loader
Picha

Wachina waliomhonga bosi TRA yawakuta

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu raia wawili wa China, Zheng Rongnan na Ou Ya kulipa faini ya Sh milioni moja kila mmoja na imetaifi sha Dola za Marekani 5,000 (Sh milioni 11.5) walizotoa rushwa kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Edwin Mhede.

Pia, mahakama hiyo imeagiza washtakiwa hao, wakazi wa Kinyanambo Mafinga mkoani Iringa, waende kufanya makubaliano kuhusu kulipa kodi ya Sh bilioni 1.3 wanayodaiwa na TRA. Kabla ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ipyana Mwakatobe aliwasomea mashtaka washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaid.

Mwakatobe alidai kuwa Februari 24, mwaka huu washitakiwa wote wakiwa katika Makao Makuu ya TRA yaliyopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, walitoa rushwa ya Dola za Marekani 5,000 sawa na Sh milioni 11.5 kwa Kamishna Mkuu, Dk Mhede kama kishwawishi ili asaidie kampuni yao kutolipa kodi ya Sh bilioni 1.3, kiasi ambacho kilipaswa kulipwa kwa mamlaka hiyo.

Katika maelezo ya awali, Mwakatobe alidai mshitakiwa Rongnan ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ronglan International Industry Ltd, ambayo Februari 21, 2020 ilikaguliwa na TRA na kubainika kuwa wanatakiwa kulipa kodi ya Sh bilioni 1.3, iliyotakiwa ilipwe kwa mamlaka; au iwekewe pingamizi, kama hawajaridhika na makadirio ya TRA.

Alidai kuwa Februari 24, 2020, washtakiwa wote kwa pamoja walikwenda kukutana na Kamishna Mhede, kwa lengo la kumueleza kuwa kampuni yao ilikadiriwa kiwango kikubwa cha kodi.

Alidai siku hiyo hiyo washtakiwa walikutana na Kamishna Mhede ofisini kwake, akiwa na msaidizi wake, ambapo walimuelezea shida yao na kuwasilisha nyaraka kadhaa, huku wakiomba wasaidiwe kutatuliwa mgogoro wao.

Baada ya kuwasilisha maombi yao kwa kamishna, walichukua bulungutu la dola za Marekani na kumpatia, kama kishawishi cha kuwasaidia kwenye suala la kodi, ambayo kampuni yao ilipaswa kulipa kwa TRA. Mwakatobe alidai Kamishna Mhede, alimwelekeza msaidizi wake ahesabu fedha hizo na kubaini zilikuwa dola za Marekani 5,000.

Alimalizia kwa kudai kuwa Kamishna Mhede, alitoa taarifa kwa Takukuru na watuhumiwa wote walikamatwa ofisini hapo pamoja na vidhibiti walivyokutwa navyo, am- bavyo ni fedha na nyaraka walizowasilisha kwa kamishna.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahid aliwaeleza washtakiwa hao, Zheng Rongnan na Ou Ya ambao ni mke na mume na wamiliki wa Kampuni ya Ronglan International Industry Ltd, kuwa Tanzania ni nchi yenye sheria na taratibu, ambazo zinapaswa kufuatwa na watu wote wakiwemo wawekezaji kama wao, hivyo kukiuka sheria na taratibu za nchi, kumewachefua.

Alisema washitakiwa wote, wanatakiwa kulipa faini ya Sh milioni moja kila mmoja. Aliwaagiza waende TRA ili wakazungumze na kamishna na kuona namna watakavyomaliza mgogoro wa kodi, uliopo baina ya mamlaka na kampuni yao. Watuhumiwa hao walipandishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Februari 25 mwaka huu.

MTANGAZAJI maarufu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Marin Hassan ...

foto
Mwandishi: Ana Mwikola

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi