loader
Dstv Habarileo  Mobile
SAMIA SULUHU HASSAN Aelezea milima na mabonde hadi Umakamu wa Rais

SAMIA SULUHU HASSAN Aelezea milima na mabonde hadi Umakamu wa Rais

ALIZALIWA katika familia ya kawaida ambayo baba yake alikuwa mwalimu na mama yake alikuwa mama wa nyumbani. Hakuwa amesoma sana. Alianza kazi akiwa ofi sa masjala.

Alionja joto ya jiwe ya mwanamke kugombea ubunge wa jimbo kwa kupewa majina ya ‘ajabu’, matusi, kejeli na dhihaka. Hakutarajia kama angeshika wadhifa wa juu katika nchi.

Huyu si mwingine, bali ni Mama Samia Suluhu, mwanamke wa kwanza nchini kushika wadhifa wa Makamu wa Rais. Simulizi hii ya maisha yake aliitoa hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanafunzi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 43 ya CCM.

Akiwa mwanamke anayetoka familia ya kawaida ambayo baba yake alikuwa mwalimu na mama yake ni mama wa nyumbani, anaeleza alivyoanza kupata elimu yake akisema hakusoma sana. Alisoma hadi kidato cha nne na hakufanya vizuri.

Alihitimu kipindi ambacho mwanafunzi akimaliza shule alikuwa anapangwa; wakati wa kipindi ambacho wataalamu walikuwa wakitafutwa. Alipangwa kwenda Ofisi Kuu ya Maendeleo wakati huo akiwa na umri wa miaka 16 na miezi saba na alipofika, mwajiri alisema hawezi kumwajiri kwani itakuwa ni kutoa ajira kwa mtoto.

“Nikarudishwa nyumbani (shida ya kusoma haraka haraka). Nikarudishwa hadi nilipofikishwa miaka 17 na miezi kama sita hivi nikaambiwa njoo. Nikaanza. Nilianza Ofisi ya Masjala,” anasema.

Alifanya kazi kwenye ofisi ya masjala kwa miaka mitatu na kwamba alikuwa mwenye kasi na juhudi ya kazi. “Kila nikifanya ile kazi nakuta niliowakuta nawaongoza mimi. Wakubwa wakitaka kitu, wananiita na kuniambia wanataka hiki na hiki na haraka najua kilipo.” Alichozingatia ni kusoma mazingira yaliyomzunguka na kujua mila na desturi za taasisi.

Alihisi anahitaji kuwa mahali pengine zaidi na ndipo alianza kujisomesha kwa kufanya kozi ya takwimu ngazi ya cheti. Baada ya hapo, alichukua kozi ya Uongozi ngazi ya cheti na kujiongezea sifa.

Kisha alikwenda Chuo cha Usimamizi wa Maendeleo (IDM) Mzumbe alipochukua Stashahada ya Juu ya Uongozi wa Umma kwa miaka mitatu na mwaka 1987 alirudi ofisini kuendelea na kazi kwa mtindo wake wa kasi kubwa akiwa Ofisa Mipango. Baada ya miaka miwili, zilitangazwa kazi kwenye Umoja wa Mataifa akaomba. Alifanyiwa usaili na kupata kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) ambako alifanya kwa miaka tisa na kisha kurudi serikalini.

“Nikaangalia serikalini nikaona watu wanakwenda pole pole nikachomoka nikaenda kwenye NGO… nikawa kiongozi pale Zanzibar,” anasema Samia.

Anasema wakati akiongoza, hawakuwa na fedha jambo ambalo ilipotokea mikutano ya kwenda nchi za nje kama vile Afrika Kusini, Zimbabwe walisafiri kwa mabasi badala ya ndege. Alianza kufikiria namna ya kupata fedha ndipo akapata Action Aid ambako alipeleka wazo lake na kupata fedha. Hata hivyo, anasema kwenye fedha lazima yawepo maneno.

Baada ya NGO yao kupata fedha yalianza maneno jambo lililomfanya aachane nayo na kuingia upande mwingine. Alivyoanza siasa Mwaka 2000 aliingiwa na hamu ya masuala ya siasa.

Anasema visiwani Zanzibar kuna Baraza la Wawakilishi ambalo lilikuwa moto kati ya upinzani na CCM. “Hasa ukisikiliza Baraza unahisi kwamba upinzani wanatuzidi.

Unamsikia waziri anajibu ambacho sicho. Nikasema ngoja nitaingia huko huko hao mawaziri wanaojibu ndivyo sivyo tutaonana.” Hata hivyo, hakujua ni namna gani ataingia kwenye siasa.

“Nikauliza. Nikaelekezwa. Nikaambiwa unafanya hivi, subiri mwezi huu fomu zitatolewa utajaza. Nikapata watu wakanishika mkono. Nikaenda wakanielekeza jaza leo twende tume,” alifafanua.

Anaongeza, “sijui kabisa siasa. Mimi ni ‘activist’ (mwanaharakati) lakini moyoni kwangu siasa ninayo. Yanayotokea kule yananiuma. Nikaenda hivyo mpaka siku ya uchaguzi viti maalumu .”

Anasema siku ya uchaguzi mkoani kwake, watu wali- kuwa wakimshangaa lakini alijieleza mpaka akakubalika. “Basi walinikubali wakanichagua. Furaha yangu haikuwa kifani.

Nikasema sasa mawaziri wanaojibu hovyo watanijua mimi ni nani. Nikasubiri tu baraza liitwe nikafanye vitu vyangu,” alibainisha. Baada ya kuapishwa wakasubiri na katika kupanga serikali, akaingizwa kwenye baraza la mawaziri. “Nikasema mimi mbona sikutaka hili nilitaka lile, nilitaka niingie nikawasute wale. Sasa nakwenda kusutwa mimi. Nikawaza kuwa waziri ni kuwa nani? Kichwa kikaniuma.”

“Halafu hilo liwizara nililopewa limekatwa vipande nikaliunge mwenyewe. Nikasema mbona hilo liwizara kubwa? Rais akasema kama umeliona kubwa unajua cha kwenda kufanya. Kwa hiyo nikaanza kazi yangu kama Waziri wa Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake na Watoto,” alieleza Makamu wa Rais.

Aliongoza wizara hiyo kwa kipindi chote cha miaka mitano tangu mwaka 2000 na 2005 aligombea tena uwakilishi wa viti maalumu. Katika kupanga serikali, alipewa Uwaziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji aliyoiongoza kwa miaka mingine mitano.

“Sikuwahi kubadilishwa wizara,” anasema. Ubunge jimboni Baada ya kutumikia vipindi viwili vya uwakilishi, anasema alijiona ameiva hivyo akaona ni wakati wa kugombea jimboni.

Kwa bahati jimbo la kijijini kwake (Jimbo la Makunduchi), mbunge aliyekuwapo alisema haendelei hivyo ikawa fursa kwake. Anasimulia kashfa na matusi aliyopokea wakati akigombea ubunge wa Jimbo la Makunduchi visiwani Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 baada ya kutumikia viti maalumu vya baraza la wawakilishi kwa vipindi viwili.

“Hapo nilionja joto ya jimbo ndugu zangu, kuwa mwanamke na kwenda jimboni. Kwa sababu huko kwenye viti maalumu ni hatua ambayo ni lazima serikali ifanye na mnashindanishwa wanawake kwa wanawake. Lakini sasa unakwenda kwenye jimbo…mwanamke peke yangu,” anasema. Anaongeza, “jina la kwanza wali-

NYOTA HABARILEO JUMAPILI MACHI 8, 2020 NYOTA

• Alianzia kazi Masjala, akaonja joto ya jiwe jimboni • Asimulia alivyolia alipopitishwa mgombea mwenza lonipa wanaume ni ‘kigego’; Huyu mwanamke kigego… yeye kaona wapi jimbo hili wakaja wanawake? Nikasema nyie twendeni hivyo hivyo.

Nipeni majina yote,” haya ni sehemu ya maelezo ya Mama Samia akielezea alivyoingia katika kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo kwa mara ya kwanza.

“Hapo niliona joto ya jimbo ndugu zangu, kuwa mwanamke na kwenda jimboni. Matusi ya wanaume, kashfa … Hayo yapo. Basi unanyamaza tu…cha msingi ni kujiheshimu na moja kati ya mambo ya kujiheshimu ni, ukitukanwa usirudishe. Nyamaza. Nyamaza wewe kuwa chanya fanya yale mazuri unayotakiwa kufanya,” anasema Makamu wa Rais.

Anasema hakujali kubezwa wala matusi aliyokuwa akipewa. Alipambana sambamba na kuendana na mila na desturi za eneo husika. Aliwatumia wanawake, akawaelimisha na kuwaambia umuhimu wa kuwa na kiongozi mwanamke. Anasisitiza kuwa jambo la msingi ni mwanamke kujiheshimu. Katika kudhihirisha heshima yake alipotukanwa hakurudisha neno bali alinyamaza.

“Nyamaza, wewe kuwa chanya fanya yale mazuri unayotakiwa kufanya. Mwisho watajikuta wanajitukana wenyewe, wanayemtukana hana habari,” alieleza.

Alishinda kinyang’anyiro hicho akawa Mbunge wa Makunduchi; ikawa fursa yake kutoka Zanzibar na kuja Bara na kuingizwa kwenye Baraza la Mawaziri akiwa Waziri Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais kwa miaka mitano. Baada ya miaka mitano ya ubunge jimboni, alianza kujiandaa kwa miaka mitano mingine ingawa anakiri kwamba vita ilikuwa kubwa.

“Sijui wangenitoa?,” anasema Mama Samia ambaye katika Bunge la Katiba alikuwa Msaidizi wa Spika, hayati Samuel Sitta. Anazungumzia bunge hilo, Mama Samia anasema hakuwahi kuona Bunge gumu. Hata hivyo, anasema kupitia Bunge hilo alionesha kuwa mwanamke anaweza. Suala kubwa analosisitiza ni heshima.

“Watu wakitukana unakuwa mtulivu, wanapiga kelele unakuwa mtulivu, unawapoza, unasimama katikati. Unafanya kazi yako, hujishushii heshima. Tulikwenda vizuri Bunge lilikwisha,” anasema.

Akizungumzia matayarisho yake kurudi jimboni kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Mama Samia anasema, “hapa ndipo nakuambia kuna mkono wa Mungu. Samia Suluhu hakutarajiwa kabisa kuwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.”

“Nilikuwa nasubiri tumalize mchakato nikazame zangu jimboni nipambane. Lakini kwa baraka ya Mungu nadhani wazee viongozi wamechekecha huko, kwanza walifanya uamuzi kwamba akiwa rais mwanamume, mwanamke awe makamu … ndugu zangu sielewi lilitokea wapi.”

Akisimulia siku alipotajwa Makamu wa Rais, Mama Samia anasema, “mimi nilikwenda zangu kwenye ukumbi nimevaa guo langu la njano zito na tandio kubwa kwa sababu siku iliyopita nilikaa kwenye mkoa wangu na ilikuwa kwenye geti na baridi yote inanipiga yote nikasema kesho naikomesha baridi. “Nikakaa zangu kwenye kiti. Shughuli inataka kuanza akapita Mjumbe wa Halmashauri Kuu akasema mheshimiwa mbona uko hapa nikasema tupo kwenye mikoa yetu.

Akasema hapana wajumbe wa Kamati Kuu tuko kule juu nyanyuka twende nikasema sikujua. “Nikamfuata. Lakini siko comfortable nilivyovaa kujipeleka kule kwenye Kamati Kuu. Nikasema ngoja niende. Shughuli zimekwenda tumepata mgombea. Sasa Kamati Kuu turudi ndani tukatafute mgombea mwenza. Basi tumeingia, mkiingia Kamati Kuu wadogo wadogo mnaachwa, vingunge wanaingia kwenye chumba. “Wastaafu na viongozi waliokuwapo wanaingia chemba nyingine.

Nyie wengine mnabaki mnapiga biskuti na kahawa mnasubiri kusikia huko kuna nini. Basi tunachokozana tunataniana. Mara tukaona wakubwa wametoka, moshi mweupe tayari tukarudi kwenye viti haraka.

“Tukakaa tukaona wamerudi tena. Nilikuwa naongoza kuchokoza na kutania watu. Walipomaliza Rais Kikwete (Jakaya) nikaona anakuja akavuta kiti. Akasema mgombea (Dk John Magufuli) anasema atafanya kazi na Samia. Mimi nikasema ‘siwezi siwezi’ wakaniambia utaweza. Makamu wa Rais, Dk Bilal akanishika mkono akasema dada utaweza, nitakusaidia.

Kilio alipopitishwa “Ujasiri ukanishinda nikaanza kupiga kilio. Basi Rais Kikwete akasema wanawake kwa kulia lia. Nenda kaoshe uso huko twende. Nikaingia, kuna kibeseni nikaosha uso tukaenda.”

Anashangaa waandishi wa habari walivyopata taarifa akisema, “tangu natoka wana makamera wananionesha na macho yangu mekundu na guo langu na tandio langu.

Sasa ndugu ningejua kuna kitu kinatokea, ningeviweka vitu vya kweli kweli mngenijua. Lakini wala sikuwa najua,” alieleza Makamu wa Rais. “Sasa wenyewe jiulizeni ilikuwaje? Sijui wanawake wangapi tulizungumzwa huko ndani? Wazee wakasema ni huyu na Mungu akaweka mkono wake. Hiyo ndiyo historia ya mimi mama yenu,” Mama Samia anawaeleza wanachuo hao wa UVCCM Tawi la UDSM.

Anahitimisha kwa kusema, “naweza kusema kwamba kuna wanawake mahiri, wamesoma zaidi kuliko mimi, pengine wana heshima kuliko mimi na sifa zaidi kuliko mimi… lakini na mkono wa Mungu ulikuwapo. Kama hupendi Samia awepo muheshimu Mungu basi.”

Awapa wanawake neno Mama Samia ambaye ni mama wa watoto wanne; wavulana watatu na msichana, ana neno la kuwapa moyo hususani wanawake viongozi kutokana na changamoto mbalimbali zinazowazunguka ikiwamo za malezi.

Akizungumza hivi karibuni mjini Dodoma wakati akizindua Mtandao wa Wanawake Viongozi kwa Bara la Afrika, Tawi la Tanzania (AWLN), alisimulia alivyokuwa na muda mchache wa kukaa na kuwapa upendo wa watoto wake kiasi cha binti yake kujuta. “Nilimpeleka Uganda kusoma. Akirudi mimi sipo. Huyo duniani nahangaika na shuguhuli za serikali. Nilikuwa na muda mchache naye,” anasema.

Kwa mujibu wa Mama Samia, siku moja mtoto huyo aliwaeleza watoto ambao mama yao alikuwa karibu akisema, “heri yenu nyie wenzangu mama yenu mnamuona. Sisi mama yetu katuzaaa anatutupa. Nilijihisi mkosa.

“Ilinichukua muda kutoka kwenye moyo wangu kweli. Hawanioni ni pesa tu inafanya kazi. Wakati pesa si kitu. Watoto wanataka upendo wa mama. Huyo ni mtoto kafika kusema hivyo. Baba yake anasemaje? (wajumbe walianguka kicheko na kushangilia). Lakini uzuri akina baba wana cooping mechanism (mbinu za kukabili matatizo). Hata hivyo, anasema kilichotokea ni kwamba, huyo binti yake sasa na yeye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, na miongoni mwa wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Niliyofanya naye anafanya vile vile. Cooping mechanism yake ni kunipa watoto wake. Akasema anajuta kusema hayo maneno. Hayo ndiyo yanayotuzunguka viongozi wanawake.”

Tusijisikie wakosaji Anashauri wanawake wanaokutana na changamoto kama hii wasihisi woga au wakosaji bali wajenge taifa, waridhishe wenza wao na maisha yaendelee. Kwa upande wa kazi, anausia wanawake akisema ili wasimame vyema kwenye nafasi zao inabidi wawe na mambo kadhaa ikiwamo umahiri.

Anasema kawaida ya mwanamke haachi kushughulika na undani wa jambo analolikuta popote. Anachoona anataka kukijua kwa undani. Anasema roho hiyo ikitumika vyema kazini, watakuwa mahiri, wadadisi na kufanya wawe na ufanisi. Anahimiza pia wanawake kuwa shupavu na kujiamini kwa maana ya kuongea na kuamini wanayosema.

Anahimiza pia wanawake kuongeza maarifa katika maeneo ya fani zao walizosomea. Mama Samia ni nani? Wasifu unaonesha alizaliwa Januari 27, 1960 visiwani Zanzibar.

Alisoma shule za msingi za Chawaka (Unguja), Ziwani (Pemba) na Mahonda (Unguja) kati ya mwaka 1966 na 1972. Alisoma sekondari Ngambo, Unguja (1973-1975) na Lumumba, Unguja (1976). Alisomea kozi mbalimbali hadi akafikia kupata Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire nchini Marekani.

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi