loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Majaliwa- Waambieni Serikali imefanya nini

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa idara, kwenda kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Pia, ametoa wito kwa wakuu wa idara, kufanya kazi kwa ushirikiano na watumishi wengine wa idara ili kuhakikisha katika kipindi hiki kilichobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu, kutekeleza sehemu iliyobaki ili Rais John Magufuli atakapokwenda kuwaeleza wananchi maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Tano taarifa ziwe sahihi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano, inafanya kazi kutokana na mwongozo wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na siyo kwa akili za watu, hivyo wakuu wa wilaya wahakikishe wanasimamia utekelezaji huo.

“Kipindi kilichobaki ni fursa kuwaambia wananchi nini Serikali ya Awamu ya Tano imefanya. Wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wakuu wa idara nendeni kwa wananchi mkasikilize matatizo yao, msiwadharau kutokana wao ndio waliofanya mpangiwe vituo vya kazi,” alisema Majaliwa.

Aliongeza; “kuna taarifa baadhi ya wakuu wa idara mnapopata maelekezo kutoka serikalini, hamyafikishi kwa watumishi wengine, wewe kama mkuu wa idara inapotokea nafasi ya kuhudhuria vikao toa nafasi kwa wengine, siyo kila safari uende wewe.”

Kuhusu makusanyo ya mapato ya halmashauri, alisema halmashauri nyingi zinapanga bajeti, lakini hazifikii lengo kutokana fedha nyingi zinaishia kwenye mifuko ya watu, hivyo kushindwa hata kutekeleza miradi ya maendeleo.

Aliwataka madiwani, wakurugenzi na wakuu wa idara, kusimamia hilo.

“Kwenye halmashauri, fedha nyingi za mapato ya ndani zinaishia kwenye mifuko ya watu badala ya kuingia kwenye bajeti ya halmashauri, ndio maana zinashindwa kufikia maendeleo,” alisema.

Alishangazwa na halmashauri za Mkoa wa Tanga, kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ikiwa ni robo ya tatu, ambapo Halmashauri ya Bumbuli imeongoza kwa kufikisha asilimia 59, Tanga Jiji asilimia 51 wakati Halmashauri ya Pangani imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 17, Muheza 25 na Mkinga asilimia 23.

Kuhusu watumishi wa umma, aliwatahadharisha kujiepusha na tabia za wizi wa mali za umma, badala yake wawe waadilifu na uaminifu.

Kuhusu huduma za jamii, alisema Mkoa wa Tanga, serikali imeleta fedha nyingi kwenye sekta ya afya na elimu ambapo kwa elimu ya msingi imeleta fedha za ruzuku Sh bilioni 6.9 na sekondari Sh bilioni 6.5.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella alisema serikali imejenga hospitali za wilaya tatu na vituo vya afya 22. Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbaruku (CUF) alisema Serikali ya Awamu ya Tano, imefanya mambo makubwa katika Jiji la Tanga kwenye elimu, maji, afya na miundombinu.

“Tuongee ukweli Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa, tuweke tofauti ya vyama pembeni, tukisimama kwa kwenye maendeleo serikali imefanya maendeleo Jiji la Tanga,” alisema Shigella.

KATIBU Tawala wa Wilaya ...

foto
Mwandishi: Cheji Bakari, Tanga

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi