loader
Picha

Makahaba kupelekwa Chanika kulima

MANISPAA ya Ilala imekuja na mkakati wa kudhibiti biashara ya ngono, kwa kuwakamata na kuwawezesha kiuchumi wanawake wanaojihusisha na biashara hiyo.

Katika mahojiano yake na gazeti hili kuhusu kukithiri kwa biashara za ukahaba katika wilaya ya Ilala, Mkuu wa Wilaya hiyo, Sophia Mjema alikiri uwepo wa wanawake wanaojiuza katika wilaya yake kwa kisingizio cha ugumu wa maisha.

Alibainisha kuwa wilaya hiyo, imeshaanza mikakati ya kukabiliana na biashara hiyo. Alisema mahakaba hao watakamatwa na kuweka kwenye eneo moja lililopo Chanika, ambapo watakuwa wakilima na kuuza bidhaa mbalimbali.

Kwa kufanya hivyo, wanawake hao watajinasua katika biashara hiyo, ambayo ni kinyume na maadili ya Watanzania huku pia wakijipatia kipato halali. Alisema ofisi yake inakamilisha taratibu za kiutendaji katika kuliandaa eneo hilo la Chanika lililokwishaainishwa, ambapo kutakuwa na shughuli za kilimo, ufugaji na nyinginezo zitawajenga kiuchumi wanawake hao.

Alisema mchakato ukikamilika, wanawake ambao watakuwa wakikamatwa kujihusisha na biashara hiyo, watachukuliwa na kupelekwa moja kwa moja na kuwekwa kwa muda, wakifundishwa mbinu kadhaa za kujiendeleza kiuchumi.

Kuhusiana na kukithiri kwa biashara ya ngono, gazeti hili katika ufuatiliaji wake wa siku tatu majira ya usiku katika Wilaya ya Ilala, umebaini uwepo wa madanguro kadhaa hasa Tabata na Buguruni. Katika eneo la Tabata Barakuda, umbali mrefu kidogo nyuma ya baa ya The Great, kuna uwanja mkubwa wa kuegesha magari, ambao kuna vyumba vitatu vilivyojengwa kwa mabati.

Vyumba hivyo ni madanguro ambayo hutumiwa na wanawake wanaojiuza karibu na baa hiyo. Huwalipa walinzi wa madanguro hayo Sh 2,000 kwa kila mteja. Lakini, pia hata nyuma ya kituo cha basi cha Tabata Barakuda upande wa kuelekea Vingunguti, kuna danguro lililojengwa kwa mabati ambalo nalo pia hutoza Sh 2,000 kwa kila anayekwenda kutumia, huku wanawake wao hutoza Sh 10,000.

Pia katika eneo la Buguruni njia ya kutoka Tabata kuelekea Buguruni Chama, kuna sehemu wanauza mbao, ambapo kwa ndani kuna danguro ambalo hutumika kwa wadada wanaojiuza.

Lakini pia zipo nyumba za kulala wageni ambazo zimetengenezwa maalumu kwa shughuli hiyo, ambazo zinapatikana Buguruni Kimboka na Sewa, ambazo wadada wanaojiuza hupendelea kuwapeleka wateja wao hapo, huku bei ya muda mfupi (short time) ikiwa ni Sh 5,000.

Buguruni kuna eneo ambalo ni maarufu kama “Kwa Wahaya” ambapo nako kuna madanguro mengi, yanayotumiwa na wanawake hao kwa ajili ya shughuli ya kujiuza. Utitiri wa maeneo hayo, nao umechangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kwa biashara hiyo, ambapo wadau wameshauri yavunjwe.

KIWANGO cha mimba za utotoni kimeripotiwa kupungua kwa kasi katika ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi