loader
Picha

Madaktari Tanzania wajitolea kutibu homa ya corona China

SERIKALI ya China imeshukuru utayari wa Serikali ya Tanzania wa kutaka kuwapeleka madaktari nchini humo, kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid -19).

Aidha, imewatoa hofu Watanzania kuhusu changamoto za kibiashara na watalii kuingia nchini kutokana na kulipuka kwa virusi hivyo kuwa ni jambo la muda na vitaondoka muda si mrefu, hivyo kuwataka wafanyabiashara kuwa watulivu huku wakiwasiliana na wadau wao waliopo China.

Hatua hiyo imetokana na Rais John Magufuli, kumpa pole Balozi wa China nchini, Wang Ke kutokana na ugonjwa huo kuathiri kwa kiasi kikubwa nchi hiyo na kumueleza kuwa serikali iko tayari wakati wowote kupeleka madaktari kusaidia matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maambukizi ya ugonjwa huo, Balozi Ke alisema mbali na serikali kuwa tayari kupeleka madaktari, pia baadhi ya madaktari binafsi, waliandika barua kwa Balozi huyo, kuonesha nia na utayari wa kutaka kwenda kusaidia kutoa matibabu. Baada ya kuonesha utayari huo, aliwasiliana na serikali yake, waliopokea hatua hiyo kwa furaha na kueleza kwa wakati huu kuna madaktari wa kutosha 40,000 wa kutoa huduma, huku maambukizi ya virusi hivyo yakiendelea kupungua.

“Niliguswa sana pale Rais John Magufuli aliponiambia ‘kwa kuwa ndugu zetu wana uhitaji, tutapeleka madaktari kusaidia kupambana na virusi hivyo China wakati wowote’,”alisema.

Alieleza kuwa hatua hiyo ilionesha jinsi nchi hizo mbli, zilivyo na ushirikiano wa kudumu. Alisema kwa niaba ya serikali ya China, anashukuru utayari wa Tanzania kusaidia kupambana na ugonjwa huo.

Alisema kwamba nchi mbalimbali, zimekuwa pamoja na China kusaidia kukabiliana na ugonjwa huo. Balozi Ke alisema kuna nchi zimewapatia misaada ya kifedha, kuwapatia barakoa (mask) na nguo kwa ajili ya kujilinda na ugonjwa huo na vifaa mbalimbali. Alibainisha kuwa mpaka sasa, bado sababu za virusi hivyo, hazijagundulika kwani wanasubiri utafiti wa kisayansi.

Alitaka wafanyabiashara wa Kariakoo, wanaolalamikia mizigo yao kuzuiliwa nchini China kuwa wanatakiwa kutulia wakati tatizo hilo linaendelea kupungua na baadhi ya viwanda vya nchi hiyo kuanza uzalishaji, hivyo waendelee kuwasiliana na waliopo nje ya nchi.

Kuhusu usalama wa wananfunzi 400 waliopo katika jimbo la Wuhan, lililoathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa huo, alisema kuwa wako salama na serikali kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini China na vyuo wanavyosoma, wanaendelea kuwapatia huduma stahiki.

Alishauri kuwa ni salama, kuendelea kubaki katika jimbo hilo. Ke alitaja jitihada zilizosaidia kutokomeza virusi hivyo vipya duniani ni: Uongozi bora wa serikali, uliofanikisha kutoa taarifa za uwazi kwa ngazi zote, kujitoa kwa raia hususan wanasayansi na madaktari ambao 20 tayari wamepoteza maisha, njia za kisayansi kudhibiti ugonjwa huo na uwazi katika kupeleka taarifa.

Alishukuru jumuia za kimataifa kwa kusaidia kupambana na ugonjwa huo hatari. Alieleza kuwa hivi sasa China imeanza kudhibiti ugonjwa huo. Alitaka nchi za Afrika, kuungana kukabiliana na ugonjwa huo, unaosambaa kwa kasi duniani.

Wagonjwa wengine wamebainika katika hatua za mwisho kwa kutoonesha dalili. Alibainisha kuwa hivi sasa ushirikiano wa China na Tanzania, unaendelea kwenye miradi na uwekezaji, licha ya kuwepo changamoto katika biashara na utalii kutokana na ugonjwa huo.

“Matokeo haya mabaya ni ya muda. Tunaamini kuwa ugonjwa huu unazidi kupungua na uzalishaji utaendelea kama kawaida. Ushirikiano na urafiki kati ya watu wa nchi hizi mbili utaimarika zaidi,”alisema.

Daktari Mkuu Mshiriki katika Hospitali ya Nanjing China, Dk Li Ping alibainisha kuwa mpaka jana maambukizi ya watu 12,000 yamedhibitiwa nchini China huku kukiwa na vifo 3,051. Waliopona ni 52,109 na wengi wa waliokufa ni wazee kuanzia miaka 60 na kuendelea.

Alibainisha kuwa watoto hawaathiriki. “Makundi yanayoathirika zaidi ni wazee wa kuanzia miaka 60 na walio na magonjwa sugu. Watoto wanaambukizwa kwa nadra, lakini dalili za ugonjwa kuchelewa kuonekana ndizo zinasababisha maambukizi kwa kiwango kikubwa,”alisisitiza.

Alipinga uvumi mbalimbali unaohusishwa na ugonjwa huo. Kwa mfano kuwa wako wanaosema “Unywaji wa maji moto huua virusi hivyo, kula vitamini C, kuvaa barakoa nyingi kuzuia ugonjwa, kutumia dawa za bakteria kuzuia maambukizi hayo au suala la wanyama wafugwao kueneza virusi”.

Alisema dalili za ugonjwa huo ni homa, kikohozi kikavu, uchovu, kiwango kidogo cha makohozi, ugumu wa kupumua, maumivu ya koo, pua kuziba na pua kutoa majimaji. Dalili hizo huonekana siku tano mpaka sita.

Alitaka wananchi kujikinga na ugonjwa huo, kwa kuosha mikono kwa kemikali au sabuni. Alisema kufanya hivyo kutapunguza athari. Alisema kugusa shavu baada ya kugusa sehemu ya maambukizi, husababisha kupata maambukizi.

Alitaja mbinu zingine za kujikinga kuwa ni:Kuacha madirisha wazi kupata hewa iingie na kutumia dawa kusafisha vitu vya ndani kama meza, viti na dawati. Mtu anapokohoa au kupiga chafya, ajifunike na kitambaa au karatasi na kisha kunawa mikono.

Alisema kutokana na virusi hivyo, kuambukizwa kwa njia ya matone ni vema kuwa mbali na watu kwa mita moja. Ikitokea una maambukizi, ni vema kuvaa barakoa unapotoka nje.

KIWANGO cha mimba za utotoni kimeripotiwa kupungua kwa kasi katika ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi