loader
Hofu pambano Yanga, Simba

Hofu pambano Yanga, Simba

KUELEKEA kwenye mchezo wa watani wa jadi leo, Kocha wa Yanga, Luc Eymael ameonesha kuwahofia wachezaji Luis Miquissone, Francis Kahata na Meddie Kagere wa Simba utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ni wa marudiano na Yanga ndio wenyeji baada ya ule wa kwanza uliochezwa Januari 4 na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Akizungumza jana, Eymael alisema maandalizi ni mazuri na leo (jana) walifanya mazoezi na kwenye mchezo wa watani wa jadi, lolote linaweza kutokea na kukiri Simba kuwa na wachezaji wazuri kama Kagere, Kahata na Luis.

Naye kocha wa Simba, Sven Vandebroeack alisema wapo tayari kwa mchezo huo isipokuwa watawakosa wachezaji Miraji Athuman na Said Ndemla ambao ni majeruhi.

“Nategemea hali ya hewa kesho (leo) itakuwa nzuri kutaturuhusu kucheza mpira na kufurahia mchezo. Tutacheza mchezo wa kweli, kwani tunawajua wapinzani wetu na tumejiandaa kuchukua alama tatu na kusonga mbele ili mwisho wa msimu tuwe mabingwa,” alisema Sven.

Naye nahodha wa Simba, John Bocco alisema wamejiandaa vizuri kwa mchezo na kuwaahidi mashabiki kujituma kwa muda wote wa mchezo.

“Sisi wachezaji tumejiadaa vizuri kwa mchezo wa kesho (leo). Tunaahidi kucheza mchezo wa kujituma ili tuwafurahishe mashabiki wetu ili tupate alama zote tatu,” alisema Bocco.

Naye nahodha wa Yanga, Juma Abdul alisema watafuata kile ambacho kocha atakacho waelekeza na wamejiandaa vizuri kimbinu, kiufundi na kisaikolojia.

“Sisi wachezaji tumejiandaa vizuri na tutafanya kile kocha atakachotuelekeza ila kuhusu matokeo tunamwachia Mungu,” alisema Abdul.

Katika mchezo wa kwanza, Simba ilitangulia kupata mabao mawili, ambayo yalifungwa na Meddie Kagere kwa mkwaju wa penalti baada ya kufanyiwa faulo na beki wa Yanga, Kelvin Yondani na jingine likifungwa na Deo Kanda.

Yanga wakasawazishia kipindi cha pili mfungaji akiwa Balama Mapinduzi na wa Simba Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alijifunga. Mchezo wa leo kuna baadhi ya wachezaji unaweza kuwa mchezo wao wa kwanza kama watapewa nafasi ya kucheza na makocha wao, kwa Yanga yupo Bernard Morisson ambaye amesajiliwa Yanga akitokea Vita Club ya DRC, lakini pia amewahi kucheza Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Morison tayari ametokea kuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, kutokana na staili yake ya kutembea juu ya mpira.

Pia kwa Yanga yupo David Molinga, japo alikuwepo tangu mwanzo mwa msimu huu kwa bahati mbaya hakucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Simba, kwani hata kwenye wachezaji wa akiba hakuwepo na kocha Eymael akimpatia nafasi huo utakuwa mchezo wake wa kwanza dhidi ya Simba.

Tariq Seif ambaye alisajiliwa kama mchezaji huru, dirisha dogo la usajili baada ya mpango wa kucheza soka la kulipwa Misri kushindikana, kama kocha wake atampanga mshambuliaji huyu chipukizi, huo utakuwa mchezo wake wa kwanza dhidi ya Simba na amekuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye mechi za Yanga hivi karibuni.

Erick Kabamba alikuja kufanya majaribio wakati wa dirisha dogo akitokea Zambia na uwezo wake ukamshawishi aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Said Maulidi ambaye alikuwa akiisimamia timu hiyo wakati huo, hivyo kama atacheza leo huu utakuwa mchezo wake wa kwanza dhidi ya Simba.

Kwa upande wa Simba yupo Luis Miquissone ambaye amesajiliwa akitokea Ud Songo ya Msumbiji, ambako alikuwa kwa mkopo akitokea Mamelody Sundown ya Afrika Kusini.

Miquissone tayari ametokea kuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi, na Jumapili iliyopita aliifungia timu yake mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC ya Kinondoni na kufikisha mabao matatu kwenye ligi tangu aanze kuichezea timu hiyo.

Endapo kocha Sven Vanderbroeck atampatia nafasi ya kucheza leo, basi huo utakuwa mchezo wake wa kwanza dhidi ya Yanga. Pia Gerson Fraga aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu, lakini uwepo wa Mkude katika nafasi ya kiungo mkabaji kunamfanya akose nafasi ya kucheza kwenye mechi dhidi ya Yanga iliyochezwa Januari 4.

Mchezo wa leo ambao utachezeshwa na waamuzi sita, utashuhudiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad ambaye atakuwa na ziara ya siku tatu nchini.

Waamuzi watakaochesha ni Martin Saanya kutoka Morogoro ambaye atakuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga na Frank Komba wa Pwani wakati mezani atakuwepo Elly Sasii wa Dar es Salaam. Katika kuhakikisha hakuna malalamiko kwenye mchezo huo na kuongeza ubora nyuma ya kila goli kutakuwepo mwamuzi mmoja ambao ni Abdallah Mwinyimkuu wa Singida na Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam.

Mtathimini wa waamuzi atakuwa Sudi Abdi kutoka Arusha na Kamishna wa mchezo ni Mohamed Mkweche kutoka Dar es Salaam. Huu utakuwa mchezo wa pili kwa hapa Tanzania kutumia mfumo wa waamuzi sita, kwani kwani mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2019 wakati wa mechi za hatua ya robo fainali ya michuano ya AFCON U-17 iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Viingilio katika mchezo huo wa leo VIP ni Sh 30,000 wakati VIP B ni Sh 20,000 wakati mzunguko ni 7,000.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/997883e2f20f498ee4b9026291609f92.jpg

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi