni muhimu kwa Waafrika kujiamini na kuchukua hatua madhubuti za kuwaondoa katika hali ya sasa ambapo rasilimali zake zinachukuliwa na mataifa ya nje ilhali wananchi wake wakikabiliwa na changamoto mbalimbali.

Rais Magufuli alimpongeza Profesa Lumumba kwa juhudi zake za kueleza wazi makosa ambayo yamekuwa yakisababisha nchi za Afrika kuendelea kubaki nyuma kiuchumi, kijamii na kisiasa na wajibu wa viongozi pamoja na wananchi wa Afrika katika kukabiliana changamoto zinazozikabili nchi zao.

“Mimi sijawahi kukutana nawe kabla, lakini nakusikia na kukuona kupitia vyombo vya habari jinsi unavyopaza sauti kuhusu Bara la Afrika, nakupongeza kwa juhudi hizo, na ninafarijika kwamba unaisema vizuri Afrika,” alisema Rais Magufuli.

Wakati wengi wakiona Magufuli anapaswa kuigwa na viongozi wa Afrika, kuna Watanzania wenzetu wamekuwa hawaoni anachokifanya na wamekuwa akiteseka sana. Sisemi kwamba yeye ni malaika na kila kitu anachofanya kiko sahihi kwa asilimia 100, bali mengi anayofanya huwa nia njema nyuma yake na hata ukosoaji kama upo ulipaswa kufanya kwa njia ya kujenga na siyo kubeza.

Pale alipoanza kusimamia rasilimali za madini ambazo kwa miaka mingi tumekuwa ‘tukipigwa’ kwa kuzuia makontena ya makinikia pale bandarini, kuna waliotokea kupinga au kubeza hatua hiyo. Walifikia kuwahimiza Wazungu watushitaki na kutufilisi kwa madai ya kuvunja mikataba! Wakati hatua hiyo ikijenga misingi ya kuhakikisha tunanufaika na madini kuna akina Zitto Kabwe waliosema kwamba ni uamuzi wa kiholela na eti imefanya tupoteze Sh trilioni 1.8 ambayo ingetokana na Capital Gains Tax.

Tuliona pia ndege yetu ya Bombardier Q 400 ilipozuiliwa Canada, hawa jamaa walijifanya kulia machozi ya mamba huku wakifurahia jambo hilo. Hali kama hiyo pia ilitokea wakati ndege yetu nyingine ilipozuiliwa Afrika Kusini. Kutokana na hilo, Mtanzania mmoja anayeishi na kufanya kazi nchini Marekani, Idd Ligongo aliandika haya kwenye akaunti yake ya Facebook: “Tofauti ya Mmarekani na sisi (Watanzania/Waafrika), hata kama wewe ni mpinzani wa mtawala, kamwe hatofurahia ama kuomba mabaya yatokee kwa nchi yako.”

“Kamwe hatopiga vigelegele jambo baya linapotokea kwa nchi bila kujali kama unamkubali mtawala au humkubali.” Linapokuja suala la maslahi ya nchi wote wanakuwa kitu kimoja.”

Mifano ya kubeza juhudi za Magufuli za kulinda rasilimali na kuwaletea Watanzania maendeleo iko mingi hata alipotangaza mradi wa kuzalisha umeme wa maji Mto Rufiji kuna waliopiga kelele sana kupinga uamuzi huo na kuubeza. Hivi hawa wanaona kama sisi au ni kama Vijana Jazz walivyoimba kwenye moja ya kibao chao cha Mama Chichi wakisema: “Kasoro ya binaadamu, tangu na enzi, ni kutopenda maendeleo ya mwingine…” Inshallah kuna siku watayaona mambo kama sisi.

WAKULIMA wa Kijiji cha Manda Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi