loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Abbasi: Serikali haijawahi kukosa fedha za SGR

SERIKALI imesema haijawahi kukosa fedha wala kutatizwa kwa namna yoyote juu ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) tofauti na uzushi wa wanasiasa, sasa ujenzi huo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro utekelezaji wake umefi kia asilimia 75 na treni itaanza kufanya kazi mwaka huu.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi alisema hayo jana jijini hapa huku akiwashangaa wanaobeza ujenzi wa SGR na kubainisha kuwa mpaka sasa ujenzi wa reli hiyo Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 75 huku ule wa Morogoro kwenda Makutupora Singida ukifikia asilimia 28.

Dk Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, alikuwa akizungumza wakati wa mkutano wake wa kila mwezi wa kuelezea utelezaji wa kazi za serikali kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.

“Sehemu kubwa ya ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro imeshatandazwa reli, nyaya za umeme na mwaka huu treni itaanza kufanya kazi,” alisema Dk Abbasi. Alisema ni jambo la ajabu kuona baadhi ya watu wanabeza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali.

“Mradi wa ujenzi wa reli ya SGR kutoka Morogoro hadi Makutupora, Singida haujawahi kukosa fedha wala kutatizwa kwa namna yoyote ile tofauti na uzushi wa wanasiasa kuwa serikali imekosa fedha kwa kipande cha Morogoro hadi Makutupora Singida,” alisema na kuwataka wananchi kuwapuza wanaobeza miradi inayotekelezwa na serikali.

“Kosoa kwa haki hii ni nchi ya kidemokrasia, usiongee uongo na kutukana serikali haijawahi kutishika wala kupata tashtiti wala jakamoyo ni jambo la kihistoria, wataongea lakini mwisho wa siku watalegea wenyewe,” alisema.

Alisema ujenzi huo mpaka sasa fedha zilizotumika sasa ni Sh trioni 2.957 na gharama za ujenzi mpaka utakapokamilika ni zaidi ya Sh trioni saba. Pia alisema zabuni ya ujenzi wa reli kutoka Mwanza hadi Isaka itatangazwa wakati wote kuanzia sasa.

Alisema leo kutakuwa na ziara ya siku mbili kwa makatibu wakuu mbalimbali kutembelea na kujionea ujenzi wa reli.

Alisema ziara hiyo itaanzia jijini Dodoma hadi Morogoro na kisha Morogoro kwenda jijini Dar es Salaam. Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere Kuhusu ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Maporomoko ya Maji ya mto Rufiji (JNHPP), Dk Abbasi alisema unaendelea kwa kasi ujenzi wake utakuwa wa awamu nne.

Alisema kazi ya handaki mtaro ina hatua tatu kuu ikiwemo kuchoronga handaki la kupitisha maji ya mto ambayo imekamilika kwa asilimia 100. Pia kuweka zege la kuimarisha handaki ambayo imefikia asilimia 10 ya ujenzi.

“Mpaka Januari 2020, fedha iliyotumika kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere ni trilioni 1.275,” alisema na kuongeza kuwa kujenga mageti ya kudhibiti kiasi cha maji yanayopita na hilo hufungwa pale yapoingilia maji ya handaki.

Mradi wa Umeme wa Maporomoko ya Mto Rufiji utakuwa na uwezo wa kufua umeme megawati 2,115 na ukubwa wa bwawa hilo ni kilometa za mraba 900 na likikamilika itaingizwa kwenye rekodi ya mabwawa 70 makubwa duniani.

“Ukianza kujenga bwawa lazima uchepushe mto, hatua ya kwanza imekamilika kwa asilimia 100, na yatachepushwa kama kilomita moja yatapita chini kwa chini na maji yatatokea chini ya mto, hii kazi ikiisha itaanza ya kuweka kingo ndani ya kuta za mto na tutashihudia tofali la kwanza la kujenga ukuta,” alisema.

Meli za Ziwa Victoria Pia alisema serikali iliahidi kuondoa adha kwenye ziwa Victoria kwa kujenga chelezo ambapo jumla ya Sh bilioni 32 zimeshalipwa. Alisema ujenzi huo ukikamilika utaruhusu meli kubwa kutia nanga.

Pia alisema ukarabati wa Mv Victoria unaendelea na zimeshatumika Sh bilioni 14 na utekelezaji umefikia asilimia 89 na ujenzi huo mpaka ukamilike utatumia Sh bilioni 22.

Pia alisema Mv Butiama inafanyiwa ukarabati mkubwa na sasa umefikia asilimia 86 na matengenezo yote yatagharimu Sh bilioni nne lakini mpaka sasa fedha zilizotolewa ni Sh bilioni tatu.

“Serikali imewekeza shilingi bilioni 80 kuund meli kubwa ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, mpaka sasa ujenzi wa meli hiyo uko asilimia 52 na tunatarajia itakamilika mwezi Septemba hadi Oktoba,” alisema.

Ripoti ya Haki za Binadamu Alisema katika kikao cha 43 Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Taifa kilichofanyika Februari 25, mwaka huu jijini Geneva nchini Uswisi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi aliwasilisha ripoti ya Tanzania kuhusu masuala ya haki za binadamu.

“Alielezea mafaniko ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kulinda na kusimamia haki za binaadamu na kutolea ufafanuzi wa sheria tatu zilizotungwa; tumeeleza nchi inavyotekeleza haki za binadamu katika mawanda yote - kisiasa, kijamii, kiuchumi na kimaendeleo,” alisema Dk Abbasi.

Ripoti ya AfDB Alisema ripoti ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ya mwaka 2020 imeitaja Tanzania kuwa moja ya nchi yenye mageuzi yanayogusa na kubadili maisha ya watu. Pia yaitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchizilizopiga hatua kubwa katika kupunguza umaskini.

Ripoti ya taasisi ya RMB ya 2020 Inaitaja Tanzania kuwa nchi ya 21 duniani ya nne kwa Afrika na ya kwanza Afrika Mashariki kwa kiwango cha biashara ndogo ndogo na uboreshaji wa shughuli za Wamachinga. Kwa Afrika Tanzania ni ya nne na kwa Afrika Mashariki ni ya kwanza.

Alisema Shirika la Habari la Kimataifa la CNBC Africa, juzi limerusha kwa zaidi ya nchi 100 duniani makala inayoeleza mafanikio ya Tanzania katika sekta mbalimbali iitwayo ‘Tanzania: The Soul of a New Africa.’ “Kwa Afrika Mashariki, Tanzania ni ya kwanza na kwa Afrika Tanzania ni ya nne,” alisema.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi